In Summary

Kocha wa zamani Yanga, Kennedy Mwaisabula alisema wazo na Waziri ni zuri kwani ameona kabisa kwamba wachezaji wa ndani wanakosa nafasi ya kucheza kiasi cha kuifanya timu ya Taifa kuwa nyepesi.

WAZO lililotolewa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe juu ya kupendekeza kuwapo kwa kanuni ya kupunguza idadi ya nyota wa kigeni wanaoruhusiwa kucheza katika mechi moja, limewagawa wadau wa michezo.
Dk. Mwakyembe alitoa rai akitaka klabu zinazochuana kusajili nyota wa kigeni zijue mapema zinapaswa kutoa nafasi zaidi kwa wazawa akitaka idadi ya wachezaji 10 wa kigeni inayotumika kwa sasa ibadilishwe na kuwa watano tu kwa mechi moja, kauli hiyo imeibua mjadala kwa wadau nchini wengi wakiipinga, huku Bodi ya Ligi (TPLB) ikiwa ipo njia panda.
Akizungumza kwenye hafla ya Kubwa Kuliko iliyoandaliwa na Yanga kwa nia ya kufanya harambee ya kusaka Sh 1.5 Bilioni, Waziri Mwakyembe alisema kwa msimu ujao anataka kuona klabu zikitumia wachezaji watano tu katika mechi moja ili kuwapa nafasi wachezaji wa nyumbani nao kucheza kwa nia ya kulisaidia soka la Tanzania.
“Hata kama timu itakuwa na wachezaji zaidi ya 10 katika mchezo mmoja wanatakiwa wacheze watano tu, kwa sababu tunataka vijana wetu wainuke na kulisaidia taifa,” alisema Mwakyembe, lakini wadau wakiwamo viongozi wa klabu na makocha wamegawanyika.
Mwenyekiti wa Simba, Swedy Mkwabi alisema kupunguza idadi ya nyota kutoka 10 kwa mchezo mmoja itaondoa morali ya wazawa lakini mapro wanasajiliwa zaidi na klabu kama nne tu, lakini bado wengi hawapati nafasi ya kulitumikia taifa.
“Timu zenye uwezo wa  kutumia wachezaji wengi katika ligi ni Simba, Yanga na Azam na hao wengine hata kama wanakuwapo ni kwa idadi ndogo. Kwa maana hiyo dhana ya wachezaji wa kigeni kuwa wengi ligi inashindwa kuendelea si jambo sahihi, kwani hata miaka ya nyuma idadi ya wachezaji wa kigeni ilikuwa watano na bado tulishindwa kupiga hatua.”
“Serikali wanachotakiwa na kuanza kutengeneza mipango ya soka kuchezwa chini kama ilivyo zamani kuanzia shule ya msingi mpaka vyuo ili kupata wachezaji wenye vipaji, lakini msimu huu tumekuwa na idadi kubwa ya wachezaji wa kigeni katika timu moja tumefuzu Afcon, inaweza tukawapunguza tukashindwa kwani kuwepo kwa wageni wengi kunawapa mzuka na kuwafanya wajitume ili kuchuana nao,” alisema Mkwabi.
Naye Kocha wa Mwadui FC, Ally Bizimungu alisema wakipunguzwa wachezaji wa kigeni kutawafanya wazawa wabweteke na kuharibu zaidi timu ya Taifa.
“Hiyo hata nyumbani Rwanda waliwahi kupunguzwa wachezaji wa kigeni na timu ndiyo ikafanya vibaya. Kikubwa ni kwamba waendele kuwepo ili wawape changamoto wazawa na muda mwingine kuiga vitu vizuri kupitia wageni,” alisema.
Hata hivyo, Kocha wa zamani Yanga, Kennedy Mwaisabula alisema wazo na Waziri ni zuri kwani ameona kabisa kwamba wachezaji wa ndani wanakosa nafasi ya kucheza kiasi cha kuifanya timu ya Taifa kuwa nyepesi.
“Yupo sahihi, wazawa ni lazima wapate nafasi ya kucheza ili timu ya taifa iwe nzuri, Uingereza walikuwa na nyota wengi kutoka nje wengi kiasi cha kuwafanya wachezaji wao wa ndani kutoonyesha ushindani katika timu yao ya Taifa kwa miaka mingi mfululizo,” alisema Mwaisabula na kuongeza;
“Ni vyema wazo la Mwakyembe lipelekwe kwenye vyombo husika ili lipitishwe na wachezaji wazawa wacheze, kwa sasa linabaki kuwa wazo tu kwani halijapitishwa hadi mamlaka za soka zikutane, ila ingevutia sana.”
Mabosi wa Azam wamesema hawawezi kusema lolote kwa sababu wao ni miongoni mwa timu yenye kusajili na kutegemea nyota wa kigeni na wanasubiri kuona kwani huenda Waziri ameona kitu na wao hawawezi kupinga.

TPLB HAWA HAPA
Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi (TPLB) Stephen Mnguto alipoulizwa pendekezo hilo la Waziri Mwakyembe, alisema wameisikia kauli hiyo lakini hawakuwahi kukaa na wizara hiyo kujadiliana juu ya mabadiliko hayo kwa sasa wadau wasubiri.

ADVERTISEMENT