In Summary

Kwa mujibu wa chombo maarufu cha habari nchini Hispania, L’Equipe wanadai PSG wapo tayari kumuuza nyota huyo wa kimataifa wa Brazil endapo watapokea ofa mwafaka kwa mujibu wa tathimini yao kuhusu Neymar.

Paris, Ufaransa. DIRISHA hili la uhamisho kazi ipo. Tayari Eden Hazard ameuzwa lakini inaelekea kuna mastaa wengi wakubwa watafutaa nyayo zake. Sasa kuna mshikemshike unaendelea kati ya mastaa wawili wakubwa, Neymar wa PSG na Paul Pogba wa Manchester United.
Wakati Pogba juzi akitangaza ana mpango wa kuondoka Manchester United, PSG wao inadaiwa wapo tayari kuachana na staa wao, Neymar na wala hana haja ya kuwasilisha maombi ya kuuzwa klabuni hapo.
Kwa mujibu wa chombo maarufu cha habari nchini Hispania, L’Equipe wanadai PSG wapo tayari kumuuza nyota huyo wa kimataifa wa Brazil endapo watapokea ofa mwafaka kwa mujibu wa tathimini yao kuhusu Neymar.
Hii imekuja baada ya Rais wa PSG, Nasser Al’ Khelaifi kudai wanataka kuondoa ‘tabia za ustaa’ katika kikosi chao huku mlengwa wa kauli hiyo akiwa ni Neymar aliyenunuliwa mwaka 2017 kwa Pauni 198 milioni na kuvunja rekodi ya uhamisho ya dunia.
“Wachezaji itabidi warudi katika majukumu yao sana kuliko ilivyokuwa awali. Lazima safari hii iwe tofauti kabisa. Itabidi wafanye kazi nzito zaidi. Hawapo hapa kwa ajili ya kujifanyia wanachotaka. Kama hawakubali basi milango ipo wazi. Kwaheri. Sitaki wachezaji wenye tabia za kistaa tena,” alisema Al-Khelaifi.
Neymar ameshindwa kabisa kuonyesha makali tangu atue kutoka Barcelona na mara nyingi amekuwa akiandamwa na majeraha huku pia akihusishwa kurudi Hispania na imedaiwa amechoshwa na maisha ya Ufaransa.
Hata hivyo, ripoti zinadai Neymar hana mpango wa kutua Santiago Bernabeu na badala yake anapenda zaidi kurudi Barcelona. Kwa sasa anauguza majeraha yake ya kifundo cha mguu baada ya kuumia katika pambano la kirafiki la Brazil dhidi ya Qatar wiki iliyopita na ataikosa michuano ya Copa Amerika inayoendelea nchini kwao Brazil.
Kwa sasa amekuwa akipambana na kesi yake inayomkabili dhidi ya mwanamke mmoja nchini Ufaransa na anashutumiwa kumbaka mwanamke huyo. Msimu huu ameanza mechi 16 tu za Ligi nchini Ufaransa lakini PSG chini ya Kylian Mbappe imefanikiwa kuchukua tena ubingwa.
Wakati PSG ikianza kuwaka moto, upande wa Pogba klabu yake imegoma kumruhusu aondoke baada ya juzi jijini Tokyo akiwa katika promosheni ya kampuni ya Adidas kudai anajisikia kwenda kupata changamoto mpya kwingine.
“Kuna maongezi mengi yanaendelea na kuna mawazo mengi pia. Kwangu mimi nimekuwa Manchester kwa miaka mitatu na nimekuwa nikifanya vema. Kuna nyakati nzuri na kuna nyakati mbaya, kama kila mtu, kama sehemu nyingine tu. Baada ya msimu huu na kila kitu ambacho kimetokea msimu hu, huku ukiwa ni msimu wangu bora pia, nadhani ingekuwa muda mzuri kwangu kutafuta changamoto mpya kwingine. Nafikiria hilo,” alisema Pogba.
Mabosi wa United inadaiwa wamekerwa na kitendo cha staa huyo wa kimataifa wa Ufaransa kwenda hadharani na kutoa madai hayo huku akiwa ana mkataba wa miaka miwili ambao pia una kipengele cha kuongezewa mwaka mmoja.
Real Madrid na Juventus zinamsaka kiungo huyo kwa nguvu na kwa upande wa Madrid inadaiwa kuwa baada ya kufanikiwa kumnasa winga wa kimataifa wa Ubelgiji, Eden Hazard kutoka Chelsea sasa wameelekeza nguvu zao kwa Pogba.
Machi mwaka huu, Pogba akiwa katika mechi za kimataifa na Ufaransa alidokeza nia yake ya kucheza Madrid huku akidai ni ndoto ya kila mchezaji kucheza Real Madrid chini ya kocha, Zinedine Zidane. Zidane aliipokea kauli hiyo kwa kusema:
“Kama siku moja akitaka kuondoka United….kwanini asije Real Madrid?”
Kwa upande wa Juventus inaeleweka Mkurugenzi wa Ufundi wa klabu hiyo, Fabio Paratici alikuwa katika ofisi za United zilizopo jijini London kwa ajili ya kuangalia uwezekano wa kumrudisha staa huyo Turin miaka mitatu baada ya kuondoka kwenda Old Trafford.

ADVERTISEMENT