In Summary

Straika huyo wa zamani wa Mathare United, Al-Arabi, Nantes, Auxerre,
Ajaccio na Dubai CSC, sio mtu wa mchezo mchezo. Ulimwengu wa soka wa
Kenya, hutingishika, jina la Dennis Oliech, linapotajwa. Anaheshimika
sana!

Dunia nzima inafahamu kuwa, straika bora kabisa kuwahi kutokea katika soka la Kenya, Dennis Oliech ‘The Menace’, ametua Gor Mahia, kwa mtakaba wa miaka miwili. Hii sio siri tena!
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kogalo, Ambrose Rachier, ni kwamba, ‘Wuod
Mary’, anakuwa mchezaji ghali zaidi nchini na pengine ukanda huu wa
Afrika mashariki, mshahara wake ukiwa ni Ksh350,000, kwa mwezi.
Ni hii, Januari 02, Straika huyo, aliyeibuliwa na timu ya Dagoreti,  aliingia mkataba ambao dau lake linatajwa kuwa ni Ksh3.5 milioni, fedha ambazo atalipwa kwa awamu mbili.
Straika huyo wa zamani wa Mathare United, Al-Arabi, Nantes, Auxerre, Ajaccio na Dubai CSC, sio mtu wa mchezo mchezo. Ulimwengu wa soka wa Kenya, hutingishika, jina la Dennis Oliech, linapotajwa. Anaheshimika sana!


Sahau mabaya yote yaliyosemwa kumhusu Oliech pamoja na changamoto
alizopitia kuanzia kuuguza Mama yake mzazi hadi urahibu wa ‘starehe na
anasa’ akiwa huko Ufaransa, jina la Oliech, linapotajwa huwa nakumbuka
kitu kimoja.
Mwaka 2003, Harambee Stars, chini ya uongozi wa kocha mzalendo Jacob
‘Ghost’ Mulee, ilishuka dimbani pale Nyayo Stadium, kucheza mechi ya
kukata na shoka, dhidi ya Cape Verde.
Jioni hiyo, Stars ile iliyokuwa na mastaa kama nahodha Musa Otieno,
Dennis Oliech, John Baraza, John ‘Mo’ Muiruri, Simeon na Titus Mulama,
iliwatuliza Cape Verde 1-0, mfungaji akiwa ni ‘The Menace’, Dennis
Oliech, wakati huo alikuwa na umri wa miaka 18 tu.

Stars wakaenda Tunisia (AFCON 2004).  Maisha yakaendelea kama kawaida.
Miaka 15, baada ya kuibeba Stars. Miaka miwili baada ya kutundika
daluga. Siku chache baada ya Kenya, kufuzu AFCON 2019, ghafla jina la
Oliech, likaibuka tena!

Kwa mujibu wa ratiba ya KPL, huenda kesho Jumapili, Januari 13,
tukamshuhudia akiwa na jezi ya kijani ya Gor, akiongoza safu ya
ushambuliaji, dhidi ya timu yake ya zamani ya Mathare United, Ugani
Moi Kasarani.

Baada ya hapo, wakazi wa mji wa Kisumu, huenda wakapata bahati ya
kumshuhudia Oliech dimbani, Gor Mahia itakapowavaa Posta Rangers.
Karibu sana ‘The Menace’ soka la Kenya linasubiri kushuhudia maajabu
ya miguu yako.

Tunaposubiri kushuhudia miguu ya ‘The Menace’ ikisakama nyavu za timu
pinzani, sio vibaya tukijadili jambo kuhusu ujio wa Straika huyu,
aliyeamua kurudi dimbani, na tumaini jipya la kuisaidia Kogalo.

Inasikitisha sana watu wanavyojadili umri wa Oliech. Hivi ni nani
katuloga? Nani kasema uwezo wa mtu hutokana na umri wake? Inachekesha
sana. Watu wanasahau kuwa, Criastiano Ronaldo, ana umri wa miaka 33.
Didier Drogba, alistaafu mwaka jana, akiwa na miaka 35.

Wanaoshangaa umri wa Dennis Oliech, wanamsahau kuwa mmoja wa mastraika hatari kwenye EPL, msimu huu, ni Glen Murray (Brighton), mwenye miaka 35. Samuel Eto’o, ana miaka 37 na bado anacheza soka. Pia, wapo
waliotundika daluga, wakarejea dimbani na kufanya makubwa.

Lothar Matthaus (1998), Roger Milla (1990), Michael Laudrup (2003),
Henrik Larsson (2004, 2008), Juan Sebastian Veron (2007), Martin
Palermo (2009), Mario Gomez (2015) na Essam El-Hadary (2017), ni mfano
tu, kwa hiyo Oliech, sio wa kwanza na wala sio wa mwisho.

Oliech, anaweza asiwe yule wa miaka ile, lakini uwepo wake, pale Gor
Mahia, una faida zaidi ya mabao au mchango wake uwanjani. Ukweli
usemwe, kwa jinsi Gor Mahia ilivyo hivi sasa. ni wazi kuwa,
wanamuhitaji mtu makini kama Dennis Oliech. Kwanini?

Unakumbuka Juan Sebastien Veron, alipotua Man United? Fernando Torres
alipotua Chelsea kwa ada ya uhamisho iliyoweka rekodi pale Stamford
Bridge. ni kwamba Veron na Torres wote walikua wachovu kinyama.

