In Summary

Serikali kupitia Wizara ya michezo iliachia Sh25 milioni ikiwa ni sehemu ya Sh244 milioni iliyotengewa kuigharamia Stars kwenye mashindano yake yajayo ya kimataifa.

HATIMAYE serikali imeachia Sh25 milioni kugharamia msafara wa Timu ya Taifa Harambee Stars, kuelekea Accra kwa ajili ya kuchuana na Ghana Jumamosi ya wiki hii kwenye dimba la AFCON 2019.
Haya yanajiri baada ya kocha Mfaransa, Sebastian Migne kucharuka na kusema kwamba kachoshwa na mahangaiko ya kifedha ambayo amekuwa akilazimika kupitia ili kuiandaa timu hiyo.
“Inakuwa vigumu kuandaa timu na hata kutoa ushindani wa maana unapoishi kuwa na hofu kama hizi. Kwa kweli nimechoka kufanya kazi katika mazingara haya. Kwa upande wangu nimejitahidi kutoa mchango kwa asilimia 100% ila hufikia wakati mtu akachoka. Kama kweli serikali ina nia ya kuina Stars ikifika mbali, basi suala la kuwezesha vilivyo wanapaswa kulichukua kwa uzito,” Migne alilalama.
Siku moja baada ya malalamishi ya kocha Migne, serikali kupitia Wizara ya michezo iliachia Sh25 milioni ikiwa ni sehemu ya Sh244 milioni iliyotengewa kuigharamia Stars kwenye mashindano yake yajayo ya kimataifa.
Afisa mawasiliano wa Shirikisho la soka nchini FKF, Barry Otieno kadhibitisha. Stars inakutana na Ghana ugenini kwenye mechi ya mwisho ya kundi lao, timu hizo zikiwa tayari zishafuzu. Stars inaongoza kwa pointi saba moja zaidi ya nambari mbili Ghana, ambayo itakuwa ikisaka kulipiza kisasi cha goli 1-0 waliyopokezwa Nairobi. Timu hizo zitachuana kwenye mechi hiyo kesho kutwa Jumamosi usiku katika Uwanja wa Ohen Djan Sports.

ADVERTISEMENT