MACHI 2, mshambuliaji wa Ruvu Shooting, Fully Maganga alifunga mabao matatu (hat trick) katika mchezo mmoja wa Ligi Kuu dhidi ya Mwadui FC uliochezwa katika Uwanja wa Mabatini mkoani Pwani.

Kikanuni alipaswa kupewa zawadi ya mpira uliotumika kuchezewa mechi hiyo na badala yake alikuja kupewa zawadi hiyo juzi, Jumatano Aprili 3, katika mchezo wa ugenini ambao timu yake ilicheza na Mtibwa Sugar.

Ni zaidi ya muda wa mwezi mmoja umepita tangu Maganga apate mpira huo ambao alipaswa kupewa siku ileile ya mchezo ambapo alifunga mabao hayo il iwe kumbukumbu kwake.

Mwaka 2013, Amissi Tambwe alipokuwa akiichezea Simba, alifunga idadi kama hiyo ya mabao kwenye mchezo mmoja wa Ligi Kuu ambao timu yake iliibuka na ushindi wa mabao 6-0 dhidi ya Mgambo Shooting lakini alinyimwa mpira na Mwamuzi, Jacob Adongo aliyechezesha mchezo huo.

Baada ya wengi kupaza sauti kwa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) pamoja na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Tambwe alipatiwa mpira lakini ilikuwa baada ya muda kidogo kupita.

Matukio kama haya yamekuwa yakitokea mara kwa mara kwenye ligi yetu lakini hatuoni dalili za kuwepo kwa mwisho wake je tunakwama wapi?

Tuna uhaba wa mipira ya kuchezea mechi za ligi kiasi hicho hadi tunakubali ligi yetu ipate aibu nyepesi kama hiyo ya kushindwa kuwapa mipira ya zawadi kwa wakati sahihi wachezaji wanaofunga nabao matatu kwenye mchezo mmoja?

Kwa ligi ambayo timu zake zimetinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho mara tatu ndani ya kipindi cha miaka minne, ligi inayokusanya idadi kubwa ya wachezaji wa kigeni, inayolipa mishahara mizuri kwa wachezaji pamoja na mvuto kwa mashabiki, ni aibu kubwa kushuhudia ikishindwa kutoa mipira kwa wachezaji wanaofunga hat trick.

Ni jambo linalotia doa soka la Tanzania lililozalisha kipaji cha nyota anayetamba Ulaya kwa sasa, Mbwana Samatta au mwenzake wa Difaa el Jadida, Saimon Msuva.

Aibu hii ya Fully Maganga inapaswa kuwa ya mwisho na haitakiwi kutokea tena nchini kwani inaepukika kulingana na thamani ya ligi yetu.

Ni jambo la kushangaza kwa nchi inayoandaa Fainali za Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 (AFCON U17), kuwa na ligi ambayo inashindwa kutoa mpira kwa mchezaji anayefunga mabao matatu kwenye mchezo mmoja.

Ni jambo la kushangaza na halipaswi kutolewa utetezi.

ADVERTISEMENT