In Summary
  • Mshambuliaji wa Juventus na timu ya taifa ya Ureno, Cristiano Ronaldo ameweka historia kuwa mtu mwenye wafuasi wengi zaidi katika mtandao wa Instagram amefanikiwa kufikisha idadi ya wafuasi milioni 144.4

NEW YORK, MAREKANI. KUBAKA? Hapana. Mashabiki wa soka na wengineo, wameiweka kando kashfa ya ubakaji inayomkabili staa wa Juventus na timu ya taifa ya Ureno, Cristiano Ronaldo na kuamua kumpandisha chati kwa kumfanya awe mtu mwenye wafuasi wengi zaidi katika mtandao huo.

Ronaldo ameweka historia kuwa mtu mwenye wafuasi wengi zaidi katika mtandao huo na kumpiku staa wa POP wa Marekani, Selena Gomez ambaye kwa muda mrefu alikuwa anashikilia nafasi hiyo katika mtandao huo unaotamba zaidi kwa sasa.

Ronaldo, staa wa zamani wa Sporting Lisbon, Manchester United na Real Madrid amefanikiwa kufikisha idadi ya wafuasi milioni 144.4 mtandaoni humo na kumpita, Selena ambaye ana wafuasi 144.3 milioni.

Katika siku za karibuni Ronaldo mara nyingi amekuwa akiposti picha za familia yake yenye watoto wanne pamoja na mpenzi wake mpya, Georgina Rodriguez ambaye amemzalia mtoto mmoja kati ya watoto hao wanne.

Umaarufu wake umekuwa ukipanda kila kukicha mitandaoni licha ya kufikisha umri wa miaka 33 katika soka na amefanikiwa kumpita Selena ambaye ni mpenzi wa zamani wa staa mwingine wa muziki, Justin Bierber, aliyekuwa amekaa kileleni tangu mwaka 2016.

Rekodi hii ya karibuni inampa faraja kubwa Ronaldo ambaye amekuwa akipitia kipindi kigumu kwa kushtumiwa kumbaka Mrembo, Kathryn Mayorga katika jumba la kifahari la kukodi karibu na Palms Casino Resort jijini Las Vegas mwaka 2009.

Polisi wa Marekani wamefungua shauri kuhusu madai hayo dhidi ya Ronaldo ambaye amekanusha kufanya baya lolote na mwanamke huyo huku yeye na Wanasheria wake wakiamini kwamba mwishowe staa huyo hatakutwa na hatia.

Hata hivyo, Ronaldo ambaye kwa sasa anatamba na Juventus baada ya kuanza kwa kusuasua amekiri kwamba tuhuma hizo zimekuwa ziimuathiri kwa kiasi kikubwa nje ya uwanja linapokuja suala zima la familia yake.

Posti yake ya kwanza tangu ashike nafasi ya kwanza katika Instagram ilimuonyesha akiwa katika hoteli yake ya kifahari aliyojenga nchini kwao Ureno, Pestana CR7 eneo la Funchal, akiwa ghorofani na kuwatazama mashabiki wake kwa chini.

Mara baada ya kuposti picha hiyo kulikuwa na mashabiki 4.5 milioni walioweka alama ya kuipenda na baadae alipiga picha akiwa Gym na mashabiki zaidi ya 5.6 milioni wakionyesha kuipenda picha hiyo. Ronaldo na mwanae, Ronaldo Jr wamekuwa wakionekana wakiwa mazoezini pamoja kwa muda mrefu.

Achilia mbali umaarufu wake, lakini inawezekana kwamba sababu nyingine kubwa iliyosababisha Ronaldo ampite Selena inatokana na kitendo cha staa huyo kuamua kupumzika masuala ya mitandaoni kwa kile alichoeleza kutafuta matibabu ya afya.

Posti yake ya mwisho alituma Septemba 23 mwaka huu huku ikipata likes 8.2 milioni na alitoa ujumbe wa kupumzika mitandaoni akisema “nachukua mapumziko ya mitandaoni tena.

“Nashukuru sana jinsi ambavyo mitandao ya Jamii inavyotupa. Nashukuru kuweza kurudi nyumba kidogo na kuishi maisha yangu ya sasa kwa muda ambao nimepewa. Nahitaji huruma yenu na kutiwa moyo kidogo. ”

Wakati Selena akiaga hivyo, Ronaldo majuzi alikuwa akiposti picha akiwa na familia yake katika sikukuu ya Halloween huku wote wakiwa wamevaa vinyago vya kutisha ikiwa ni ishara ya kumbukumbu ya sherehe hizo maarufu duniani hasa barani Ulaya.

Katika soka Ronaldo anafukuziwa kwa mbali na staa wa PSG na timu ya taifa ya Brazil, Neymar ambaye mpaka sasa ana wafuasi 104. Hata hivyo Kwa dunia Neymar anashika nafasi ya tisa akiwa amempita kwa nafasi moja, Justin Bierber ambaye anashika nafasi ya 10 akiwa na wafuasi 102 milioni.

Mpinzani wa karibu wa Ronaldo katika soka, Lionel Messi ambaye ni staa wa kimataifa wa Barcelona na Argentina ameachwa mbali na Ronaldo huku akiwa na wafuasi 100 milioni. Messi hayupo katika kumi bora za Instagram.

Achilia mbali Ronaldo na Selena, staa wa mwingine wa Pop, Ariana Grande anashika nafasi ya tatu akiwa na wafuasi 132 milioni huku staa mwingine wa Marekani, Kim Kardashian akishika nafasi ya nne akiwa na wafuasi 120 milioni.

ADVERTISEMENT