In Summary

Akiitoa rangi serikali ya Joho, Mwalala alisema itakuwa aibu kubwa sana kwa Bandari kulazimika kuhosti mechi zao za nyumbani mjini Nairobi wakati uwanja wanao sema ni ovyo na mamlka inayostahili kuichangamikia na kuiboresha wala hata haijishughulishi.

Nairobi. KOCHA wa Bandari FC, Bernard Mwalala kamtoa rangi Gavana wa kaunti ya Mombasa, Ali Hassan Joho kwa kushindwa kuukarabati Uwanja wa Mbaraki ili kuiwezesha kuchezesha mechi za kimataifa.
Bandari timu ya pekee inayowakilisha mkoa wa Pwani ilifanikiwa kujikatia tiketi ya kushiriki dimba la CAF Confederation msimu ujao baada ya kutwaa ubingwa wa Kombe la GOTV Shield Cup.
Hata hivyo, licha ya kufuzu, Bandari watalazimika kuchezea mechi zao za nyumbani mbali na nyumbani kutokana na uwanja wao wa Mbaraki kutokidhi viwango vya kimataifa vinavyotakiwa na CAF.
Kulingana na kocha Mwalala wa kulaumia ni serikali ya kaunti inayoongozwa na Gavana Joho kwa kulalia masikio kazini.
Akiitoa rangi serikali ya Joho, Mwalala alisema itakuwa aibu kubwa sana kwa Bandari kulazimika kuhosti mechi zao za nyumbani mjini Nairobi wakati uwanja wanao sema ni ovyo na mamlka inayostahili kuichangamikia na kuiboresha wala hata haijishughulishi.
“Ni kitu cha aibu kwa kweli. Ukiangalia sehemu ambazo hata soka halina mashiko kama vile Machakos, wanao uwanja wa wa kuchezesha mechi ya levo hizi.
“Kisha unajiita kaunti 001 lakini unashindwa kuwa na uwanja wa maana. Serikali ya kaunti inazembea kwa kweli. Tunatokea Mombasa lakini hatuwezi kucheza mechi zetu za nyumbani huku.
“Mombasa ni mji mkubwa tena wa kitaliii, unajulikana kote duniani lakini haina uwezo wa kuchezesha mechi za kimataifa. Inachekesha” Mwalala mwenye machungu katiririka.
Kulingana na jinsi uwanja wa Mbaraki ulivyo, CAF kamwe haiwezi kuidhinisha kutumika kwa mechi zake. uwanja mbadala ni ule wa Manispaa ya Mombasa lakini nao hauwezi kutumika kwa kuwa umefungwa kutokana na kuwa katika hali mbaya zaidi, ukiwa umeota makwekwe.
Kwa miezi kadhaa kumekuwa na kelele za kuufanyia ukarabati kutoka kwa kaunti  lakini mpaka sasa hamna kinachoendelea.

ADVERTISEMENT