KATIKA sehemu ya kwanza ya mahojiano haya baina ya Mwanaspoti na mwanasoka Mtanzania Yusuf Soka, anayeishi Sweden, alizungumzia jinsi alivyoshangazwa na uvumi kwamba alifungwa jela miaka 30 na mwingine wa kwamba alinyongwa, akisema hajui hata ulianzaje. Katika sehemu ya pili leo tena huyu hapa Soka. Twende naye pamoja:

MAISHA YA SWEDEN

“Niliposafiri kutoka Tanzania kuja Sweden nilifikia kwenye Klabu ya AFC Eskilstuna ambayo inashiriki Ligi Daraja la Nne. Lakini, kutokana na sheria za hapa Sweden wao walikuwa wakinitunza na kunitafutia timu ya juu nikacheze,” anasema Soka.

Anasema, kwa sababu klabu hiyo ni kama ya ridhaa walikuwa wanampa matunzo na mahitaji muhimu kama chakula, malazi na mambo mengine lakini walikuwa hawamlipi mshahara.

AGOMEA KUUZWA ESPERANCE

“Sasa baada ya kukaa pale ile klabu ilinitafutia timu ya kucheza kitu ambacho, kina manufaa kwao wanapomuuza mchezaji. Timu ambayo walinitafutia ilikuwa Esperance de Tunis ya Tunisia,” anasema Soka.

“Kurudi Afrika kusema kweli mimi sikukubaliana na jambo lile kwa sababu hamu na malengo yangu ilikuwa ni kucheza Ulaya, sasa naambiwa narudi tena Afrika, nikajiongeza.”

Anasema klabu hiyo imekuwa ikiwauza wachezaji wenye malengo ya kucheza soka la kulipwa katika klabu mbalimbali zikiwamo za Afrika.

“Baada ya kukataa, ile timu ilibidi waache kunihudumia. Hapo sasa ikabidi niondoke na kuingia mtaani na nilikwenda kukutana na ndugu zangu ambao wanaishi Sweden.”

BALAA VIZA ILIPOISHA

Soka anasema alipokwenda Sweden alitakiwa kukaa kwa muda kulingana na viza yake ya kuingia nchini humo, lakini yeye alipitiliza.

“Nikaonekana nimezamia, lakini si kweli. Kama nilivyosema awali sikutaka kurudi Tanzania kabla sijatimiza ndoto zangu. Sasa nilipokuwa naishi kwa ndugu zangu walinielekeza jambo la kufanya kama nataka kuendelea kubaki Sweden kwa kufuata taratibu,” anasema Soka.

“Walinielekeza niende Wizara ya Uhamiaji nikaeleze kila kitu hasa ndoto zangu, nikafanya hivyo. Uhamiaji walinielewa na kwa sababu umri wangu ulikuwa mdogo, uhamiaji walinitafutia mahali pa kuishi na hii ilikuwa ni familia ya watu wa Sweden ambao jukumu lao ni kunilea na uangalizi zaidi,” anasema Soka.

MAISHA NA FAMILIA YA WASWEDEN

Anasema, kwa sababu hakuwa na matatizo, aliishi kwa nidhamu katika familia ile iliyomlea kama mtoto wao na alijisikia kama yuko nyumbani.

“Katika kipindi chote hicho nacheza mpira nilikuwa katika familia yangu ya Kisweden kabla ya kuanza kujitegemea mwenyewe. Walinilea vizuri, walinipenda na hata sasa, licha ya kuwa najitegemea mwenyewe wao wamekuwa kama wazazi wangu hapa Sweden,” anasema Soka.

Anasema, akiwa nyumbani kwa Wasweden hao, aliendelea na shughuli zake za mpira kama kawaida lakini pia walimwendeleza kimasomo.

“Nilipelekwa shule kwa ajili ya kusoma lugha ya Sweden na pia masomo ya sekondari ambako nilisoma kidato cha tano na sita. Mbali na masomo hayo pia wana programu ya kusomea kitu cha ziada, mimi nilichagua ualimu.”

ANACHEZA HUKU ANAFUNDISHA

Anasema, alipomaliza masomo hayo kwa sababu tayari alikuwa na kitu cha ziada ikabidi aanze kufundisha.

“Kwa sababu muda wa mazoezi mara nyingi huwa ni jioni, asubuhi huwa mara chache, katika siku tatu za wiki kuanzia Jumatano, Alhamisi na Ijumaa nimekuwa nikifanya kazi ya kufundisha asubuhi. Nafundisha watoto wadogo wa chekechea,” anasema Soka.

Anasema, kazi hiyo imekuwa ikimwongezea kipato lakini pia anafanya hivyo kwa sababu hataki kushinda nyumbani bila kazi.

ACHAGULIWA TIMU YA TAIFA SWEDEN

“Kwa sababu nilikuwa na kipaji kikubwa cha mpira, waliniita timu ya taifa ya vijana ya Sweden chini ya miaka 20. Kwa sababu nilikuwa mdogo walijua ni Msweden,” anasema Soka.

