In Summary

Ingawa James hakucheza lakini bado kiwango chake kiliishawishi Swansea kumpa mkataba wa miaka mitatu. Aliwekwa katika benchi katika pambano la Ligi Kuu dhidi ya Stoke.

MANCHESTER, ENGLAND. HATIMAYE Kocha wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer amefanya usajili wake wa kwanza akiwa kocha wa timu hiyo.
 Kuelekea msimu ujao ameamua kumnasa winga mahiri wa kimataifa wa Wales, Daniel James kutoka Klabu ya Swansea kwa dau la Pauni 18 milioni. Ni nani kijana huyu aliyepewa sifa nyingi?

Mtoto wa Wales, azaliwa England
Jina lake kamili ni Daniel Owen James na alizaliwa katika eneo la Kingston upon Hull, England Novemba 10, 1997 ingawa baba yake ni raia wa Wales. Baadaye alisoma katika Shule ya South Hunsley School. James alianza kucheza katika shule ya soka ya klabu ya Hull City kabla ya kuonwa na maskauti wa klabu ya Swansea City waliomnunua kwa dau la Pauni 72,000 mwaka 2014. Hapohapo akaingia katika kikosi cha chini ya umri wa miaka 18.
Msimu wa 2016–17, James alikuwa sehemu ya kikosi cha chini ya umri wa miaka 23 cha Swansea ambacho kilipanda kwenda daraja la kwanza wakishinda ubingwa kwa tofauti ya pointi 11. Lakini pia akaonyesha kipaji kikubwa katika michuano mbalimbali.
Kutokana na kuonyesha kiwango kikubwa hatimaye James alijumuishwa katika kikosi cha kwanza cha Swansea kwa mara ya kwanza Januari 2016 katika pambano la FA dhidi ya Oxford United ambapo walipoteza mechi hiyo.
Ingawa James hakucheza lakini bado kiwango chake kiliishawishi Swansea kumpa mkataba wa miaka mitatu. Aliwekwa katika benchi katika pambano la Ligi Kuu dhidi ya Stoke.
Juni 30, 2017 James alipelekwa kwa mkopo katika klabu ya daraja la pili ya Shrewsbury Town mpaka mwisho wa msimu. Hata hivyo, mkopo huo ulikoma Agosti 31, 2017 aliposhindwa kulazimisha kuingia katika kikosi cha kwanza.
Mechi pekee ambayo alijumuishwa katika kipindi hicho cha mkopo ilikuja katika pambano la raundi ya kwanza Kombe la Ligi dhidi ya Nottingham Forest ambapo hata hivyo hakutumika.  Februari 6, 2018 aliichezea Swansea mechi ya kwanza akiingia uwanjani dakika za mwisho katika pambano la FA dhidi ya Notts County ambalo walishinda 8-1. Aliingia dakika ya 82 na kufunga bao moja.
Alicheza mechi yake ya kwanza kamili kwa Swansea katika pambano la Ligi Daraja la Kwanza dhidi ya Birmingham City Agosti 17, 2018  huku pambano hilo likimalizika bila ya kufungana. Alifunga bao lake la kwanza kwa klabu Novemba 24, 2018 wakati walipochapwa nyumbani 4-1 na Norwich City.
Kufikia Desemba 2018 huku James akiwa mchezaji wa kudumu Swansea na mmoja kati ya wachezaji waliokuwa wanaonyesha kiwango kizuri, kocha wake, Graham Potter aliripoti kwamba klabu yake ilikuwa imeanzisha mazungumzo ya mkataba mpya na staa huyo.
Pamoja na mjadala uliokuwa unaendelea kuhusu yeye kuhamia Leeds United katika dirisha la Januari mwaka huu, James alitajwa katika kikosi cha kwanza cha Swansea ambacho kilitarajiwa kucheza na Birmingham City Januari 29. Katika pambano hilo alifunga bao lake la pili la msimu katika pambano ambalo lilimalizika kwa sare ya 3-3.

apeperuka leeds
Januari 31, 2019, huku James akielezea tamaa yake ya kutua Leeds United, dau la Pauni 10 milioni lilikubaliwa baina ya klabu hizo na James alikwenda kukubaliana maslahi binafsi na Leeds huku akipimwa afya yake.
Baadaye akafanya mahojiano huku akipigwa picha katika jezi ya klabu yake mpya kwa ajili ya kusubiri dili kukamilika. Dakika za mwisho ziliibuka habari kwamba kulikuwa na kutokukubaliana kuhusu jinsi ya malipo ya dau lake baina ya mmiliki wa Swansea na watu wa Leeds.
Aliachwa katika Uwanja wa Elland Road akisubiri hatima yake lakini mwishowe dili hilo lilivunjika huku likimuacha James na wakala wake wakiwa na hasira. Mwishoni mwa msimu, Kocha wa Leeds, Marcelo Bielsa aligoma kuilaumu timu yake kwa kushindwa kukamilisha uhamisho huo.

Atua United na sifa kibao
Juni 6, 2019, James alifanyiwa vipimo vya afya Manchester United baada ya klabu hiyo kukubaliwa dau la Pauni 15 milioni ambalo litapanda mpaka Pauni 17 milioni kutegemeana na kiwango chake. Baadaye ilitangazwa United na Swansea zimekubaliana na dau. James anawasili na sifa ya kuwa winga mwenye kasi kubwa na maarifa mengi huku akionekana kuwa staa ajaye katika soka la Kiingereza kutokana na baadhi ya wachambuzi kudai anafanana na Cristiano Ronaldo wa utotoni.
James ana uwezo wa kucheza pembeni lakini pia ana uwezo wa kucheza katikati. Kutua kwake Manchester United kunamfanya apambane kutinga katika kikosi cha kwanza moja kwa moja na sio kusubiri nafasi yake siku za usoni.

Aitosa England, Akiwa amezaliwa England, James alikuwa na uwezo wa kucheza Timu ya Taifa ya England au Timu ya Taifa la Wales ambalo ni taifa la baba yake, Kevin aliyezaliwa Wales katika Mji wa Abderdare. Ameichezea Wales katika ngazi za soka la vijana na aliifungia Wales U20 bao pekee katika ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Bahrain.
Aliitwa kwa mara ya kwanza katika kikosi cha wakubwa katika pambano la kufuzu Kombe la Dunia 2018 dhidi ya Serbia 2017 chini ya Kocha, Chris Coleman. Hata hivyo, mechi yake ya kwanza alicheza chini ya Kocha, Ryan Giggs Novemba 2018 dhidi ya Albania akicheza dakika 58 za mechi hiyo. Aliifungia Wales bao la kwanza katika mechi yake ya pili tu dhidi ya Slovakia dakika ya kwanza huku ikiwa ni mechi  ya kwanza uwanja wa nyumbani.

ADVERTISEMENT