In Summary

Agosti 22, 2013, Barcelona iliamua kumnasa Suarez katika ada ambayo haikuwekwa hadharani huku akisaini mkataba wa miaka minne. Msimu wa 2013–14 alicheza mechi nyingi katika kikosi cha Barcelona B Ligi Daraja la Kwanza.

LONDON, ENGLAND

KOCHA wa Arsenal, Unai Emery hatimaye amefanikiwa kuinasa saini ya mkopo ya kiungo mchezeshaji wa Barcelona, Denis Suarez ambaye anaweza kumnunua jumla mwishoni mwa msimu huu kwa dau la Pauni 20 milioni kama akiridhishwa na kiwango chake.

Ni nani huyu Denis Suarez?

Azaliwa Hispania, aibukia Man City. Jina lake kamili ni Denis Suárez Fernández na alizaliwa katika kitongoji cha Salceda de Caselas nchini Hispania mnamo Januari 6, 1994. Alianza kucheza soka katika klabu za vijana za Porrino na kisha Celta Vigo.

Kutokana na kiwango kizuri ambacho alionyesha, Suarez alianza kuandamwa na klabu mbalimbali kubwa za Ulaya lakini walikuwa Manchester City ambao waliinasa saini yake mnamo Mei 23, 2011. Kwa kuinasa saini yake, City ilikuwa imezipiga bao klabu za Barcelona, Chelsea na Manchester United ambazo zilionyesha nia ya kumchukua.

City walilipa dau la Pauni 850,000 huku kukiwa na uwezekano wa pesa hizo kuongezeka mpaka Pauni 2.75 milioni kutokana na kiwango chake na idadi ya mechi ambazo atakuwa amecheza. Alicheza mechi ya kwanza katika pambano la maandalizi ya msimu mpya wa 2011–12 dhidi ya Los Angeles Galaxy akiingia dakika ya 88 kuchukua nafasi ya Edin Dzeko.

Akakaa benchi katika pambano la kombe la Ligi dhidi ya Birmingham City na kisha kucheza mechi yake ya kwanza ya ushindi katika ushindi wa mabao 5-2 dhidi ya Wolves Kombe la Ligi akiingia uwanjani katika dakika ya 67 kuchukua nafasi ya Samir Nasri.

Mei 17, 2012 Suarez alianza katika pambano la wachezaji wa akiba kati ya Manchester City na Manchester United ambapo aling’ara katika mechi hiyo licha ya City kuchapwa mabao 2-0. Mwishoni mwa msimu huo alipigiwa kura ya kuwa mchezaji bora kijana wa mwaka na mashabiki wa City.

Barcelona yamrudisha Hispania

Agosti 22, 2013, Barcelona iliamua kumnasa Suarez katika ada ambayo haikuwekwa hadharani huku akisaini mkataba wa miaka minne. Msimu wa 2013–14 alicheza mechi nyingi katika kikosi cha Barcelona B Ligi Daraja la Kwanza.

Julai 2014 alipelekwa kwa mkopo wa misimu miwil katika kikosi cha Sevilla katika dili ambalo lilikuwa sehemu ya uhamisho wa kiungo wa kimataifa wa Croatia, Ivan Rakitic kwenda Barcelona huku pia Sevilla wakipata pesa.

Alicheza mechi yake ya kwanza ya ushindani Agosti 12, 2014 katika pambano la SuperCup dhdi ya Real Madrid Uwanja wa Cardiff dhidi ya Real Madrid huku ikichapwa mabao 2-0 . katika pambano hilo alitoka katika dakika ya 78 na nafasi yake kuchukuliwa na José Antonio Reyes.

Desemba 11 alifunga bao pekee la Sevilla katika pambano la mwisho la makundi michuano ya Europa dhidi ya HNK Rijeka huku akiipeleka timu hiyo katika hatua inayofuata.

Katika msimu wake huo ambao alicheza Sevilla, Suarez alianza mechi 25 huku kwa ujumla akicheza mechi 46 katika michuano mbalimbali. Alitwaa ubingwa wa Europa chini ya kocha wa sasa wa Arsenal, Unai Emery huku Sevilla ikimaliza nafasi ya tano La Liga. Alifunga mabao sita na kupika mabao matano.

Atinga Villarreal arudi tena Barcelona

Agosti 29, 2015 Suarez alitinga katika Klabu ya Villarreal baada ya klabu hiyo kukoshwa na kiwango ambacho alikionyesha akiwa na Sevilla. Alisaini mkataba wa miaka minne lakini Barcelona wakiweka kipengele ambacho kingewaruhusu kumnunua kwa bei kiduchu.

Msimu huo Suarez aliwasha moto vilivyo huku akiipeleka Villarreal katika michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Ulaya ambapo alifunga mabao matano na kupika mabao 11. Kutokana na kiwango chake Barcelona walianza kumtamani tena.

Julai 4, 2016 Barcelona ilitangaza kurudi kwa Suarez katika kikosi chao baada ya kutumia kipengele cha kumrudisha kwa bei kiduchu ambapo walilipa kiasi cha Euro 3.5 milioni kumnunua huku akisaini mkataba wa miaka minne. Katika msimu wake wa kwanza alifanikiwa kuanza mechi 12 tu za La Liga.

Atinga kikosi cha Hispania

Suarez alianza soka la kimataifa kwa kukipiga katika kikosi cha Hispania chini ya umri wa miaka 17 wakati alipofunga mabao mawili katika mechi dhidi ya Moldova na Ireland ya Kaskazini. Vile vile alikuwa katika kikosi cha Hispania chini ya umri wa miaka 19 kilichotwaa michuano ya Euro chini ya umri huo mwaka 2012.

Katika pambano la fainali dhidi ya Ugiriki alitolewa nje katika dakika ya 71 huku akicheza mechi sita za michuano hiyo ambayo alifunga mabao mawili huku akicheza kwa dakika 284.

Mei 29, 2016 alicheza mechi yake ya kwanza kwa timu ya wakubwa ya Hispania alipoingia uwanjani kuchukua nafasi ya David Silva katika pambano dhidi ya Bosnia & Herzegovina.

ADVERTISEMENT