In Summary

Ngoma alijiunga na Azam FC, Juni 11 mwaka jana akitokea Yanga ambayo ilivunja mkataba naye baada ya kusumbuliwa na majeraha ya muda mrefu.

Dar es Salaam. Klabu ya Azam FC leo imemuongezea mkataba wa mwaka mmoja, mshambuliaji wake Donald Ngoma kutoka Zimbabwe.

Nyota huyo aliyeifungia Azam FC mabao saba kwenye Ligi Kuu msimu huu, alijiunga na timu hiyo Juni mwaka jana kwa mkataba wa mwaka mmoja ambao sasa ulikuwa umebakiza muda wa miezi mitatu kabla ya kumalizika kwake.

Ofisa Habari wa Azam FC, Jaffer Iddi alisema baada ya mazungumzo baina ya klabu hiyo na Ngoma, mshambuliaji huyo ameamua kusaini mkataba mpya utakaomfanya aendelee kusalia klabuni hapo.

"Kikosi cha Azam kimezidi kujiimarisha kwa maana ya leo tumeweza kupata saini ya mchezaji Donald Ngoma ambaye amesaini mkataba mwingine wa mwaka mmoja zaidi baada ya kutumikia mkataba wake wa awali ambao umekwisha.

Ngoma amefurahia kusaini mkataba huo na klabu yake na amezidi kuomba ushirikiano kwa wachezaji wenzie kama alivyosaini mwanzo na kucheza katika matumaini makubwa. Vilevile ameomba mashabiki wa Azam kuzidi kuhamasisha na kuwa karibu na timu yao.

Ameomba uongozi kuhakikisha unasimamia kila jambo liende sawa na matumaini yao kama wachezaji, watafanya vizuri," alisema Iddi.

Azam inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na pointi 56 ilizozipata baada ya kucheza mechi 27.

ADVERTISEMENT