In Summary

Makala hii inakuletea sababu zilizowapa nafasi Kagera na Mwadui kubaki Ligi Kuu msimu ujao pamoja na matukio yaliyojitokeza kwenye michezo hiyo iliyopigwa kwenye mikoa ya Kanda ya Ziwa na kuwa burudani ya aina yake kwa mashabiki wa soka wa ukanda huo.

MWANZA . KWISHNEI. Zile dakika 180 za mechi za play-off zilimalizika wikiendi iliyopita kwa timu za Kagera Sugar na Mwadui kusalia katika Ligi Kuu Bara na kuziacha Pamba na Geita Gold FC zikiumia vidole kwa kuikosa kiduchu.

Timu hizo nne zilionyeshana ubabe katika kusaka nafasi ya kuwa kwenye Ligi Kuu Bara msimu wa 2019-2020, lakini walikuwa ni Mwadui na Kagera waliotumia uzoefu kuwazima wapinzani wao na kusalia kwenye ligi hiyo yenye timu 20.

Licha ya Pamba na Geita kutakata, lakini haikuwa kazi ndogo kutokana na ushindani waliokutana nao kutoka kwa wapinzani wao wanaoshiriki Ligi Daraja la Kwanza (FDL).

Hata hivyo matokeo hayo yalipokewa kwa hisia tofauti kutokana na matarajio ya baadhi ya mashabiki walioamini huenda timu moja kati ya Kagera au Mwadui ingeaga Ligi Kuu.

Makala hii inakuletea sababu zilizowapa nafasi Kagera na Mwadui kubaki Ligi Kuu msimu ujao pamoja na matukio yaliyojitokeza kwenye michezo hiyo iliyopigwa kwenye mikoa ya Kanda ya Ziwa na kuwa burudani ya aina yake kwa mashabiki wa soka wa ukanda huo.

UZOEFU WAZIBEBA KAGERA, MWADUI

Moja ya sababu kubwa ya Kagera na Mwadui kubaki Ligi Kuu ni uzoefu kutokana na jinsi zilivyocheza kwa kujiamini dakika zote 180.

Licha ya Geita na Pamba kuonyesha uwezo na ushindani mkubwa hadi dakika za mwisho, lakini kukosa uzoefu wa mashindano yenye presha ndiko kulikowagharimu na kuzikosa Simba na Yanga Ligi Kuu msimu ujao.

Tulishuhudia kazi nzuri ya nyota wa timu za Ligi Kuu, Ally Ramadhan na Japhet Makarai (Kagera) na straika Salimu Aiyee (Mwadui) waking’ara na kuonyesha uwezo binafsi kuendelea kuzibakiza timu zao TPL.

NGUVU YA MASHABIKI

Baada ya mechi za awali kumalizika kwa suluhu, timu hizo zilienda kujipanga kwa michezo ya marudiano, huku kila moja ikitaka kubebwa na mashabili wao.

Ilishuhudiwa Uwanja wa Kaitaba mashabiki wakijaa vya kutosha majukwaani kuipiga tafu Kagera Sugar sawa na ilivyokuwa Mwadui Complex walikoishangilia timu yao. Hali hiyo iliwapa presha kubwa Pamba na Geita kufurukuta ugenini na kushindwa kufikia malengo yao, kwani mashabiki wao walikuwa wachache ikilinganishwa na wenyeji.

Sapoti kubwa ya mashabiki kwa Kagera na Mwadui iliwapa hamasa wachezaji, huku timu zikicheza kama zina deni kwao kwa kuhakikisha wanawapa raha.

MECHI KUAHIRISHWA

Moja ya tukio litakalodumu vichwa ni mwa mashabiki wa soka ni kuahirishwa kwa michezo ya play-off dakika chache kabla ya mechi kuanza jambo ambalo liliwashangaza wengi.

Mechi za awali zilipangwa kuchezwa Juni 2, lakini katika hali ya sintofahamu ilikuja taarifa kutoka Bodi ya Ligi (TPLB) kuahirisha michezo hiyo kwa madai ya usalama.

Hata hivyo kabla ya taarifa hiyo, mapema timu za Daraja la Kwanza zilianza kuvutana na wafanyakazi wa kituo cha Azam TV kuhusu kurusha mechi hizo mubashara.

Moja ya sababu za viongozi wa timu hizo kutotaka kurushwa mechi hizo ni kutokana na kutokuwapo kwa makubaliano, huku uongozi wa Pamba ukitishia kuwapeleka mahakama ya biashara iwapo watalazimisha kuonyesha ‘live’ mechi yao.

