In Summary

Jezi rasmi za AFCON, zilizozinduliwa mapema wiki hii, zitauzwa Ksh 3,500 na zitapatikana kwenye mtandao wa FKF na duka la vifaa vya michezo la Nairobi (Nairobi Sports House).
 

KATIKA kuhakikisha timu ya taifa Harambee Stars, inapata sapoti ya kutosha katika makala haya ya 32 ya Kombe la Mataifa ya Afrika, ambayo yataanza kutimua vumbi Juni 21, Shirikisho la Soka nchini (FKF), imeanza kuuza jezi za Stars mtandaoni ili kuwafikia wakenya wengi.
Kwa mujibu wa taarifa ya FKF, ambayo imefafanua namna ya kujipatia jezi hizo, ni kwamba jezi rasmi za AFCON, zilizozinduliwa mapema wiki hii, zitauzwa Ksh 3,500 na zitapatikana kwenye mtandao wa FKF na duka la vifaa vya michezo la Nairobi (Nairobi Sports House).
Aidha, mashabiki pia watapata fursa ya kutinga jezi za Stars za zamani kwa kiasi cha Ksh 2,500. Hii inakuja saa chache kabla vijana wa Migne hawajajitosa uwanjani kukabiliana na DR Congo, katika mchezo wa mwisho wa kirafiki, kabla ya kwenda Cairo.
Mchezo huo, utapigwa kuanzia saa 2 usiku,  jijini Madrid, Hispania. Baada ya hapo, Juni 19, Harambee Stars, inavunja kambi ya mazoezi ya wiki tatu, iliyokuwa imeweka huko Paris, na kuelekea Cairo, ambapo Juni 23 itaanza kampeni yake dhidi ya Algeria.
Kulingana na taarifa hiyo, mashabiki ambao wangependa kununua jezi hizo kwa njia ya mtandao, watatuma muamala kwa njia ya Lipan a M-pesa, ambapo hivi karibuni wataweza kutumia Airtel Money, PayPal, VISA na MasterCard.
Kenya iliyokatia tiketi ya kushiriki fainali za mwaka huu, chini ya ukufunzi wa Sebastien Migne, iko kundi C, pamoja na majirani zao Tanzania, Algeria na Senegal. Juni 27 Stars itamenyana na Tanzania kabla ya kumalizana na Senegal, Julai Mosi.
 

ADVERTISEMENT