In Summary

Beki huyo ghali duniani kuna wakati alikimbia spidi ya kilomita 34.5 kwa saa, ikiwa ni kasi kubwa kuwahi kufanywa na mchezaji yeyote kwenye ligi hiyo

Liverpool, England. Beki wa kati wa Liverpool, Virgil van Dijk ndiye mchezaji mwenye kasi zaidi katika Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita kuliko yeyote, akiwafunika mastaa wote unaowafahamu wewe kwa kasi kama vile Leroy Sane, Kyle Walker na Kylian Mbappe.

Beki huyo Mdachi hafahamiki sana kama ana kasi kihivyo ndani ya uwanja, hasa huko kwenye kikosi cha Liverpool, ambapo mastaa wanaotambulika kwa kukimbia kasi zaidi uwanjani ni Mohamed Salah na Sadio Mane.

Lakini, beki huyo ghali duniani kuna wakati alikimbia spidi ya kilomita 34.5 kwa saa, ikiwa ni kasi kubwa kuwahi kufanywa na mchezaji yeyote kwenye ligi hiyo ya Ulaya kwa msimu uliopita.

Van Dijk alikimbia kwa kasi hiyo katika mechi ya kwanza ya nusu fainali dhidi ya Barcelona huko uwanjani Nou Camp, ambapo Liverpool walikumbana na kichapo cha Bao Tatu Bila.

Barcelona walianzisha shambulizi la kushtukiza katika dakika ya 92 lililomlazimu Van Dijk kutoka spidi kwenda kuokoa hatari hiyo. Hakuna mchezaji mwingine aliyekimbia kwa kasi kama hiyo kwenye Ligi ya Mabinga Ulaya kwa msimu wote uliopita.

Mastaa wengine waliokimbia kwa kasi zaidi kwenye michuano hiyo kwa msimu uliopita ni Sane, Walker, Nemanja Radonjic na Gareth Bale, ambaye alikimbia kilomita 33.8 kwa saa.

ADVERTISEMENT