In Summary
  • Kiungo huyo aliyetamba pia na Taifa Stars, alitumia nafasi hiyo kuwaomba wanachama wenzake kuwa makini katika kampeni kwa kusikiliza hoja za wagombea ambazo zinatakiwa kulenga mabadiliko ambayo yanaweza kuivusha klabu kutoka katika mfumo wa kuwa tegemezi na kuingia katika mfumo wa uendeshwaji wa kujitegemea.

NYOTA wa zamani na Mwanachama wa Yanga, Sekilojo Chambua amesema anashangazwa na baadhi ya wagombea ambao walishawahi kuiongoza klabu hiyo bila mafanikio kurudi tena katika mchakato wa kuwania uongozi kwenye Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwezi ujao.

Akizungumza na Mwanaspoti, Chambua alisema hataki kuonekana kama anawapigia debe wagombea wapya katika uchaguzi huo, lakini kikubwa anacholenga ni kuona kinachowarudisha baadhi ya viongozi ambao hawakuwahi kuwa na mafanikio katika uongozi wao miaka ya nyuma.

Kiungo huyo aliyetamba pia na Taifa Stars, alitumia nafasi hiyo kuwaomba wanachama wenzake kuwa makini katika kampeni kwa kusikiliza hoja za wagombea ambazo zinatakiwa kulenga mabadiliko ambayo yanaweza kuivusha klabu kutoka katika mfumo wa kuwa tegemezi na kuingia katika mfumo wa uendeshwaji wa kujitegemea.

Yanga ni klabu kubwa inahitaji kupata viongozi wenye upeo mkubwa wa kuifanya iwe mfano wa kuigwa ndani na nje ya nchi, watakaoweza kufanya hivyo ni watu wapya ambao watakuja na mawazo mapya na siyo viongozi waliopita miaka ya nyuma na kushindwa kuifanya timu ikawa na mifumo bora.”

“Tulikuwa na mfumo wa kumtegemea tajiri mmoja, ameondoka unaona kabisa timu ilivyoyumba na kukosa ubora wa kiushindani. Sidhani kama kuna wanachama wanapendezewa na hili, hivyo naomba iwe changamoto kwetu kuhakikisha tunachagua kiongozi bora na mwenye nia nzuri ya kuivusha klabu kutoka hapa ilipo na kuipelkeka sehemu nyingine,” alisema na kuongeza;

“Inashangaza kuona viongozi wameitumikia timu kwa muda mrefu bila mafanikio wanarudi tena na ndiyo maana nawasisitiza kuwa makini katika hili kwa kusikiliza zaidi hoja za watu wapya, kwani waliokuwepo mwanzoni walishindwa wapi kama wanataka kurudi tena kwa mara nyingine,” alisema.

Alisema Yanga ina mtaji mkubwa wa wanachama ambao hata wao wenyewe wakiamua kuiendesha klabu yao wanaweza, kinachokosekana ni watu sahihi wa kuisimamia na kutumia vizuri jina kubwa walilonalo ili iweze kujiendesha yenyewe.

Uchaguzi wa Yanga umepangwa kufanyika Mei 5 baada ya kuwepo na sintofahamu ya muda mrefu, jambo ambalo Chambua alisema anatamani awamu hii usiahirishwe tena kama awali.

ADVERTISEMENT