MADRID, HISPANIA: KIUNGO fundi wa mpira, Christian Eriksen, jina lake kwa sasa linatajwa huko Hispania, akidaiwa kuwindwa na vigogo wa La Liga, Barcelona na Real Madrid.

Kiungo huyo anayekipiga kwenye kikosi cha Tottenham Hotspur amedaiwa kuzivutia timu zote mbili na huenda mwishoni mwa msimu huu vigogo hao wa La Liga wakaingia vitani kuchuana kuwania huduma yake huku wakitarajia kupata upinzani kutoka kwa timu nyingine kama vile Paris Saint-Germain, Manchester United na Chelsea.

Hata hivyo, Eriksen hatakuwa mchezaji wa kwanza kuwaingiza kwenye vita kali vigogo Real Madrid na Barcelona katika kuiwania huduma yake baada ya huko nyuma kutokea masupastaa kibao waliowafanya mabosi wa timu hizo watunishiane misuli katika kuwania saini zao.

Alfredo di Stefano

Nafasi: Straika

Washindi: Real Madrid

Ada: Pauni 184,000

Straika matata kabisa, Di Stefano aligombaniwa na timu hizo mbili, lakini aliamua kumwaga wino kuichezea Real Madrid na kuwaweka kando Barcelona mwaka 1953, licha ya kwamba klabu yake ya Millonarios ilikubaliana na Barcelona kwanza. Di Stefano alikuwa mchezaji muhimu katika kuifanya Real Madrid kutamba kwa miaka kibao kwenye soka la Ulaya, kuisaidia timu hiyo kubeba ubingwa kwa misimu mitano mfululizo.

Di Stefano bado anashika nafasi ya tatu kwa mabao kwenye kikosi hicho cha Madrid, akifunga mara 308, akizidiwa na Cristiano Ronaldo (451) na Raul (323).

Johann Cruyff

Nafasi: Straika

Washindi: Barcelona

Ada: Pauni 922,000

Straika mwingine matata kabisa wa kiwango cha dunia, ambaye wakati anaondoka Ajax alizua vita kali baina ya Real Madrid na Barcelona na mwisho wababe wa Nou Camp walishinda vita ya kunasa saini yake. Staa huyo wa Kidachi kwa sasa ameshafariki, lakini alikwenda kuifanya Barcelona kuwa timu bora zaidi duniani kuanzia wakati huo hadi sasa bado inapita kwenye misingi yake. Ada yake, milioni 6 za Kidachi iliweka rekodi kwa wakati huo, lakini pesa hiyo ilikwenda kuonekana kuwa ndogo kwa alichokifanya Barcelona. Alitua Nou Camp mwaka 1973 akawapa ubingwa wa La Liga, waliokuwa wakiusubiri kwa miaka 13, huku akiongoza mauaji ya kuwachapa Real Madrid 5-0.

David Beckham

Nafasi: Kiungo wa kulia

Washindi: Real Madrid

Ada: Pauni 29 milioni

Barcelona ndio waliokuwa wa kwanza kuonyesha dhamira ya kuinasa saini ya staa wa Manchester United, David Beckham na hiyo ilikuwa mwaka 2003. Kinachoelezwa ni kwamba Man United walikubaliana na Barcelona kabla ya mchezaji huyo kuamua kwenda kujiunga na Real Madrid. Jambo hilo linadaiwa lilimkera sana rais wa Barcelona kipindi hicho, Joan Laporta kwa sababu tayari alikuwa na uhakika anakwenda kuinasa huduma ya Mwingereza huyo kabla ya wapinzani wake Madrid kumzidi ujanja. Beckham alianza kwa mkwara kwenye La Liga, akifunga kwenye dakika ya tatu tu katika mechi yake ya kwanza, kisha akafunga tena mara nne katika mechi 15 zilizofuatia. Baada ya misimu minne Bernabeu, Beckham aliondoka na kutimkia zake LA Galaxy.

Ronaldinho

Nafasi: Kiungo mshambuliaji

Washindi: Barcelona

Ada: Pauni 25 milioni

Barcelona iliumizwa sana na namna walivyokosa saini ya David Beckham kwa kuzidiwa ujanja na Real Madrid, hivyo na wao wakaamua kulipa kisasi kwa kumsajili Ronaldinho kutoka PSG, kwa sababu naye alikuwa kwenye mipango ya Real Madrid ikitaka kumsajili. Bao hilo la Barca kwa Real Madrid kuhusu Ronaldinho lilikuwa la maana kubwa sana kwani baada ya Mbrazili huyo kutua Nou Camp tu basi alibadili kabisa mambo huko kwenye La Liga na Blaugrana wakaanza kutamba kwenye ligi na michuano ya Ulaya pia. Ronaldinho alikuwa moto kwenye kikosi cha Barca akifunga mabao 94 na asisti 69 katika mechi 207 alizotumikia timu hiyo. Aliondoka kwenye timu hiyo kwenda AC Milan baada ya misimu mitano kabla kuja kukiri anajutia uamuzi huo kwa sababu umemkosesha nafasi ya kufaidi kucheza na Lionel Messi kwa muda mrefu.

