In Summary

Suarez amekuwa kwenye kiwango bora kabisa tangu alipotua Barcelona, ambako amebeba mataji kibao, huku akifunga mabao 164 katika mechi 220 alizocheza kwenye kikosi hicho cha La Liga.

WANASEMA hivi, lisemwalo lipo na kama halipo basi litakuja tu.

Huko Barcelona kwa sasa kumekuwa na taarifa kwamba wamechungulia kote na kuona kwamba straika wa Tottenham Hotspur, Harry Kane ndiye mtu mwafaka wa kwenda kurithi mikoba ya Luis Suarez kwenye kikosi chao.

Wababe hao wa Hispania wanafahamu wazi kwamba fowadi wao huyo, Suarez umri umeshaanza kumtupa mkono na hivyo wameanza mchakato wa kumtafuta mbadala wake mapema, huku mchezaji huyo mwenyewe akiwaambia mabosi wake hao kwamba wafanye hivyo haraka.

Suarez amekuwa kwenye kiwango bora kabisa tangu alipotua Barcelona, ambako amebeba mataji kibao, huku akifunga mabao 164 katika mechi 220 alizocheza kwenye kikosi hicho cha La Liga.

Lakini, si muda mrefu atatimiza miaka 32 na hivyo Barcelona wanadhani umefika wakati wa kuanza kumtafuta mshambuliaji mwingine mwenye uwezo wa kuja kuendeleza na pengine kufanya vyema zaidi kuanzia pale alipokomea supastaa huyo wa kimataifa wa Uruguay.

Katika kuchuja majina ya washambuliaji inawataka, Barcelona imeona Kane atawafaa zaidi, licha ya kwamba mshambuliaji huyo wa England amekuwa na mkataba mrefu kwenye kikosi cha Spurs utakaokomea 2024.

Kane mwenye umri wa miaka 25, amechangia mabao 160 katika mechi 242 alizocheza Spurs na hakika timu hiyo ya London bila ya shaka itataka ada inayoanzia Pauni 100 milioni katika kumuuza supastaa wao huyo.

ADVERTISEMENT