In Summary

Kama haitoshi Barcelona ilichapwa kwenye fainali ya Copa del Rey kumetibua msimu wao na hivyo wanataka kujipanga upya hasa ukizingatia wapinzani wao Real Madrid wanashusha vyuma tu huko Bernabeu.

BARCELONA, HISPANIA.KOCHA wa Barcelona, Ernesto Valverde amejifungia ofisini kwa muda wa saa tatu na mabosi wa timu hiyo wakijadili hatima ya viungo wawili, Philippe Coutinho na Ivan Rakitic.

Kikao hicho na mabosi kilifanyika Jumanne iliyopita, ambapo jambo kubwa alilotaka kufahamu kocha ni kuhusu mambo ya kiufundi hasa katika kipindi hiki cha usajili.

Licha ya kushinda taji la Ligi Kuu ya Hispania ‘La Liga’, kukomea kwao kwenye nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kutolewa kinyama na Liverpool.

Kama haitoshi Barcelona ilichapwa kwenye fainali ya Copa del Rey kumetibua msimu wao na hivyo wanataka kujipanga upya hasa ukizingatia wapinzani wao Real Madrid wanashusha vyuma tu huko Bernabeu.

Na sasa wababe hao wa Nou Camp wanachofikiria ni kuwafunguliwa milango ya kutokea viungo wake wawili, Coutinho na Rakitic. Mastaa hao wote wawili wamehusishwa na mpango wa kutimkia kwenye Ligi Kuu England, ambapo Manchester United ikiripotiwa kuhitaji huduma zao.

Valverde anaamini Rakitic bado ana kitu anachoweza kukifanya kwenye kikosi hicho na pia hataki kumpoteza Coutinho licha ya kucheza chini ya kiwango msimu uliopita.

Kitu ambacho Valverde anakifanya kwa sasa ni kuwasikiliza tu wanavyotaka mabosi hasa ukizingatia kiungo Arthur na Arturo Vidal walisajiliwa bila ya mapendekezo yake yeye.

Tayari Barcelona imeshamsajili kiungo mwingine wa kimataifa wa Uholanzi, Frenkie de Jong kutoka Ajax.

ADVERTISEMENT