In Summary
  • Kabla ya kikao cha Ijumaa iliyopita kati ya Serikali kupitia wizara ya Michezo, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na baadhi ya viongozi wa Yanga, klabu hiyo ilikuwa katika sintofahamu kuhusu hatma ya aliyekuwa Mwenyekiti, Yusuf Manji.

WAKATI mchakato wa uchaguzi wa Yanga ukiendelea, Katibu wa Baraza la Wazee wa klabu hiyo, Ibrahim Akilimali amesema Yanga ilikuwa kwenye kizungumkuti ambacho haikustahili kufikia hapa ilipo.

Kabla ya kikao cha Ijumaa iliyopita kati ya Serikali kupitia wizara ya Michezo, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na baadhi ya viongozi wa Yanga, klabu hiyo ilikuwa katika sintofahamu kuhusu hatma ya aliyekuwa Mwenyekiti, Yusuf Manji.

“Sisi Yanga hatuna shida na yule ‘bwana mdogo’ akimaanisha Manji, aliondoka bila kugombana na mtu, hakufukuzwa na wala hakutukanwa, kama akisema anahitaji kurejea sisi tuko tayari, ila twende kwanza kwenye uchaguzi,” alisema Akilimali.

Alisema Serikali imetoa maelekezo kama Manji anahitaji kurejea Yanga basi arudi kama mdhamini, mlezi au mwekezaji, hiyo ni sawa kabisa kwani hakuna anayemchukia na akitamka anarudi wala hayupo atakayempinga, cha msingi ni twende kwanza kwenye uchaguzi,” alisema.

Alisema hali hiyo ilifanywa na baadhi ya watu kutaka Yanga ifike hapo.

“Unajua kuna watu walitaka kutulisha ugali na supu ya samaki, lakini sasa tunakwenda tunaelewana,”alisema Akilimali huku akihoji kama Mwenyekiti alikuwepo, mbona tena nafasi yake imekaimiwa.

“Tujiulize tu mbona juzi wamechaguana na amepatikana Kaimu Mwenyekiti wa Yanga, wakati Mwenyekiti yupo?,” alihoji.

Alisema Yanga hawakuwa na sababu ya kufika hapo lakini sasa anaamini mambo yatakwenda vizuri na kizungumkuti kilichotokea ni upepo tu ambao ulipita.

“Narudia tena, Manji hakugombana na mtu Yanga, hakufukuzwa wala hakutukanwa, akisema anahitaji kurudi hakuna atakayempinga, lakini atamke mwenyewe hata baada ya uchaguzi, atarudi kwa njia nyingine kama ambavyo Serikali imeshauri,”.

Ijumaa iliyopita katika kikao cha Yanga, Serikali na TFF, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo nchini, Yusuph Singo alisema njia iliyopo ya Yanga kumrejesha Manji ni kumfanya awe mlezi, mdhamini au apitie njia alizotumia mfanyabiashara Mohamed Dewji (Mo Dewji) Simba.

ADVERTISEMENT