FAINALI za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) kwa Vijana U-17 zitafanyika Aprili 14-28 hapa Tanzania. Hii ni mara ya kwanza kwa Tanzania kuhodhi fainali za aina hii kwa soka, huku tumaini lake likiwa kwa Serengeti Boys.

Kitendo cha timu hiyo kubeba mataji ya vijana kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) kisha Ukanda wa Kusini Mwa Afrika (Cosafa) kumewafanya mashabiki kuwa na imani kubwa na timu hiyo.

Hata hivyo, tukiwa tumesaliwa na miezi minne tu kabla ya fainali hizo kumeibuka sintofahamu baada ya TFF kutaka kuleta kocha mwingine kutoka nje ili kuisongesha timu hiyo katika fainali hizo.

Mwanaspoti linakuletea baadhi ya mambo yanayoweza kuigharimu timu hiyo, iwapo itakuwa mikononi mwa kocha mwingine na kuachana na Oscar Mirambo anayeinoa sasa.

MIRAMBO KIUNGO

Ikumbukwe viajana wa Serengeti wamelelewa kwenye mikono ya Mirambo, anayafahamu mahitaji yao kwani amewakuza kisoka na kuwalea kwa asilimia kubwa.

Mirambo ni kocha ambaye alizunguka mikoani kuwatafuta vijana katika mashindano ya Umitashumta na Umisseta ili kupata wachezaji, ndio maana leo wanafanya vizuri chini yake kwani anazifahamu tabia za kila mchezaji baada ya kukaa nao kambini kwa takribani siku 100 akiwachuja wenye viwango bora zaidi ya wengine.

Kama Mirambo akitimka kwenye benchi la ufundi kunaweza kuleta shida kidogo kwa vile ndiye aliyekuwa kiungo cha mafanikio ya Serengeti Boys katika michuano yote iliyoshiriki na kutumainiwa kuifanyia makubwa nchi katika fainali hizo za Afcon.

Labda aletewe mtu ambaye atakubali kufanya kazi na benchi ambalo limepambana na timu hii muda wote .

MFUMO UTATA

Alipoondoka Kim Poulsen wengi walishika vichwa na kuhisi soka la vijana litapotea kwa sababu timu hii tangu 2011 mpaka 2018, licha ya kuondoka 2014 na kurejea nchini 2016 iliijengea mwelekeo mzuri.

Kim aliwaibua kina Frank Domayo na Mudathir Yahya na vijana wengi ambao aliwalea. Alijenga mfumo wa Scandinavia kuendesha soka.

Hata hivyo, aliporejea aliacha mfumo wake na mbinu kwa Mirambo ambaye ameweza kuvaa viatu vya Poulsen baada ya kukubali kufanya naye kazi kwa ukaribu.

Kim alivyoondoka bado tumeiona Serengeti ikiendelea kucheza soka safi la utulivu, lakini anapokuja kocha mwingine na kutaka kuanzisha mifumo wake katika kikosi hiki vyovyote vile ataipotezea ladha timu kwani vijana ni ngumu kubadilika haraka kimfumo huku kukiwa na muda mchache.

MORALI HUENDA IKASHUKA

Japo sio rahisi kuamini, lakini wachezaji hawa kabla ya michuano ya Cosafa walipitia changamoto nyingi. Hata hivyo, benchi la ufundi chini ya Mirambo liliwajenga kisaikolojia na kufakiwa. Kazi iliyofanywa na benchi hilo iliwajenga na kuwapa morali kujituma na mwishowe walirudishwa kwa ndege nchini.

Hivyo, wanajua kabisa wamepitia mapito magumu na walimu wao, ikifikia hatua ya kuwabadilishia, wanaweza kuharibikiwa kisaikolojia kwa sababu wataona wazazi wao wanafanyiwa jambo lisilo sahihi. TFF inabidi wafikirie kabla ya uamuzi.

MUDA SIO RAFIKI

Imebakiza miezi minne tu kabla mashindano hayo kuanza Aprili mwaka huu, wakati huo huo Serengeti ikiwa imealikwa kwenye mashindano Uturuki ikiwa ni kama sehemu ya maandalizi kwa ajili ya maandalizi ya fainali hizo.

Kubadilisha kocha kwa muda fupi uliobaki ni kuwavuruga vijana hawa, ni vizuri mabadiliko kama hayo yangefanywa mapema na utaduni wa kubadilisha makocha dakika za mwisho TFF wangeuacha kwa klabu ambazo ni desturi yao kubadili kadiri wanavyoona inafaa maana wachezaji wao wanajitambua na umri wao ni mkubwa kuliko hawa vijana wadogo kabisa.

Mabadiliko hayazuiliki lakini kama kocha anayeletwa kuongeza nguvu kwenye benchi la ufundi akiwa kama mshauri ambaye atawaongozea ushauri kina Mirambo kuhakikisha Serengeti wanafanya vizuri.

Tofauti na hivyo ni kuwavunja nguvu tu makocha ambao wametoka mbali na timu.

ADVERTISEMENT