In Summary

Baada ya Simba kuambulia kipigo cha mabao 5-0 dhidi ya Al Ahly hatua ya makundi ya ligi ya Mabingwa Afrika, hiki ndicho alichokisema Shiza Kichuya  kwa Wanamsimbazi ili washinde siku ya Jumanne.

Dar es Salaam. Wakati mashabiki wa soka nchini wakiisubiria kwa hamu kubwa pambano la Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Simba na wageni wao, Al Ahly ya Misri, winga wa zamani wa Msimbazi, Shiza Kichuya ameamua kujilipua na kuipenyezea Simba siri za Waarabu ili waimalize Jumanne kwenye Uwanja wa Taifa.
Kichuya ambaye aliondoka na Simba kwenda kuifuata Al Ahly waliowafumua Vijana wa Msimbazi mabao 5-0 kabla ya kuishia mikononi mwa Pharco FC iliyomsajili na kumtoa kwa mkopo ENPPI, alisema ujanja wa Waarabu ni dakika 45 tu, kama Simba itaibana itashinda gemu.
Winga huyo alivaana na Al Ahly Ijumaa iliyopita kwenye mechi ya Ligi Kuu ya Misri na timu yake ya mkopo, ENPPI kulala mabao 2-1 na alisema wapinzani hao wa Simba wanacheza zaidi dakika 45 za kwanza na kama Wekundu wa Msimbazi wakakomaa ndani ya muda huo itakuwa freshi.
Alisema kipindi cha pili kwa Al Ahly ni cha kujilinda, hivyo anaitaka Simba ijipange kwa muda uliosalia ili kupata ushindi kwani anaamini nafasi hiyo wanayo na kiu yake ni kuona chama lake la zamani likipata ushindi nyumbani kwa m,ara ya pili baada ya kuibutua JS Saoura kwa 3-0.
"Simba ina nafasi kubwa ya kuwafunga Al Ahly, tofauti na namna wanavyofikiri, kikubwa ni kupambana nao kipindi cha kwanza ambacho wao ndio wazuri zaidi na wanakuwa na malengo yao maalumu na ndicho walichokifanya walivyowafunga mabao 5-0.
"Jambo lingine wana dhamira ya pamoja kwa kila mchezaji kuwajibika asilimia mia kwa nafasi yake, umakini mwingi ndani ya dakika hizo, jambo pekee ninaloliona Simba wawabane na kuwachosha kipindi cha kwanza huku wakiwa wanatafuta mpenyo wa kufunga mabao.
"Simba kipindi cha pili watatakiwa kutumia nguvu sana, kwani Al Ahly watakuwa wamepunguza kasi na plani yao ya kwanza itakuwa imefeli, inawezekana wajipange vizuri na wachezaji waongezewe morali," alisema.
Kuhusu maisha yake Misri, Kichuya alisema hali ya hewa ya baridi inamfanya apambane ili aendane nayo hasa isimfanye ashindwe kucheza.
"Huku kunawaka jua lakini baridi lake usiombe, akili yangu haijakubali kushindwa nimeamua kukubaliana na hali halisi ya hewa hivyo hainisumbui," alisema.

ADVERTISEMENT