Anasema, pamoja na kukaa huko kwa kipindi kirefu hakuweza kubadilisha uraia wake, anaishi kwa kibali maalumu cha kuishi muda wote (permanent) lakini yeye ni raia wa Tanzania.

SABABU YA KUTOBADILI URAIA

“Sikuweza kubadili uraia kwa sababu nilitambua kuwa mimi ni Mtanzania bado ninatakiwa kutoa mchango kwa timu yangu ya Taifa kwa sababu bado inanihitaji. Nilikuwa na uwezo wa kubadili uraia na kuwa Msweden, lakini sikufanya hivyo,” anasema Soka.

Anasema, anaamini siku moja atapata nafasi ya kuichezea timu ya taifa ya Tanzania hata kama si leo. “Nitarudi nyumbani Tanzania na kuichezea timu yangu ya Taifa Stars pale walimu watakaponiona na kuridhika na kiwango changu.”

TIMU ALIZOPITA

“Baada ya kukataa dili la Esperance. Nilipata timu ya daraja la nne ya Bergs IK kisha nikajiunga na Ope IF mwaka 2012 lakini 2013 nikaumia goti, hivyo nikawa nje kwa muda kiasi na kuendelea na programu za daktari wangu,” anasema Soka na kuweka wazi mbali na mazoezi ya daktari alikuwa anafanya programu ya GYM kwa ajili ya kujenga misuli.

Anasema, alipopona aliumia tena sehemu hiyo ikabidi afanyiwe upasuaji akakaa miaka miwili nje uwanja na alipopona akarudi tena kwenye soka na kujiunga na IFK Östersund 2015.

“Nilicheza nusu msimu tu nikaonwa na timu ya Daraja la Kwanza ya IFK Gothenburg lakini kwa sababu timu ilikuwa kubwa na mimi natoka kwenye maumivu ushindani ulikuwa mkubwa hivyo sikupata nafasi ya kucheza ikabidi wanipeleke kwa mkopo kwenye timu ya Ligi Daraja la Pili ya IFk Östersund ili niweze kupata nafasi zaidi ya kucheza,” anaeleza Soka.

“Lakini, kwa sababu ilikuwa imepita miaka mingi sijarudi Tanzania na kama hivyo ndugu walikuwa hofu, niliamua kurudi nyumbani kwa ajili ya kusalimia na kupata baraka zaidi ya wazazi.”

ALIPORUDI SWEDEN KWA MARA NYINGINE

“Tanzania nilikaa kwa kipindi kirefu kama miezi saba kwa sababu ya kutuliza akili na mambo mengine. Nilirudi kucheza Ligi Daraja la Pili timu ambayo nachezea sasa ya IFk Östersund,” anasema Soka.

Anasema, amekubali kucheza timu hiyo kwa ajili kujiweka fiti zaidi kwa sababu alikuwa nje ya uwanja kwa kipindi kirefu alipokuwa Tanzania.

KASI YA KUFUNGA MABAO

Soka anasema, kasi yake ya kufunga bao ipo kama kawaida kwani pamoja na kutokuwa fiti aliporudi Sweden kwenye Klabu ya IFk Östersund alicheza.

“Pia, nilipata tatizo nikaumia bega. Lakini kwa sababu timu ilikuwa na watu wengi majeruhi na mimi tatizo langu lilikuwa bega tu ikabidi wawe wananitumia hivyo hivyo nikawa naingia na kucheza dakika tano, 10 hadi 30,”anasema Soka.

“Licha ya kucheza dakika hizo chache, niliwafungia sana mabao na nikawa nashika nafasi ya pili kwa wapachikaji mabao kwenye Klabu. Nilicheza mechi 19, nikafunga mabao manane na mfungaji wa ligi nzima alipachika mabao 29,”anasema Soka.

Anasema, anamshukuru Mungu kwa sababu kama ni mguu wa kufunga bao anao: “Naweza kusema nimeumbwa kwa sababu ya kufunga. Kazi yangu ni kufunga tu sitaki mambo mengi uwanjani.”

ALIVYOJIPANGA KWA KAZI

“Kwa kipindi chote cha maandalizi (pre seasons) nimekuwa nafanya vizuri na wiki ijayo (hii) tunaanza msimu mpya, nategemea kufanya vizuri zaidi. Sasa wanaosema nimepotea kwenye soka waanze kunifuatilia ili wanione kwa vitendo maana mimi sipendi kuongea,” anasema Soka.

Anasema, anapoangalia mitandao ya Tanzania kuna kauli moja inayozungumzwa kwa wingi: “Ule usemi mmoja ambao Watanzania wanapenda kuzungumza (anautafuta na kuutaja kwa shida) kuwa mambo ni mengi na muda ni mchache.”

“Nasema hivi, maneno huwa hatayatendi nipe muda dada, matendo yangu yatazungumza, wewe subiri tu,” anasisitiza.

Usikose sehemu ya tatu ya masimulizi haya kesho Jumamosi uone kilichomtokea alipofuatwa na vigogo wa Simba wakiwa na maburungutu ya pesa.

ADVERTISEMENT