In Summary

Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mnigeria Emmanuel Amunike katika mazoezi yake ya mwisho akitoa mbinu za nyota kukaba na kushambulia kwa pamoja, alifichua wachezaji saba aliowapiga chini akiwamo Jonas Mkude na Ibrahim Ajibu.

Dar es Salaam. Kikosi cha timu ya Taifa Tanzania kimeondoka jana mchana kuelekea nchini Misri kwa ajili ya kuweka kambi ya wiki mbili wakijiandaa na Fainali za Afcon 2019 zitakazoanza Juni 21.
Kikosi hicho kimeondoka na wachezaji 32 ambao  watachujwa baadaye ili kubakia 23 watakaokinukisha katika fainali hizo za 32 ambazo kwa mara ya kwanza zitashirikisha mataifa 24.
Awali fainali hizo zilikuwa zikishirikisha nchi 16 tu, lakini mabadiliko makubwa yaliyofanywa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limesaidia kuongeza idadi hiyo mpya na Tanzania imefuzu kwa mara ya pili baada ya awali kushiriki fainali za 1980 nchini Nigeria.
Kabla ya kutimka zao, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mnigeria Emmanuel Amunike katika mazoezi yake ya mwisho akitoa mbinu za nyota kukaba na kushambulia kwa pamoja, alifichua wachezaji saba aliowapiga chini akiwamo Jonas Mkude na Ibrahim Ajibu.
Nyota hao wanaokipiga Simba na Yanga wamekuwa na msimu mzuri ndani ya klabu zao, lakini nidhamu mbovu waliyoionyesha kwenye kambi ya Stars imemfanya Kocha Amunike kuwapiga chini.

TIZI KALI
Katika mazoezi ya mwisho yaliyofanyika katika Uwanja wa Taifa jijini Dar, Amunike aliwapanga wachezaji kwa nafasi zao na kisha kutoa mazoezi ya namna ya kukaba na kushambulia kwa pamoja na mazoezi hayo yalionekana kueleweka.
Baada ya mazoezi hayo Amunike aligawa vikosi viwili na kucheza, huku akiangalia namna ambavyo mazoezi aliyowapa wachezaji wake yanafanya kazi.
Kikosi cha kwanza kilikuwa na Aishi Manula, Aggrey Morris, Vincent Andrew, Gadiel Michael, Frank Domayo, Feisal Salum, Farid Mussa, Thomas Ulimwengu, Mbwana Samatta na Simon Msuva, huku cha kikosi cha pili kikiongozwa na Aaron Kalambo na David Mwantika.
Wengine walikuwa ni; Hassan Kessy, Abdi Banda, Fred Tangalu, Yahya Zayd, Miraj Athuman, Shiza Kichuya, Shaaban Chilunda na Adi Yusuph.
Kwenye kikosi cha kwanza kuanzia eneo la kiungo lililokuwa chini ya Frank Domayo na Feisal Salum, walionyesha kuelewana vya kutosha kwani wote walikuwa wakikaba na kupiga pasi.
Huku Simon Msuva na Mbwana Samatta nao wakicheza kwa maelewano, huku spidi yao ikigeuka kuwa changamoto kwa mabeki David Mwantika na Abdi Banda, huku kila mchezaji akionyesha makeke kulingana na walivyoelekezwa na Kocha Amunike.

AJIBU, MKUDE
Katika kikosi ambacho kimefanya mazoezi ya mwisho jana, Ibrahim Ajibu na Jonas Mkude hawakuwepo na Amunike alitaja sababu zilizofanya waondolewe.
Kocha Amunike alianika sababu ya kuwatema nyota wao wanaokipiga Simba na Yanga sambamba na wengine ikiwamo suala la nidhamu na kuwa majeruhi, huku akisisitiza anaamini jeshi analoenda nao Misri litafanya kweli kwenye fainali hizo za 32.
Mkude amekuwa mmoja ya nyota tegemeo wa Simba tangu alipopandishwa kikosini msimu wa 2011-12 na kuwepo kwenye kikosi kilichoinyoa Yanga mabao 5-0, Mei 6, 2012, huku Ajibu akiibeba Yanga msimu huu ikimaliza nafasi ya pili kwenye msimamo.
Ajibu aliyesajiliwa Yanga misimu miwili iliyopita akitokea Simba na amekuwa na msimu mzuri akiasisti mabao 16 na kufunga mengine sita, japo kiwango chake kimekuwa hakitabiriki kiasi cha kukosa nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha Mwinyi Zahera.
Upande wa Mkude amekuwa mchezaji muhimu katika kikosi cha kwanza Simba huku akiisadia timu hiyo kuchukua kombe la Ligi Kuu, lakini pia kuifikisha timu katika hatua ya robo fainali klabu bingwa Afrika msimu huu.
MSIKIE AMUNIKE
“Najua kila mtu ana mchezaji wake na akiona wachezaji hawa wamekosekana katika kikosi changu wanakuwa na mawazo tofauti, mimi naangalia mchezaji mwenye nidhamu pamoja na kujituma mazoezini, isingekuwa nidhamu hata mimi mwenyewe nisingekuwa katika kikosi cha Barcelona au kucheza kwa mafanikio, kwangu mimi nidhamu ndiyo jambo la kwanza,” alisema.
Pamoja na Ajibu na Mkude, wengine waliotemwa ni Ali Ali, Ayoub Lyanga, Shomari Kapombe, Kassim Hamis, Kennedy Wilson.  
WALIOSEPA HAWA
Makipa: Aishi Manula (Simba SC), Metacha Mnata (Mbao), Aaron Kalambo (Tz Prisons), Seleman Salula (Malindi) na Claryo Boniface (U20)

Mabeki: Hassan Kessy (Nkana, Zambia), Vincent Philipo (Mbao), Gadiel Michael (Yanga), Mohamed Hussein (Simba), Ally Sonso (Lipuli), Erasto Nyoni (Simba), Kelvin Yondani (Yanga), David Mwantika (Azam), Aggrey Morris (Azam) na Abdi Banda (Baroka, Afrika Kusini)

Viungo:
Himid Mao (Petrojet, Misri), Mudathir Yahya (Azam), Feisal Salum (Yanga), Fred Tangalu (Lipuli), Frank Domayo (Azam), Saimon Msuva (Difaa El Jadid, Morocco), Shiza Kichuya (ENPPI, Misri), Farid Mussa (Tenerife, Hispania), Miraj Athumani (Lipuli), Yahya Zayd (Ismaily, Misri)

Washambuliaji:
Thomas Ulimwengu (JS Soura, Algeria), Shaaban Idd Chilunda (Tenerife, Hispania), John Bocco (Simba), Mbwana Samatta (Genk, Ubelgiji), Kelvin John ‘Mbappe’ (U17), Rashid Mandawa (BDF, Botswana) na Adi Yusuf (Blackpool, England).

ADVERTISEMENT