Ndani ya Uwanja, Veron na Torres walionekana kuwa hasara kwa vilabu
vyao, lakini kuna kitu walichokuwa nacho. Uwepo wao ulikuwa ni kivutio
kwa mashabiki. Watu walijaza uwanja kuwashuhudia.

Hata Ronaldo, amesajiliwa huko Juventus kwa sababu hiyo. Ukiachalia
mbali kiwango chake kizuri, Juve wamemsajili kuongeza mapato. Ujio wa
Oliech, utawasaidia Gor Mahia, kupiga hela ndefu. Kwanza watazamaji
wataongezeka uwanjani.

Pili, watapata dili nyingi za matangazo, wanachotakiwa kukifanya, ni
kutumia jina la Oliech, ambayo ni brandi, kutengeneza pesa. Lakini pia
kwa kuwa Oliech ana uzoefu, anakuja kuwaamsha mastraika wa Kogalo,
ambao wanaonekana kusinzia.

Tangu wasajiliwe, Ephreim Guikan, Nicholas Kipkirui, Francis Mustapha
na Erisa Ssekisambu, wameshindwa kutengeneza kombinesheni nzuri ya
upachikaji mabao. Hakuna mtu aliyefanikiwa kuziba pengo la Meddie
Kagere.

Kuanzia aondoke Kagere, na kuelekea Simba ya Tanzania, safu ya
ushambuliaji ya Gor, imepoteza makali yake. Tuyisenge amebaki mpweke.
Hana pacha tena. Yale makali ya safu ya ushambuliaji ya Kogalo sasa
inamtegemea ‘Babu’ Dennis Oliech.

Kuna taarifa zinazomhusisha Jacque Tuyisenge na uhamisho wa kwenda
Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini. Kama hilo litatokea, Kogalo watakuwa
wamepata mtu, ambaye kutokana na uzoefu na rekodi nzuri ya kupachika
mabao, atarithi viatu vya Tuyisenge.

Katika siku za hivi karibuni, Gor Mahia haijawa na utulivu. Zaidi ya
mara moja, kumekuwa na taarifa za mgomo baridi. Shinikizo la mishahara
na kelele za mashabiki wakitaka uongozi wa Kogalo ubadilishwe. Yote
haya yanaifanya klabu kukosa mshikamano.

Sio kwamba, anakuja kutatua matatizo ya timu, lakini katika hali kama
hii, ni rahisi sana wachezaji kupoteza mwelekeo na umakini uwanjani,
kama inavyotokea hivi sasa.

Bila kupepesa wachezaji wa Kogalo kwa sasa, ambao wengi wao hawazidi
miaka 30, wanamhitaji mtu aliyekomaa kimawazo, ambaye atatumia uzoefu
wake, kuwatuliza. Mtu huyo ni Dennis Oliech, kwa sababu wengi wao
(wachezaji), wanamheshimu na kumchukulia kama ‘role model’.

Oliech wa sasa, sio yule tuliyemshuhudia miaka 14 iliyopita, akiwa na
miaka 18. Lakini ujio wake, ukitumiwa vizuri na Gor Mahia, unaweza
kusaidia kurudisha mshikamano klabuni hapo, kitu ambacho nachelea
kusema kuwa, kwa sasa haupo.

Aidha, kwa muda sasa, Kogalo ambayo hapo nyuma ilikuwa ni moja ya timu
za kuogopwa, kwenye michuano ya ligi ya mabingwa Afrika na hata lile
la Shirikisho, hawajawa na muenendo mzuri. Baada ya kushindwa
kufurukuta kwenye ligi ya mabingwa, Kogalo wameshushwa hadi Kombe la
Shirikisho.

Huko wamepangiwa kukutana na Star Doula ya Cameroon, katika mechi ta
mtoano, kubaini ni nani ataingia kwenye hatua ya makundi ya msimu wa
2018/19 ya Kombe la Shirikisho barani Afrika. Ugumu wa mchezo
utakuonesha ni namna gani, Gor Mahia, wanamhitaji Straika makini na
mtulivu mbele ya lango, kama Dennis Oliech.

Yote tisa, kumi ni kwamba, kwa mshahara atakaolipwa Dennis Oliech, ni
matumaini yetu kwamba, atazitumia kusahihisha makosa aliyoyafanya hapo
nyuma. Sitegemei kumshuhudia Oliech akijiingiza katika starehe na
anasa kama ilivyokuwa huko nyuma. Kila mtu anafahamu ilikuwaje!

Mshahara wa Ksh300,000 kwa wiki na ada ya usajili ya Ksh3.5 milioni,
zinamtosha Oliech kuanza upya na kutuliza machungu ya kuondokewa na
Mama yake Kipenzi ambaye, alitumia sehemu kubwa fedha zake, kuokoa
maisha yake.

Mpaka kufikia hapo itoshe tu kusema kuwa, wakenya wanasubiri
kushuhudia miujiza ya miguu ya Oliech. Kila mtu anatamani kumuona
Malaika huyu Mzee, akirudisha matumaini yaliyoanza kupotea katika
kambi ya Gor Mahia. Kila la heri, Wuod Mary!

ADVERTISEMENT