In Summary

Said Mtupa alikuwa winga wa zamani wa Tanzania Prisons, Kahama United na Tukuyu United pia amewahi kuitwa timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars’.

Dar es Salaam. Wanasoka mbalimbali wamejitokeza Mbagala jijini Dar es Salaam kumpumzisha mpendwa wao Said Mtupa aliyefariki dunia, Jumapili ya Juni 16 kwa ajali pikipiki jijini Mbeya.

Nahodha wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Shadrack Nsajigwa aliongoza wanasoka wenzake katika mazishi ya winga huyo wa zamani wa Tanzania Prisons yaliyofanyika katika makaburi ya Kwa mzee Seif, Mbagala kwa Selenge.

Mbali na Nsajingwa wanasoka wengine wa zamani na sasa waliojitokeza kwenye msiba huo ni Kenny Ally, Hassan Kapalata, Kelvin Friday na kaka wa Mbwana Samatta, Mohammed.

Wengine ni baba yake Mbwana, mzee Samatta pamoja na  wachezaji wote wa timu ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 wa Tanzania Prisons ambao wapo chini ya kaka wa marehemu, aitwaye Shaaban.

Shaaban ambaye ni kocha wa vijana wa Tanzania Prisons, alisema mdogo wake ameacha mke na watoto watano ni pigo kwenye familia yao.

"Alinikuta Prisons. Hakuwa mdogo tu kwangu alikuwa zaidi ya ndugu nakumbuka tulivyokuwa tukiishi miaka ya nyuma wakati tunacheza pamoja, lakini haya ni mapenzi ya Mungu," alisema kaka huyo wa marehemu.

Msemaji wa familia ya Mtupa kaka yeka Omary alisema watamuenzi kwa mazuri ambayo amewaachia.

"Alipata ajali eneo moja linaitwa Iwambi, Mbeya alifia pale pale mwili wake ukaenda kuhifadhiwa hospitali ya rufaa Mbeya," alisema Omary.

ADVERTISEMENT