In Summary
  • Yote yafanyike, lakini suala la Coutinho kwenda kujiunga na Man United hakika litawakera sana mashabiki wa timu hiyo.

BARCELONA, HISPANIA.UNAAMBIWA hivi Manchester United itabidi wajilaumu wenyewe tu kama watashindwa kumnasa kiungo wa Kibrazili, Philippe Coutinho kutoka Barcelona baada ya staa huyo kutuma ujumbe kwa wakali hao wa Old Trafford waende kumchukua.

Ripoti zilizofichuliwa wiki iliyopita zimedai kiungo huyo wa zamani wa Liverpool yupo tayari kwenda kujiunga na Man United kuondoka Barcelona, mahali ambako amekuwa akikumbana na wakati mgumu.

Dili hilo limedaiwa linaweza kukamilika kwa Pauni 100 milioni.

Barcelona ilimnasa staa huyo kwa Pauni 142 milioni Januari mwaka jana, lakini ameshindwa kufanya kweli huko Nou Camp na sasa jina lake linahusishwa na mpango wa kuondoka kwenye timu hiyo.

Mambo ni magumu baada ya Barcelona kumnasa Frenkie De Jong, ambaye bila shaka msimu ujao atakuja kukamatia sehemu ya kiungo kwenye kikosi hicho cha Nou Camp.

Yote yafanyike, lakini suala la Coutinho kwenda kujiunga na Man United hakika litawakera sana mashabiki wa timu hiyo. Jambo hilo litaifanya Liverpool kupoteza mamilioni ya pesa kwa sababu mkataba wake na Barcelona ni kwamba ingekuwa ikilipwa Pauni 4.4 milioni kila atakapocheza mechi 25 kwenye La Liga na itakuwa hivyo hadi zifike mechi 100.

Hadi sasa Coutinho amecheza mechi 43, hivyo akifika 50 tu kuna mkwanja unaingia Liverpool, lakini sasa suala la kwenda Man United litawatibulia wababe hao wa Anfield kupata mamilioni yao.

ADVERTISEMENT