In Summary
  • Washambuliaji Cavan, Suarez wamekuwa na rekodi nzuri katika timu yao ya taifa kila mara wanaposhiriki katika mashindano mbalimbali

Sao Paolo, Brazil. Washambuliaji Edinson Cavani na Luis Suarez wameiongoza Uruguay kupata ushindi wa kishindo cha mabao 4-0 dhidi ya wachezaji 10 wa Ecuador katika mchezo wa Copa Amerika.

Uruguay pia ilipata bao lililofungwa na Nicolas Lodeiro na lile la kujifunga kwa beki wa Ecuador, Arturo Mina katika mchezo wa Kundi C uliofanyika kwenye Uwanja wa Mineirao.

Uruguay ilianza kucheza na faida ya mchezaji moja zaidi katika dakika 24, baada ya nyota wa Ecuador, Jose Quintero kuonyeshwa kadi nyekundu kwa kumpiga kiwiko Lodeiro. Quintero alipewa kadi ya njano, lakini picha ya video ilionyesha kuwa alithahiri kadi nyekundu.

Uruguay ilikuwa inatawala mchezo huo wakati Quintero anatolewa nje kwenye Uwanja wa Mineirao, katika mchezo huo ulioshuhudiwa na mashabiki wachache 13,000.

Lodeiro alifunga bao la kwanza katika dakika sita akimalizia pasi ya Suarez akiwa ndani ya eneo la 18, kabla ya Cavani kuongeza bao la pili kwa shuti akimalizia mpira uliotemwa na kipa wa Ecuador, Alexander Dominguez katika dakika 33.

Suarez aliongezea bao la tatu kwa mpira wa kona dakika 44, kabla ya Mina kujifunga mwenyewe katika dakika 78 akijaribu kuokoa mpira wa krosi.

ADVERTISEMENT