Baada ya mvutano huo uliodumu kwa muda na baadaye kuafikiana, timu zilianza kujiandaa kuingia uwanjani, huku wadau na mashabiki wakisubiri kwa hamu kandanda, zikaja taarifa za kusogeza mechi hizo hadi siku iliyofuata.

Mechi hizo zilipaswa kuchezwa Nyamagana, Mwanza na Geita.

Taarifa hiyo ilionekana kuwavuruga wengi viwanjani, na baadhi ya wadau wa soka walihoji sababu na kanuni zilizosababisha kuahirishwa kwa mapambano hayo.

Mbali na mashabiki, hata mabenchi ya ufundi ya timu zote yalilalamikia kitendo hicho kwani walishafanya maandalizi waliyoshindwa kuyatumia siku hiyo, japo walicheza siku ya pili yake.

MWADUI CHUPUCHUPU

Hakuna ubishi Mwadui walipo wanashukuru Mungu kwa kuponea chupuchupu kushuka daraja baada ya kupata matokeo dakika za nyongeza, huku mashabiki na wadau wa soka wakiwa wameshaamini Geita imepanda Ligi Kuu.

Katika mchezo huo uliopigwa mkoani Shinyanga, Geita Gold ilihitaji sare au ushindi ili ipande Ligi Kuu na kama isingekuwa bao la pili la Salim Aiyee dakika tatu za nyongeza, mashabiki Shinyanga wasingeiona Ligi Kuu msimu ujao, kwani Stand United imeshashuka.

Ilishuhudiwa dakika 90 zikimalizika kwa sare ya bao 1-1 ambapo zile za nyongeza Mwadui ilipata bao la pili, ambalo liliwachanganya kabisa mashabiki wa Geita waliokuwa wameshaanza kusherehekea timu yao kucheza Ligi Kuu.

KIPA GEITA AMWAGA CHOZI UWANJANI

Baada ya mchezo kipa wa Geita Gold, Khomein Abubakary aliangua kilio kufuatia bao la pili dakika za nyongeza.

Awali, Geita walijua wazi kwamba wanaenda Ligi Kuu, lakini ghafla kipa huyo akajikuta anafungwa bao lililowakosesha nafasi hiyo na kuangulia kilio cha haja.

Mbali na kipa huyo, hata mfungaji wa bao hilo, Aiyee naye alijikuta akishindwa kujizuia kumwaga machozi ya furaha na mechi ilipoisha alikaa sehemu moja na kushindwa kunyanyuka.

Licha ya shangwe iliyolipuka uwanjani hapo kwa mashabiki wa Mwadui, lakini Aiyee alikuja kunyanyuliwa na wachezaji wenzake kwa furaha kutokana na kazi nzuri aliyoifanya.

WASIKIENI MAKOCHA, MABOSI

Kocha wa Kagera Sugar, Mecky Maxime alisema licha ya kusubiri mechi ya mwisho, lakini aliamini kwa asilimia zote kuwa lazima timu yake ibaki Ligi Kuu.

“Wapinzani wamepambana ila mimi na vijana wangu hatukuwa na wasiwasi, niliamini timu haishuki daraja, nina wachezaji wazuri sema tu hadi kufika hapa ni matokeo ya mpira,” alisema Maxime.

Kaimu Mwenyekiti wa Pamba, Alem Alibhai alisema wanashukuru kwa hatua waliyofikia kwani wachezaji walipambana vya kutosha, lakini wanaenda kujipanga upya kwa ajili ya msimu ujao.

“Tangu mwanzo tulisema sisi Pamba hatuna cha kupoteza wala presha kama Kagera, kwa ujumla tunawapongeza vijana wetu kwa hatua hii,” alisema Alibhai.

Kocha wa Mwadui, Ally Bizimungu alikiri kuwa licha ya kubaki Ligi Kuu, lakini kazi haikuwa rahisi na kwamba ingekuwa rekodi mbaya kwake kushusha timu kwa mara ya kwanza.

“Lazima tushukuru Mungu kwa matokeo haya, siyo siri haikuwa kazi nyepesi, kikubwa ni kujipanga na msimu ujao kurekebisha kasoro zilizoonekana ili kufanya vizuri,” alisema.

Naye Katibu wa Geita Gold, Seif Kulunge alisema wanakubaliana na matokeo licha ya timu ya kupambana kwa uwezo wao.

“Haikuwa bahati kwa sababu tulikuwa tumeshaamini kucheza Ligi Kuu, lakini dakika 90 zikaamua, kwa hiyo lazima tukubaki matokeo na kujipanga tena kwa msimu ujao wa FDL,” alisema Kulunge.

ADVERTISEMENT