In Summary
  • Akizungumzia maandalizi yao, Ambokile alisema yako vizuri na anachoshukuru Mungu ni ushirikiano ambao anaopewa na wachezaji wenzake tangu alipojiunga na timu hiyo.

STRAIKA wa Mbeya City, Eliud Ambokile ambaye amejiunga na Black Leopard ya Afrika Kusini kwa mkopo, huenda Jumatano akaichezea klabu yake hiyo mpya mchezo wake wa kwanza kwenye Kombe la Nedbank dhidi ya Bidvest Wits.

Chama hilo la Ambokile litakuwa nyumbani katika uwanja wao wa nyumbani wa Peter Mokaba, ulipo mji wa Polokwane kuwakaribisha Bidvest Wits kwenye hatua ya 16 bora.

Akizungumzia maandalizi yao, Ambokile alisema yako vizuri na anachoshukuru Mungu ni ushirikiano ambao anaopewa na wachezaji wenzake tangu alipojiunga na timu hiyo.

“Furaha yangu ni kucheza kikosi cha kwanza, nimekuwa nikijituma mazoezini ili nianze kupata nafasi ya kucheza kwenye michezo ya hivi karibuni, natambua sio rahisi kwenda sehemu na kufika moja kwa moja kuanza kucheza.

“Mchezo uliopita tulipoteza mbele ya Mamelodi Sundowns kwa mabao 3-0, sikupata nafasi ya kucheza kwa sababu ya ugeni wangu, nadhani mwalimu anaweza kunipa nafasi Jumatano,” alisema Ambokile.

Mshambuliaji huyo mwenye miaka 25, aliongeza mpango wake ni kuhakikisha anatumia vizuri nafasi ya kucheza kwa mkopo ili mwisho wa msimu asalie kwenye klabu hiyo, iliyoanzishwa mwaka1983.

ADVERTISEMENT