In Summary

Picha kadhaa ziizosambaa kwenye mitandao ya jamii, inamuonesha beki huyo asiyekuwa na masihara, akiwa na ndevu nyeupe, muonekano unaomfanya aonekane 'mzee '.

Nairobi. Katika fainali za Kombe la Euro zilizofanyika mwaka 2000, yakiandaliwa na Hispania kwa ushirikiano na Austria, Ufaransa wakiibuka mabingwa, walikuwa na mtu aliyeitwa Djibril Cisse kikosini. Mbali na kasi yake, Cisse alikuwa maarufu kwa muonekano wake wa nywele.

Kawaida yake ilikuwa ni kubadili mitindo ya nywele mara nyingi, akiweka muonekano wa kizee, yaani kupaka nywele na ndevu zake rangi nyeupe. Mwaka 2002, katika fainali za mataifa ya Afrika, zilizofanyika nchini Mali, Rigobert Song, ambaye alikuwa nahodha wa mabingwa wa makala hayo, Cameroon, naye aliweka muonekano wa kizee.

Mwaka 2000 baada ya umri wa wachezaji kutajwa watu walichonga sana kuhusu umri na muonekano wa Cisse. Mwaka 2002 vilevile, mashabiki walichonga Sana kuhusu umri wa 'Babu' Song. Tofauti kati ya mifano hii ikiwa ni kwamba, Song licha ya kuweka rangi umri wake ulikuwa kweli umekimbia.

Miaka 17 baadae historia imejirudia mwanangu, safari hii ikitokea katika kikosi cha Kenya. Baada ya Kocha mkuu wa Harambee Stars, Sebastien Migne kutangaza kikosi cha Wachezaji 23 wanaokwenda Cairo, kilichofuata ni shirikisho la soka nchini (FKF), kuweka bayana data za jeshi hilo.

Baadhi ya mambo ambayo, huwekwa wazi kisheria, ni umri wa wachezaji. Hapo ndipo mjadala ulipoanza kwenye majukwaa ya michezo na mitandao ya jamii. Kwa wiki nzima Harambee Stars ikawa inatrendi tu kwenye Facebook na twitter. Gumzo ni umri wa baadhi ya nyota wa Stars.

Wachezaji ambao umri wao ulionekana kutiliwa shaka ni nahodha Victor Wanyama, kipa Farouk Shikalo anayekwenda Yanga na beki Joash Onyango. Kwa mujibu wa data hizo, ilionekana kuwa Wanyama ana miaka 26, Shikalo 22 na beki kisiki wa Gor Mahia, Joash 'the Berlin Wall' akadaiwa kuwa na miaka 26. Wadau hawakuridhika unaambiwa!

Hiyo sio ishu, ni hivi baada ya taarifa kufika huko kambini Paris, Ufaransa, kwamba eti wadau wa soka wanateta kuhusu umri wao, wachezaji hao, wakiongozwa na Joash, walimaindi vibaya sana. Mambo yakatulia na maisha yakaendelea.

Leo Juni 18, siku moja kabla timu iaanze Safari ya kuelekea Cairo, kwa ajili ya fainali za AFCON, Joash ameliamsha tena. Picha kadhaa ziizosambaa kwenye mitandao ya jamii, inamuonesha beki huyo asiyekuwa na masihara, akiwa na ndevu nyeupe, muonekano unaomfanya aonekane 'mzee '.

Kitendo hicho wengi wanalitafsiri kama hatua ya kuwajibu watu ambao wamekuwa wakichonga kuhusu umri wake. Aidha mbali na dhihaka yake kwa wapinzani wake, wachambuzi wa mambo wanaitabiri kuwa bishara njema kwa Kenya, katika fainali hizo.

Tusiandikie mate, ila historia inaonesha kuwa, Cisse alipoweka nywele rangi Ufaransa walitwaa ubingwa wa EURO 2000, miaka miwili baadae Cameroon wakatwaa ubingwa wa AFCON, miaka 17 baadae twenzetu Cairo, tukashuhudie buradani ya kukata na shoka itakayoanza Ijumaa hii hadi Julai 19.

ADVERTISEMENT