RAIS wa Shirikisho la Kimataifa la Soka, (Fifa), Gianni Infantino ameendelea kufanya mabadiliko kama si maboresho mbalimbali ya katika soka duniani.

Kuna mengi ameyafanya ikiwemo mabadiliko ya tarehe za Kombe la Dunia ambalo mwaka 2022 litachezwa mapema zaidi tofauti na linavyofanyika katikati ya mwaka.

Fifa pia imeongeza timu za Kombe la Dunia kutoka 32 na sasa zitakuwa 48 na tayari utaratibu wake umetajwa na Afrika ikiwa na uwankilishi wa timu tisa.

Mtawanyiko kwa kila nchi kufuzu uko wazi.

Mwanzoni wakati utaratibu unabadilishwa, ilielezwa kuwa timu 48 zitaanza kucheza 2026, lakini sasa mambo yamebadilika tena.

Kilichopo sasa, Infantino ametangaza mabadiliko mengine kwa timu zitakazokata tiketi ya kwenda Qatar fainali zijazo za Kombe la Dunia 2022.

Infantino juzi alitangaza mabadiliko mengine. Alibadilisha uamuzi wa kuongeza timu zitakazoshiriki Kombe la Dunia kutoka 32 hadi 48 kwa fainali za 2026 na sasa timu 48 zitaanza kuwania nafasi ya fainali zijazo za 2022.

Pamoja na hayo, uamuzi huo wa mabadiliko utawalazimisha Qatar kushirikiana na nchi jirani zake katika kuandaa fainali za mwaka 2022.

Mataifa ya Marekani, Canada na Mexico ndiyo yalishinda uwenyeji wa fainali za 2026, lakini Infantino sasa anataka kufanya hivyo kwa fainali za 2022 mapema zaidi.

“Inawezekana, kwanini ishindikane?” alisema.

Infantino ambaye hana msamiati wa kushindwa katika akili yake, alisema Fifa inataka kuangalia kama inawezekana au kama itakuwa bora. Alisema kama Fifa, itazungumza na marafiki wao wa Qatar kuona jinsi gani wanavyoweza kupata nafasi ya kushiriki kikamilifu Fainali za Qatar.

Infantino alisema pia kama Fifa watazungumza na marafiki zao wa ukanda huo ni matumani yake kuwa watafanikiwa.

Alinukuliwa akisema: “Kama itashindikana, lakini tutakuwa tumejaribu. Tunatakiwa kujaribu kwa sababu katika kujaribu unapata kitu bora.”

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa makao makuu mapya ya Shirikisho la Soka Asia jijini Kuala Lumpur, Infantino pia alisema kuhusu mpango huo kwamba wanataka kufanya yawe mashindano makubwa hasa.

“Tunataka kila taifa duniani liguswe na kila fainali, lishiriki tofauti na zamani kwamba ni baadhi ya timu tu zina.”

Tumeshuhudia mabadiliko hayo ambayo kwa upande mwingine ameiambukiza Afrika.

Afrika kwa mfano, Fainali za Cameroon mwakani zitashirikisha nchi 24 badala ya 16 za awali. Mabadiliko mengine ni kwamba fainali hizo zitachezwa katikati ya mwaka tifauti na miaka mingine, kwamba Afcon huchezwa kati ya Januari mwisho na Februari mwanzoni.

Mpango wa sasa ni kukomaa kuhakikisha Tanzania inacheza fainali za Afrika, aliouanzisha Rais John Magufuli.

Katia chachu kuhakikisha Tanzania inamaliza kiu ya miaka 38 na kwenda Cameroon mwakani kwenye fainali hizo. Timu hiyo itaanza kwa kuweka kambi huko Bondeni.

Sasa, mpango wa Fifa ndio huo, nako mkakati uwekwe, tunakata kiu ya miaka 38, tunatengeneza mpango mkakati wa kwenda Qatar 2022.

Hilo linawezekana. Tanzania huwa ina bahati ya kuanzishwa kwa mifumo mipya ya mashindano.

Wakati Fainali za Afrika zinatoka timu nane hadi 16, Tanzania ikawemo kule Lagos 1980.

Wakati CAF inaanzisha mashindano ya Fainali za Afrika kwa wachezaji wa Ligi za Ndani, CHAN 2009, Tanzania iliingia fainali hizo kule Ivory Coast ikiilaza Sudan 2-1.

Sasa, hili la kubadilika kwa mashindano ya mwakani kutoka 16 hadi 24, basi lazima na tayari moto umewashwa na usizimwe, ukazimwe Younde, Cameroon mwakani.

Wakati tukihakikisha timu inakwenda Cameroon, vilevile tuhakikishe mipango ya 2022 inaanza mapema. Tusema lazima twende Qatar 2022.

Tulishindwa kwa timu 16 hata 24 za Afcon tukose? Kombe la Dunia kutoka nafasi tano za Afrika, hata hizo nne zilizoongezeka kutoka Afrika tukose?

Mikakati ikifanyika inawezekana kwa TFF na wadau lakini Serikali ni mdau mkubwa wa kusimamia michezo.

Tunaamini Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harisson Mwakyembe atakuwa mshika bendera wa mstari wa mbele akituongoza mbio tukiweka nia, lengo, dhamira na mkakati kwamba lazima twenda Qatar 2022. Hakuna kinachoshindikana.

ADVERTISEMENT