In Summary

Sevilla ndio timu ya kwanza inayoshiriki Ligi Kuu ya Hispania kutua kufanya ziara Tanzania na katika mchezo huo wa kimataifa wa kirafiki, iliibamiza Simba kwa mabao 5-4

Dar es Salaam. Tukio la mshambuliaji wa Simba, Adam Salamba kuonekana akimuomba nyota a Sevilla, Ever Banega ampatie viatu mara baada ya kumalizika kwa mechi ya kirafiki baina ya timu hizo juzi, limeonekana kuwa gumzo kwa wadau wa mpira wa miguu nchini.

Wapo wanaoamini kuwa mshambuliaji huyo alifanya jambo sahihi kwa sababu tukio la namna hiyo limekaa kihisia na sio jambo baya kwa sababu inamuachia kumbukumbu mchezaji ya kucheza mechi kubwa na kukutana na mchezaji wa daraja la juu kama Banega.

Upo upande unaoamini pia kuwa Salamba hakupaswa kuomba viatu na badala yake angeweza kuomba jezi iliyotumiwa na mchezaji huyo kama ambavyo imezoeleka kwa wachezaji mbalimbali duniani.

Hata hivyo kiuhalisia suala la mchezaji kuomba au kupewa jezi, viatu au vifaa vingine na mchezaji wa timu nyingine na ifuatayo ni orodha ya matukio yaliyowahi kushuhudiwa ya wachezaji wakifanya hivyo.

Eto'o kuomba jezi ya Cannavaro wa Stars

Juni 21, 2008, timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' ilichapwa mabao 2-1 na Cameroon kwenye mechi ya kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia mwaka 2010.

Katika mchezo huo, Eto'o aliyekuwa anachezea Barcelona licha ya kupachika mabao mawili, alidhibitiwa vilivyo na beki wa Yanga, Nadir Haroub 'Cannavaro' ambaye pia alicheza vizuri pindi timu hizo zilipokutana Dar es Salaam.

Baada ya mchezo huo kumalizika, Eto'o kwa kuonyesha kuikubali kazi ya Cannavaro, alimkimbilia beki huyo na kumuomba wabadilishane jezi jambo ambalo Cannavaro hakuonyesha hiyana na wakabadilishana ingawa baadaye Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) lilitangaza kumkata posho beki huyo ili kufidia gharama ya jezi.

El Shaarawy kumuomba jezi Messi

Mwaka 2013, Barcelona ilicheza na AC Milan na mara baada ya mechi hiyo kumalizika, mshambuliaji Stephan El Shaarawy alimkimbilia kwa haraka mshambuliaji nyota wa Barcelona, Lionel Messi na kumuomba wabadilishane jezi lakini katika hali ya kushangaza, Messi alimgomea.

Ronaldo kuombwa jezi Israel

Mwaka 2017 timu ya Taifa ya Ureno ilicheza mechi ya kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia dhidi ya Israel na pindi mpira ulipomalizika, mmoja wa wachezaji wa Israel alimfuata Cristiano Ronaldo na kumuomba jezi lakini mshambuliaji huyo alipinga kwa kile alichokisema kwamba alifanya hivyo makusudi ili aonyeshe kutounga mkono namna Israel inayoionea Palestina.

 

Andre Santos kumuomba jezi Van Persie

Mwaka 2012 beki Andre Santos wa Arsenal aliwakera mashabiki wa timu hiyo baada ya kumuomba jezi mshambuliaji wa Manchester United, Robin Van Persie ambaye wakati huo alikuwa ametoka kuihama timu yao na kujiunga na mahasimu wao hao.

Kilichowakera zaidi Arsenal ni kuwa Santos siku hiyo alifanya makosa ya kizembe yaliyopelekea timu yake kuchapwa mabao 2-1.

Raja Casablanca kumuibia jezi, viatu vya Gaucho

Mwaka 2013, timu ya Raja Casablanca ya Morocco ilicheza dhidi ya Atletico Mineiro ambayo kwenye kikosi chake ilimjuisha kiungo mshambuliaji Ronaldinho Gaucho aliyewahi kuwika kwenye soka duniani.

Katika mchezo huo ambao Raj Casablanca waliibuka na ushindi wa mabao 3-1, wachezaji wake waligeuka kituko baada ya kumuibia Gaucho, jezi, viatu, soka na hata vifaa vingine ilimradi tu wabaki na kumbukumbu ya kucheza naye.

ADVERTISEMENT