In Summary

Awali Yanga ilikuwa imemweka kwenye orodha ya nyota wa kigeni wa kutemwa kikosini, lakini Kamusoko ameonyesha moto katika mechi za mwisho za Ligi Kuu Bara kiasi cha kuitwa timu yake ya taifa, The Mighty Warriors walipo Misri kwa fainali za Afcon.

Dar es Salaam. Kiwango cha hali juu kilichoonyeshwa na kiungo wa Zimbabwe, Thabani Kamusoko kwenye mechi zao za kirafiki za kujiandaa na Fainali za Afcon 2019 zimewafanya mabosi wa Yanga kugawanyika kama wamuache ama wambakishe kikosini.
Awali Yanga ilikuwa imemweka kwenye orodha ya nyota wa kigeni wa kutemwa kikosini, lakini Kamusoko ameonyesha moto katika mechi za mwisho za Ligi Kuu Bara kiasi cha kuitwa timu yake ya taifa, The Mighty Warriors walipo Misri kwa fainali za Afcon.
Kiungo huyo aliyejiunga na Yanga mwaka 2015 akitokea FC Platinum ya kwao Zimbabwe alikuwa atemwe kwa madai ya kuwa na umri mkubwa kwani jina lake lilipendekezwa na Kocha Mwinyi Zahera apewe mkono wa kwaheri.
Hata hivyo, soka alililolionyesha Kamusoko dhidi ya Taifa Stars na mchezo kumalizika kwa sare ya 1-1 sambamba na mechi nyingine za kujipima nguvu za timu yake ya taifa imewagawa mabosi wake.
Chanzo cha ndani kutoka klabu hiyo kililiambia Mwanaspoti kuwa viongozi wamekaa na kuanza kumjadili baada ya kusikia na kuona ni miongoni mwa nyota wa timu ya taifa ya Zimbabwe ambao wanapata nafasi ya kucheza na ameonekana kufanya vizuri.
“Suala la Kamusoko limerudi tena mezani, lakini bado halijakaa vizuri kwasababu kuna baadhi ya viongozi hawataki aongezwe mkataba na wengine wanasema apewe nafasi kutokana na kuonyesha uwezo mara baada ya kutoka majeruhi,” kilisema chanzo hicho.
“Kamusoko alikuwa ni miongoni mwa nyota ambao waliondolewa katika mpango wa mwalimu lakini kile anachokifanya katika maandalizi ya Afcon kimewachanganya baadhi ya viongozi na kuona kama anaweza akawa na msaada katika kikosi chao msimu ujao kutokana na uzoefu wake wa mashindano makubwa,” kilisema chanzo hicho.
Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela alisema hawajawahi kutangaza kumuacha mchezaji hata mmoja tangu msimu umeisha wamekuwa wakishuhudia tu kutoka katika vyombo vya habari kwamba wamewaacha wachezaji wao.
“Hatujaacha mchezaji, Yanga nyota wengi wamemaliza mikataba na suala la kuongeza au kutokuwaongeza ni jukumu la mchezaji na mwajiri wake kukaa meza moja na kufikia makubaliano, hivyo kwenye hilo tusubiri kuona baada ya dirisha la usajili kufungwa kila mmoja atatambua ni nyota gani wanaendelea na wapi wanaachwa,” alisema Mwakalebela.
“Tuna tamasha la Siku ya Mwananchi ambalo tunatarajia kulifanya Agosti mwaka huu ni maalum kwaajili ya kutambulisha nyota wapya waliosajiliwa ikiwa ni sambamba na wachezaji ambao wataitumikia timu yetu kwa msimu mpya hivyo ni muda tu ambao utaamua nani ni nani Yanga,” alisema Mwakalebela.

ADVERTISEMENT