In Summary

Baada ya kuhakikishiwa ni kweli wachezaji hao mmoja akiwa na Mnamibia na mwingine Mghana wametua Jangwani, fasta akapendekeza mikataba ya awali aliyokuwa amesaini na nyota hao wa kigeni ichanwe ili nafasi zao zije kuchukuliwa na wakali wengine

Dar es Salaam. Kocha Patrick Aussems yupo likizo kwa sasa nchini Ufaransa, lakini amekuwa akiwasiliana na mabosi wake kujua kinachoendelea kwenye ishu za usajili na kushtushwa kusikia Yanga imesajili nyota nane, wakiwamo wawili aliokuwa amependekeza watue Msimbazi.
Baada ya kuhakikishiwa ni kweli wachezaji hao mmoja akiwa na Mnamibia na mwingine Mghana wametua Jangwani, fasta akapendekeza mikataba ya awali aliyokuwa amesaini na nyota hao wa kigeni ichanwe ili nafasi zao zije kuchukuliwa na wakali wengine ambao tayari ameelekeza wasajiliwe kwa msimu ujao wa Ligi Kuu na michuano ya kimataifa.
Mpaka jana Jumatatu, Yanga ilikuwa imeshasajili wachezaji nane, wakiwamo straika Mnamibia Sadney Urikhob kutoka timu ya Turo Magic na beki wa kati Mghana Lamine Moro aliyetokea Buildcon inayoshiriki Ligi Kuu ya Zambia ambao walishasainishwa mkataba wa awali ili watue Msimbazi.
Urikhob na Moro walifanya majaribio Simba kupitia michuano ya SportPesa Super Cup 2019 ambayo timu hiyo ikimaliza nafasi ya tatu na mabosi wa Msimbazi wakawasainisha mkataba wa awali kabla ya kuondoka nchini kurudi katika timu zao.
Lakini wakati wakiendelea kujadiliana juu ya usajili wa wachezaji hao, Yanga waliwaleta na kuwasainisha mikataba ya miaka miwili ili kuitumikia timu yao, ndipo Aussems akapelekewa taarifa naye kuamua kuwachania mikataba hiyo mara moja.
Aussems alisema wachezaji hao walikuja katika majaribio na kila mmoja alikuwa nao kwa zaidi ya wiki, hivyo aliamini labda msimu huu angekuwa nao badala ya dirisha dogo la usajili hata hivyo amesikia kilichotokea.
“Urikhob na Moro si wachezaji wabaya, ila kulingana na ambavyo nataka kuiona Simba msimu ujao, ila nimewaambia viongozi waachane nao hata kama walikuwa tayari wameshawasainisha mikataba ya awali,” alisema Aussems.
“Walikuja nchini kufanya majaribio na nilipendekeza hilo kwa wakati ule tulikuwa na shida ya kuongeza mchezaji hasa nafasi ya ulinzi kutokana tulikuwa na shida katika eneo hilo tulipokuwa tunashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika ,” aliongeza.
Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Crescentius Magori alisema Urikhob na Moro walitaka kuwasajili moja kwa moja kwani Kocha Aussems alikuwa anataka mshambuliaji na beki wa kati ambaye atakwenda kuongeza nguvu katika Ligi ya Mabingwa Afrika.
“Tuliwasainisha mikataba ya awali, ila Aussems hakuridhishwa nao,” alisema.

ADVERTISEMENT