In Summary
  • Kocha huyo Mtaliano amesaini mkataba wa miaka mitatu ya kufanya kazi Stamford Bridge na ametua hapo kuchukua mikoba ya Antonio Conte, aliyefutwa kazi Ijumaa iliyopita.

CHELSEA imemtangaza Maurizio Sarri kuwa kocha wao mpya kuanzia sasa.

Kocha huyo Mtaliano amesaini mkataba wa miaka mitatu ya kufanya kazi Stamford Bridge na ametua hapo kuchukua mikoba ya Antonio Conte, aliyefutwa kazi Ijumaa iliyopita.

Chelsea imeshaanza mazoezi ya kujiandaa na msimu mpya hivyo kocha Sarri atakwenda kuungana nao na kuendeleza makali.

“Nasubiri kuanza kazi na kukutana na wachezaji Jumatatu kabla ya kwenda Australia, ambako nitapata nafasi ya kukielewa zaidi kikosi tutakapocheza mechi,” alisema Sarri.

“Natumaini tutacheza soka la kuburudisha mashabikio wetu na tutashindania mataji pia mwisho wa msimu kitu ambacho ndicho kinachotakiwa kwenye klabu hii.”

Mkurugenzi Marina Granovskaia ameweka imani yake kwa Sarri na anaamini atawapatia Chelsea huduma bora kabisa na kuleta falsafa nzuri kwenye kikosi hicho.

Chelsea pia imekamilisha usajili wa kiungo wa Napoli, Jorginho kwa ada inayotajwa kuwa ni zaidi ya Pauni 50 milioni. Chelsea imemnasa staa huyo baada ya Manchester City kujitoa katika dakika za mwisho kwenye mbio hizo na hivyo Jorginho amesaini mkataba wa miaka mitano ya kutumikia klabu hiyo ya Stamford Bridge. Huo utakuwa usajili wa kwanza kwenye kikosi cha Chelsea katika dirisha hili la majira ya kiangazi huku ikiwa na kazi ya kuzuia nyota wake wengine wasiondoke.

ADVERTISEMENT