In Summary

Torreira amelalamikia ligi pia, kwamba mechi zimekuwa nyingi sana kiasi cha kumfanya awe kwenye wakati mgumu kukabiliana nazo. “Imenilazimu kuzoea kucheza mechi kila baada ya siku tatu, kitu ambacho ni kigumu.

LONDON, ENGLAND.HUYU Lucas Torreira anataka kuondoka. Msimu mmoja tu kwenye kikosi cha Arsenal, lakini anadai Italia maisha matamu kuliko England.

Kiungo huyo wa kati alitua Arsenal akitokea Sampdoria ya Italia kwa ada ya Pauni 26 milioni, mwaka jana, lakini baada ya sasa kuwindwa na AC Milan tayari ameibuka na madai ameyamisi maisha ya Italia.

Torreira amekuwa na mchango mkubwa kwenye kikosi hicho cha Kocha Unai Emery, hivyo kama maneno yake hayo akiwa na maana anataka kuachana na maisha ya Emirates, basi litakuwa pigo kubwa sana kwenye kikosi hicho.

Milan imekuwa ikihusishwa na mpango wa kumrudisha kiungo huyo kwenye soka la Serie A baada ya kocha wake wa zamani huko Sampdoria, Marco Giampolo kuchukua mikoba ya kuinoa timu hiyo ya San Siro.

Torreira amezua hofu akisema: “Sijui kama kuna mambo mengi niliyofurahia. Nadhani ilikuwa bora zaidi Italia. England ni dunia tofauti kabisa, nchi kubwaaa. Lugha pia imekuwa tatizo kuweza kuwasiliana vyema na wachezaji wenzangu. Ni jambo gumu kukaa bila ya kuzungumza na wenzako.

“Kuna hili la hali ya hewa. Huwezi kutoka nje asubuhi, kuna ukungu, ukichelewa kurudi nyumbani, kuna ukungu. Ni mambo ya ajabu sana. Labda pengine miaka inakwenda, pengine nitazoea.”

Torreira amelalamikia ligi pia, kwamba mechi zimekuwa nyingi sana kiasi cha kumfanya awe kwenye wakati mgumu kukabiliana nazo. “Imenilazimu kuzoea kucheza mechi kila baada ya siku tatu, kitu ambacho ni kigumu.

Kuna mechi nyingi. Kwa upande wangu nashukuru na nimefurahi kwa nilichokifanya.”

ADVERTISEMENT