In Summary

Staa huyo amekuwa akihusishwa na mpango wa kuhamia Real Madrid, lakini dili hilo limekuwa kwenye mashaka makubwa kwa sababu ya matakwa ya Man United kuhitaji ilipwe Pauni 150 milioni kwenye mauzo ya kiungo huyo.

MANCHESTER, ENGLAND. Kiungo wa Manchester United, Paul Pogba yupo kwenye maandalizi ya kuachana na wababe hao wa Old Trafford kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi huko Ulaya.
Kiungo huyo Mfaransa ametangaza hadharani dhamira yake ya kuachana na Man United kwenye dirisha hili, akisema anahitaji changamoto mpya.
Staa huyo amekuwa akihusishwa na mpango wa kuhamia Real Madrid, lakini dili hilo limekuwa kwenye mashaka makubwa kwa sababu ya matakwa ya Man United kuhitaji ilipwe Pauni 150 milioni kwenye mauzo ya kiungo huyo.
Pogba dhamira yake ni kuondoka Man United na atafanya kila awezalo hata kwa kugoma kuhakikisha anaondoka kama akiona timu hiyo inambania kwenda kutimiza ndoto zake.
 Hata hivyo, Man United haihitaji kuwa na mawazo sana kutokana na ukweli kwamba kuna viungo watano hao, wanatosha kabisa kuja kuchukua buti zake huko Old Trafford na wakafanya maajabu.

Bruno Fernandes
Jina la Fernandes kwa muda sasa limekuwa likihusishwa na mpango wa kujiunga na Man United. Staa huyo wa Kireno amekuwa akihusishwa na mpango wa kutua Old Trafford kwa muda sasa tangu dirisha la uhamisho wa majira ya lilipofunguliwa. Fernandes ni kiungo wa kati anayefanya vizuri sana kwenye kushambulia. Ameshaweka wazi kwamba yupo tayari kuzungumza na Sporting Lisbon ili kumfungulia mlango wa kutokea kama kutakuwa na timu ambayo ipo siriazi kuhitaji huduma yake. Atletico Madrid imekuwa ikihitaji saini yake pia, lakini kwa Man United kwa sababu inaelekea kumpoteza Pogba, basi itakuwa jambo zuri kumkimbilia kiungo huyo wa Kireno ili atue kwenye kikosi hicho. Ada yake inaweza kuwa Pauni 44.6 milioni.

Adrien Rabiot
Hili ni chaguo jepesi zaidi. Kitu kizuri kuhusu Rabiot ni kwamba anapatikana bure kabisa kutokana na kumaliza mkataba wake huko Paris Saint-Germain. Kiungo Rabiot bado kijana na huduma yake ya uwanjani si ya mchezo licha ya kwamba amekuwa akibaniwa kupewa nafasi huko kwenye kikosi cha PSG.
Huduma yake imekuwa ikisakwa na timu nyingi, lakini Kocha Ole Gunnar Solskjaer anaweza kuchangamka na kukamatia huduma yake ili kumweka kwenye kikosi chake kuondoa shida endapo kama Pogba ataondoka.

Youri Tielemans
Staa huyo wa Kibelgiji, Youri Tielemans ameonyesha ubora mkubwa sana kwenye Ligi Kuu England alipocheza kwa mkopo huko Leicester City msimu uliopita. Tangu hapo, staa huyo wa Monaco amekuwa akihusishwa na mpango wa kunaswa na Man United na timu nyingine kubwa za Ulaya.

Christian
Eriksen
Staa wa Tottenham Hotspur, Christian Eriksen ametangaza wazi anataka kuachana na kuihama klabu hiyo ya London, huku kuna wakati jina lake lilitajwa huko Real Madrid. Lakini habari za huko Bernabeu kwa sasa ni Pogba, jambo linalomfanya Eriksen kumwaambia wakala  wamuulize Florentino Perez kama dili la kuhamia Madrid liko hai au limeshafutwa. Man United iliripotiwa kuhitaji huduma ya mchezaji huyo na sasa inaweza kukoleza mwendo zaidi ili aje kuchukua mikoba ya Pogba kama ataamua zake kuondoka katika dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi huko Ulaya. Eriksen anaweza kuwa chaguo sahihi.

Philippe Coutinho
Kiungo wa Barcelona, Philippe Coutinho kwa muda mrefu amekuwa akihusishwa na mpango wa kusajiliwa na Manchester United.
Staa huyo wa Kibrazili, aliyetamba sana Liverpool ameshindwa kuonyesha makali yake tangu alipotua huko Nou Camp na imeripotiwa kwamba ameshafunguliwa milango ya kuhama timu hiyo.

ADVERTISEMENT