In Summary

Mshambuliaji Allan Wanga kwa sasa anakipiga katika klabu ya Kakamega Homeboyz, ambako pia ameajiriwa kama Mkurugenzi wa michezo. Straika huyu timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars, aliyepata kuichezea Sofapaka, Tusker FC, AFC Leopards, na Azam ya Tanzania, atakuwa nyota wa saba kusajiliwa na Gor Mahia, endapo dili hilo litafanikiwa.

Nairobi, Kenya. Unaweza usiamini, lakini habari ndio kama ulivyosikia. Katika harakati za kuimarisha safu yake ya ushambuliaji, Kocha wa mabigwa watetezi wa Ligi Kuu Kenya (KPL), Gor Mahia Muingereza Dylan Kerr anamtaka mshambuliaji mkongwe Allan Wanga.

Baada ya kuwaruhusu mastraika wake, Mnyarwanda Meddie Kagere na Muivory Coast, Ephreim Guikan waondoke, Kocha huyo aliyeipatia Gor Mahia ubingwa wa 17 wa KPL, ameamua kumjumuisha ‘mkongwe’ Wanga katika kikosi chake kinachojiandaa na ligi kuu msimu wa 2018/19 na mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika.

Wanga, mwenye umri wa miaka 32, amewahi kucheza katika klabu ya AFC Leopards, Tusker FC, Sofapaka na Azam FC ya Tanzania, kwa sasa anakipiga Kakamega Homeboyz pia ni mchezaji wa timu ya taifa, Harambee Stars.

Alipoulizwa sababu za kumtaka Wanga ambaye anaonekana kushuka makali, Kerr alisema: Wanga ni Mkenya. Pili ukiangalia safu yangu ya sasa, kuna kitu ambacho tunakikosa, Guikan alishindwa kutupatia kitu hicho na mwisho wa siku akaondoka. Unapomtazama Wanga, bila kujiuliza mara mbili, unakiona unachokitafuta kwa straika. Ana nguvu, kasi na akili ya kufunga.”

Hata hivyo, Kerr anakiri kuwa, anaona ugumu wa kuipata saini ya straika huyo, licha ya kumwambia Mwenyekiti wa Kogalo, Ambrose Rachier amfanikishie hilo, kwa sababu licha ya kuwa mchezaji, Wanga pia ni mkurugenzi wa michezo katika kaunti ya Kakamega, hivyo ni ngumu kumshawishi Gavana wa kaunti hiyo kumuachia.

Gor Mahia, tayari imeshafanya usajili kadhaa, katika dirisha hili la usajili ambapo mbali na kuzinasa saini za Shafiq Batambuze na Kenneth Muguna kutoka SIngida United (Tanzania) na KF Tirana (Albania), wamewasajili mastraika Nicholas Kipkirui (Zoo Kericho), Erisa Ssekisambu (Vipers SC, Uganda) na beki Pascal Ogweno (Kariobangi Sharks).

Kogalo, kwa sasa wanajiandaa kuwakabili Nyasa Big Bullets ya Malawi, utakaopigwa kati ya Novemba 27 na 28, ugani Moi Kasarani, katika mchezo wa mtoano wa ligi ya mabingwa Afrika, kabla ya kuwafuata Jijini Blantyre, wiki moja baadae.

ADVERTISEMENT