In Summary

Mke wa kipa, Juma Kaseja ameshinda tuzo ya wanawake katika masuala ya kuwaremba watu, huku akieleza ana deni kubwa kwa walaiomuamini

Dar es Salaam. Nasra Kaseja mke wa wa kipa wa klabu ya KMC, Juma Kaseja, ameshinda tuzo za African Women Film Festival (AWAFFEST).

Tuzo hizo zilifanyika usiku wa jana Machi 31, 2019 katika ukumbi wa makumbusho ya Taifa, huku vipengele 24 vikiwa vinawania.

Kwa upande wake Nasra aliibuka kidedea kupitia kampuni yake ya Nasralicious Kaseja katika kipengele cha mrembaji bora na kuwapiga chini aliokuwa akishindana nao  akiwemo Tunu Designs, Flolina Beauty, Eve Makeover na Bic Glam Beauty.

Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo Nasra amesema ana deni kubwa  kwa waliompigia kura na kuahidi hatowaangusha.

“Moja ya mambo nitakayoyafanya katika kurudisha deni hilo ni pamoja na kuzalisha wapambaji wengine kazi ambayo naenda kuianza mara moja, amini sitawaangusha mlioniamini na kunipigia kura,”amesema Nasra.

Awali muandaaji wa tuzo hizo, ambaye ni msanii wa filami, Yvonne Cherrie ‘Monalisa’, amesema ameamua kuja na tuzo hizo kama moja ya njia ya kutambua mchango wa wanawake katika tasnia ya sanaa mbalimbali.

Monalisa amesema tuzo hizo zilitanguliwa na kufanyika kwa maonyesho ya siku tatu katika kijiji cha Makumbusho Kijitonyama yalioyanzi Machi 29 hadi 31, 2019  ambapo pamoja na mambo mengine wanawake walionyesha kazi zao.

Mbali na Nasra wasanii wengine waliibuka kidedea na vipengele walivyoshinda kwenye mabano ni Riyama Ally (msanii bora wa filamu), Vannesa Mdee (mtumbuizaji bora),  Hellen George’Ruby’(mtumbuizaji bora) , Dina Marios (mwandishi wa habari bora) huku tuzo ya heshima ikienda kwa Hadija Kopa.

Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu, Joyce Fisoo, alisema Monalisa ameonyesha uthubutu, na kushauri litakapofanyika tena mwakani watu wengi wajitokeze huku akiahidi serikali kuendelea kumuunga mkono katika juhudi zake hizo a kuwatambua wanawake.

ADVERTISEMENT