In Summary

Ronaldinho Mshindi wa kombe la Dunia 2002, Tuzo ya Ballon d’Or (2005) na tuzo ya mchezaji bora wa dunia (2004), aliwahi kucheza kwa mafanikio katika klabu ya Barcelona, Paris Saint Germain na AC Milan.

Nairobi, Kenya. Nyota wa zamani wa Barcelona na timu ya taifa ya Brazil, Ronaldinho Gaucho atakuwa nchini Kenya wikendi hii, kwa ajili ya kushuhudia programu maalum ya soka.

Kwa mujibu wa taarifa zilizoifikia Mwanaspoti ni kwamba, Ronaldinho ambaye anatajwa kama mmoja wa wanasoka bora kabisa kuwahi kutokea katika uso wa ulimwengu wa soka, atakuwa mgeni rasmi katika mechi ya fainali ya Super 8 Champions League.

Taarifa zinasema kuwa Ronaldinho, ambaye ni mshindi wa tuzo ya Ballon d’Or mwaka 2005 na ile ya mchezaji bora wa dunia (2004), atawasili Kenya Ijumaa ya Novemba 9, ambapo  Jumamosi anatarajiwa kuwepo uwanjani Camp Toyoyo Jijini Nairobi, kushuhudia fainali hiyo.

Kwa mujibu wa Meneja wa Matukio wa kampuni ya michezo ya Extreme Sports, Athanas Obang’o, ambao ndio wanaomleta, ni kwamba ziara ya Ronaldinho itasaidia sana kuhamasisha jamii kuona umuhimu wa michezo.

Mbali na Jiji la Nairobi, Obang’o alisema kuwa, Ronaldinho pia anatarajiwa kuhudhuria hafla maalum ya kimichezo, itakayofanyika Moi Stadium, mjini Kisumu.

ADVERTISEMENT