In Summary

Simba itacheza nusu fainali za michuano hiyo leo Ijumaa usiku dhidi ya Malindi ambapo kwenye wachezaji wanane waliobaki ni Mo Ibrahim pekee anayecheza nafasi ya kiungo.

KOCHA Mkuu wa Simba, Patrick Aussems aliwataka viongozi wake kumuongezea viungo wanne kutoka timu ya vijana ambao watasaidiana na Mohamed Ibrahim katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi.

Simba itacheza nusu fainali za michuano hiyo leo Ijumaa usiku dhidi ya Malindi ambapo kwenye wachezaji wanane waliobaki ni Mo Ibrahim pekee anayecheza nafasi ya kiungo.

Kikosi kilichotua juzi Jumatano cha wachezaji wanane ambacho kimeungana na kikosi kilichobaki Zanzibar viungo wapo wanne ambao ni Yahya Mbegu, Salum Shaban, Dickson Mhilu na Oscar Modest.

Wachezaji wengine ni straika mmoja atakayesaidiana na Adam Salamba na Abdul Seleman wakati mabeki ni Mfaume Omary na Juma Gombelo watakaopigania namba dhidi ya Asente Kwasi, Paul Bukaba, Yusuph Mlipili na Zana Coulibaly wakati kipa aliyeongezwa ni Ally Athuman aliyeungana na Ally Salim.

Kocha wa timu hiyo, Nico Kiondo, alisema anaamini kikosi chake kipo vizuri na tayari kwa nusu fainali hiyo ambapo amedai amewasoma wachezaji wa timu pinzani baada ya kuwaangalia katika mechi yao ya juzi ambayo ilikuwa ni kumalizia hatua ya makundi dhidi ya Azam FC.

Hata hivyo, Kiondo alisema wachezaji waliobaki walikuwa chini ya Aussems ndiyo watakaopewa nafasi kubwa ya kucheza mechi hiyo ingawaje atawachanganya na baadhi wapya.

“Kila kitu kipo vizuri na sina majeruhi yoyote, tunawajengea kujiamini wawapo uwanjani na ndiyo maana wote wanajiamini kucheza mechi hiyo ingawa watakaotumika weni wao ni wale waliobaki hapa.

“Wachezaji tuliokuja nao ni kwa mujibu ya matakwa ya Kocha Aussems ikiwemo kufuata programu yake aliyoiacha, tunaamini kila kitu kitakwenda vizuri pasipo kuharibu mipango ya ushindi,” alisema Kiondo ambaye alikuwa mchezaji wa Simba miaka ya nyuma.

Simba iliingia hatua hiyo baada ya kushinda mechi zake zote tatu za makundi na kukusanya pointi tisa kutoka Kundi A.

ADVERTISEMENT