Dani Alves

Nafasi: Beki wa kulia

Washindi: Barcelona

Ada: Pauni 23 milioni

Mbrazili, Dani Alves aliachana na Barcelona kwenye msimu wa 2016/17 na kwenda kujiunga na Juventus bure kabisa kabla ya kuamua kuondoka hapo kwenda kujiunga na mabingwa wa Ufaransa, Paris Saint-Germain. Lakini akiwa kwenye kikosi cha Barca, Alves alikuwa mchezaji muhimu kwelikweli akicheza kwenye beki ya kulia, kiungo na hata wakati mwingine alitumika kama mshambuliaji.

Bila shaka Real Madrid ilikuwa kwenye majuto makubwa kutokana na kuikosa huduma ya mchezaji huyo kwa sababu wao walikuwa wa kwanza kumtaka kabla ya kuja kuzidiwa ujanja na mahasimu wao hao wa El Clasico. Alves aliisaidia Barcelona kushinda mataji sita ya La Liga, matatu ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na mara mara nne kwenye Copa del Rey.

David Villa

Nafasi: Straika

Washindi: Barcelona

Ada: Pauni 33 milioni

Barcelona ilimsajili David Villa kutoka Valencia katika msimu wa 2010/11, ikiwa ni mwaka mmoja baadaye baada ya vita kali ya Barca na Real Madrid walikuwa wakipambana kumshawishi mshambuliaji huyo kwenda kujiunga na timu zao.

Kulikuwa na ripoti Villa alikubaliana na Real Madrid kwenda kujiunga na timu yao kwa ada ya Pauni 38 milioni kabla ya Barcelona kupindua meza. Maisha yake huko Nou Camp yaliandamwa na majeruhi, hasa katika msimu wa 2012/13, ambao ulimfanya fowadi huyo asiwe na mwanzo wake mtamu sana katika kikosi cha wababe hao wa Nou Camp. Aliondoka kwenda Atletico Madrid, ambako aliisaidia kushinda ubingwa wa La Liga kabla ya kutimkia zake Marekani kwenda kujiunga na New York City FC.

Neymar

Nafasi: Kiungo wa kushoto

Washindi: Barcelona

Ada: Pauni 71 milioni

Dili la usajili wa Neymar lilianza mwaka 2011 katika michuano ya Klabu Bingwa Dunia, ambapo Neymar alikuwa kwenye kikosi cha Santos kilichomenyana na Barcelona. Uhamisho wa Neymar haujawahi kukosa utata, ambapo kabla ya hapo, Real Madrid ilikuwa kiguu na njia kwenda Brazil kufukuzia huduma ya mchezaji huyo kabla ya kuzidiwa ujanja na Barcelona ambayo ilitoa ahadi nyingi kwa wakala wa Neymar, ambaye ni baba yake.

Baada ya purukushani za muda mrefu, hatimaye Barca ilishinda vita ya kuinasa huduma ya staa huyo mwaka 2013. Neymar aliisaidia Barca kubeba mataji kibao ikiwamo matatu makubwa kwa msimu mmoja huku akifunga mabao 105 katika misimu yake minne aliyokuwa kwenye timu hiyo, huku mabao 68 akifunga kwenye La Liga.

Kwa sasa amejiunga na Paris Saint-Germain kwa ada iliyovunja rekodi ya dunia ya Pauni 200 milioni.

Luis Suarez

Nafasi: Straika

Washindi: Barcelona

Ada: Pauni 65 milioni

Straika, Luis Suarez aliwahi kukaririwa akisema kulikuwa na uwezekano mkubwa wa kwenda kujiunga na Real Madrid wakati anaondoka Liverpool, lakini shida ni kwamba Barcelona nayo ilikuwa kwenye mbio za kuinasa saini yake, hivyo ilikuwa ngumu kwa upande kuacha fursa ya kwenda kucheza timu moja ya Lionel Messi mpite.

Kutokana na hilo, Suarez alikwenda kujiunga na Barcelona baada ya fainali za Kombe la Dunia 2014, ambako alikuwa na majanga yake kutokana na kumng’ata beki wa Italia, Giorgio Chiellini na kukumbana na adhabu ya kufungiwa na Fifa. Tangu atue kwenye kikosi cha Barcelona, Suarez amekuwa moto kwelikweli na kufunga mabao na kubeba mataji kibao akiwa na kikosi hicho huku akicheza sambamba na Messi na kuna kipindi alikuwa akiunda kombinesheni hatari sana kwenye fowadi sambamba na Neymar iliyokuwa ikifahamika kwa jina la MSN, kwa maana ya Messi, Suarez, Neymar.

ADVERTISEMENT