In Summary

Ombi hilo limetolewa na Kocha Mkuu wa Bandari FC, Bernard Mwalala ambaye alilaumu vitendo vilivyotekelezwa na Sony Sugar wakati wa mechi yao ya Ligi Kuu iliyochezwa uwanja wa Awendo ambapo walishindwa kwa mabao 2-0.

 MOMBASA. SHIRIKISHO la Soka la Kenya (FKF) na Kenya Premier League (KPL) zimeombwa zichunguze tabia za baadhi ya timu kutumia vitisho na vitendo visivyofaa kwa kulazimisha matokeo ya ushindi kwenye mechi zao za nyumbani.

Ombi hilo limetolewa na Kocha Mkuu wa Bandari FC, Bernard Mwalala ambaye alilaumu vitendo vilivyotekelezwa na Sony Sugar wakati wa mechi yao ya Ligi Kuu iliyochezwa uwanja wa Awendo ambapo walishindwa kwa mabao 2-0.

“Tumekubali kushindwa kama wanamichezo lakini yale yaliyotendeka wakati wa mchezo wetu huo yanastahili kuchunguzwa na kukomeshwa kwani si sawa kufanyika kwenye ligi kuu. Ni uzuri KPL na FKF itambuwe yale yanayofanyiwa timu zinazocheza hapo Awendo,” akasema Mwalala.

Alidai kuwa hata wakati alipoumia vibaya beki wao Bernard Odhiambo, wahusika hawakushughulika naye mpaka Kocha wa magolikipa Razak Siwa kwenda kumtoa kiwanjani.

“Ni muhimu kwa timu zinazocheza nyumbani kuwa nanidhamu na kuhakikisha zinashinda mechi zao kwa njia za halali na wala si kuwaogopesha na kuwalazimisha marefarii kutoa maamuzi ya kusaidia wapate ushindi wa lazima,” akalalama Mwalala.

Kutokana na kushindwa huko na Sony Sugar, Bandari iliyocheza mechi 17, imebakia nafasi ya tatu ikiwa na pointi 32 sawa na walizonazo Gor Mahia ambayo imecheza mechi 15 pekee, Gor inapigiwa upatu wa kuhifadhi taji lao.

Kwa wakati huu, Sofapaka ndiyo iko kileleni mwa Ligi Kuu ya SportPesa ikiwa na pointi 33 lakini imecheza mechi 18, tatu zaidi ya Gor na moja zaidi ya Bandari ambayo ikifanikiwa kushinda mchezo wao ujao, itarudi kileleni mwa ligi hiyo.

ADVERTISEMENT