In Summary

Everton FC na Gor Mahia, zitakutana Novemba 6, mwaka huu kwa mara ya pili. Mara ya kwanza kukutana  Julai 13, Mwaka 2017, nchini Tanzania, ambapo Everton FC, ilishinda 2-1, wafungaji wakiwa ni Wayne Rooney na Kieran Dowell huku bao pekee la Kogalo likiwekwa wavuni na Jacques Tuyisenge.

Nairobi, Kenya. Everton FC ilifanya makusudi kabisa. Wala haikuwa bahati mbaya kuisambaratisha Brighton and Hove Albion namna ile. Ilikuwa ni salamu kwa wageni wao kutoka Kenya, klabu ya Gor Mahia. Walimaanisha kuwakaribisha Goodison Park kwa staili ya aina yake.

Wakifahamu fika kuwa Mabingwa wa ligi kuu nchini Kenya (KPL) na kombe la Sportpesa, klabu ya Gor Mahia, wapo uwanjani Goodison Park, tena katika siti za mbele kwa ajili ya kuwasoma kimbinu kabla ya mechi ya kirafiki ambayo pia ni ya kuwania kombe la SportPesa Super Cup, Everton FC waliamua kufanya walichokifanya.

Mabao matatu kutoka kwa Richarlison aliyetupia mawili, katika dakika ya 26 na 77, na Seamus Coleman (dk 50), yalitosha kabisa kuwabashiria vijana wa Dylan Kerr kile kinachowasubiri, watakapokutana uwanjani hapo, siku ya Jumanne, Novemba 6, kuanzia saa nne usiku.

Everton walitangulia katika dakika ya 26, baada ya kazi nzuri ya Gylfi Sigurdsson, aliyekuwa mwiba mkali kwa Brighton na huenda akawa tishio kwa Kogalo, akimlisha pasi Richarlison pasi murua. Coleman alipiga la pili katika dakika ya 50 kabla Richarlison hajamalizia kunako dakika ya 77. Bao pekee la kufuta machozi kwa upande wa Brighton, liliwekwa kimiani na Lewis Dunk.

Mechi ya Jumanne usiku, ambao unatazamiwa kuwa mkali, ni mechi ya kihistoria kwani ni ya kwanza kukutanisha timu kutoka Afrika Mashariki na klabu kubwa ya ligi kuu ya England katika Ardhi ya Waingereza.

ADVERTISEMENT