In Summary

Tarehe  Juni 16, miaka 12 iliyopita, Tanzania ilitambulisha kipaji kilichofuata cha Erasto Edward Nyoni. Ilikuwa kwenye mchezo wa ugenini mjini Ouagadougou, Burkina Faso, kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika 2008 zilizofanyika huko Ghana.

WIKI iliyopita niliahidi kuwaletea uchambuzi wa kina kuhusu Ibrahim Ajibu pamoja na wapinzani wake wa namba kwenye kikosi cha timu ya taifa ‘Taifa Stars’.
Hii inafuatia kuwaletea uchambuzi wa Jonas Mkude katika mfumo na muundo huo huo.
Lakini bahati mbaya sitawaletea uchambuzi huo kwa sababu nimeridhika pasi na shaka kwamba wachezaji hawa hawakuachwa na Kocha Emmanuel Amunike kutokana na uwezo wao wa kimpira, bali ni nidhamu zao.
Mkude, kama nilivyogusia wiki iliyopita, ni kweli kwamba aliondoka kambini baada ya kuhudhuria siku moja tu na hakurudi tena hadi siku ya safari.
Ajibu hali kadhalika, alikuwa anakwenda mazoezini akiwa na mabarafu kwamba ni majeruhi.
Lakini, hata hivyo, Ajibu alionyesha kutofurahia kuitwa tangu katika kile kikosi cha wachezaji 39 akisema hajawahi kuona timu ina watu wengi kiasi hicho. Awali kulikuwa na madai ya mpango wa kukataa kabisa kuripoti kambini.
Kutokana na hilo, nimejidhihirisha kwa kina kwamba hapo hayupo aliyeonewa na Kocha Amunike.
Hata ningekuwa mimi nd’o kocha, nisingefanya tofauti na hivyo. Hivyo, nimeamua kuachana na mjadala wao na kuwekeza nguvu katika mambo mengine. Badala ya kuwajadili wachezaji ambao hawapo kwenye timu, naomba niwaletee mtu huyu wa shoka, Erasto Nyoni na utumishi wake uliotukuka ndani ya Stars.
Upupu huwasha, lakini muwashwaji sio lazima ajisikie mateso...anaweza akajisikia raha tu, kutokana na usugu wa ngozi yake. Wakati mwingine kuwashwa ni raha. Muulize Nandy (utani kidogo).
Tarehe kama ya juzi, Juni 16, miaka 12 iliyopita, Tanzania ilitambulisha kipaji kilichofuata cha Erasto Edward Nyoni. Ilikuwa kwenye mchezo wa ugenini mjini Ouagadougou, Burkina Faso, kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika 2008 zilizofanyika huko Ghana.
Siku hiyo, Kocha Marcio Maximo alimpa nafasi kijana huyo wa miaka 19 kuichezea Taifa Stars kwa mara ya kwanza.
Naye hakumwangusha kocha wake, akaipamba siku hiyo muhimu kwake kwa kufunga bao pekee na la ushindi kwa Stars.
Ushindi ule ulikuwa wa kwanza kwa Tanzania katika mechi za ugenini kuwania kufuzu kwa Fainali za Mataifa ya Afrika, tangu Februari 16, 1969.
Mwaka huo, katika harakati za kuwania kufuzu Afcon 1970, Tanzania iliifunga Kenya 1-0 jijini Nairobi.
Nyoni ambaye wakati huo alikuwa akiichezea Vital’O ya Burundi, alifunga bao hilo dakika ya 77, lakini mtangazaji wa Kituo cha Runinga cha Taifa, TVT (sasa TBC) kilichoonyesha mchezo huo, Juma Nkamia akasema mfungaji alikuwa Boban (Haruna Moshi) na kuwachanganya Watanzania.
Na hii ilikuwa kutokana na ugeni wa kijana huyo miongoni mwa Watanzania wenzake. Hakuwa akifahamika kabisa, nadhani ndio sababu hata ndugu mtangazaji akajichanganya.
Kikosi kamili siku hiyo kilikuwa kama ifuatavyo: Ivo Mapunda, Nadir Haroub, Salum Swedi, Erasto Nyoni, Amir Maftah (Malegesi Mwangwa 89’), Haruna Moshi, Nsajigwa Shadrack (Kadi Nyekundu 62), Henry Joseph
Shaaban Nditi, Said Maulid (Dani Mrwanda 78) na Nizar Khalfan. Kocha: Marcio Maximo
Hiyo ilikuwa Juni 16, 2007. Miaka 12 baadaye, katika tarehe kama ileile, Juni 16, 2019, kijana yule sasa akiwa na miaka 31, aliiongoza Stars katika mchezo wa juzi dhidi ya Zimbabwe kujiandaa na fainali za Afcon huko Misri.
Mchezo huo uliomalizika kwa sare ya 1-1 ulikuwa wa 63 kwa Nyoni ambaye alivaa kitambaa cha unahodha kuliongoza jahazi.
Katika wachezaji 11 walioanza, watatu walikuwa wakicheza mechi yao ya kwanza na Stars nao ni Metacha Mnata, Vincent Philip na Adi Yussuf. Ni Thomas Ulimwengu (aliyeanza kuichezea Stars 2011) na Gadiel Michael (aliyeanza kuichezea Stars 2014) ndiyo wanaweza kujiita wakongwe.
Katika michezo yake hiyo 63, Nyoni ameitumikia Stars katika mashindano mbalimbali kama inavyochanganuliwa hapa chini.
Mara 10 katika michuano ya kuwania kufuzu kwa Fainali za Kombe la Dunia. Mara 15 kwenye kufuzu fainali za Afcon.
Mara 9 kufuzu fainali za wachezaji wanaocheza vilabu vya ndani ya Afrika maarufu kama Chan. Mara 6 kwenye michuano ya Cosafa. Mara  15 kwenye mechi za kirafiki za kimataifa. Mara 8 kwenye michuano ya Cecafa Challenge Cup akiwa na timu ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars).

NYONI NI NANI?
Alizaliwa Mei 7, 1988 na alianzia soka lake katika kituo cha Rolling Stone cha Ally Mtumwa, jijini Arusha. Mwaka 2005 akamvutia Kocha Madaraka Bendera wa AFC ya jijini huko aliyemjumuisha kikosini akiwa kijana wa chini ya miaka 17.
Mwaka 2006 akajiunga na Vital’O ya Burundi kufuatia AFC kushuka daraja. Mwaka 2007 ndio akaitwa mara ya kwanza kwenye timu ya Taifa na Kocha Marcio Maximo.
Mwaka 2010 akarudi nyumbani kutoka Burundi na kujiunga na Azam FC. Mwaka 2017, Nyoni aliondoka Azam FC na kujiunga na Simba aliyonayo hadi sasa.
Mwaka 2019 anaiongoza Taifa Stars katika tarehe kama ileile aliyoichezea kwa mara ya kwanza.
Ni Erasto Nyoni, shujaa asiyeimbwa, licha ya kuifanyia Tanzania makubwa kupitia soka.

ADVERTISEMENT