JUMAMOSI ya Novemba 15, 1884, Kansela wa Ujerumani, Otto von Bismarck, aliitisha mkutano mkubwa kwa ajili ya kuligawa Bara la Afrika.

Mkutano huo uliofahamika kama Berlin Conference, ulifanyika kwenye makazi yake huko Wilhelmstrasse, Berlin.

Mkutano huo ulilenga katika kuwaepusha wababe wa Magharibi kutumbukia vitani wakati wakigombania mali za Afrika.

Mataifa 14 yalihudhuria, wakiwemo Ujerumani wenyewe, Uingereza, Marekani (wakiwakilishwa na Henry Morton Stanley), Himaya ya Ottoman (Dola ya Mtukufu Sultan wa Azam TV), Denmark, Ufaransa, Muungano wa Austria na Hungary, Urusi, Ureno, Hispania, Muungano wa Sweden na Norway, Ubelgiji, Italia na Uholanzi.

Mkutano huu ndio uliosababisha ukoloni barani Afrika, kwani uliazimia katika kuligawa bara hili miongoni mwa wababe waliohudhuria, kwa faida yao.

Baada ya mkutano huo, mataifa hayo yakatuma wawakilishi wao kuja Afrika kuchukua maeneo na mali.

Ujerumani ikamtuma kijana wa miaka 28, aliyeitwa Karl Peters, akiwa na vijana wenzake watatu; Dk. Karl Juhlke, Pfeil na August Otto.

Vijana hawa wakafunga safari hadi Afrika na kutia nanga Zanzibar na baadaye kuanza safari ya bara hadi walipofika Usagara ambako walikutana na Chief Mangungo katika Ikulu yake ya Msovero. Usagara kwa sasa ndio Kilosa.

Karl Peters akatumia ujanja, hila na ulaghai kuingia mkataba na kiongozi huyo wa kiafrika uliosababisha Ujerumani kuchukua eneo lake lote pamoja na watu wake.

Mkataba huo uliandikwa kijerumani na Chief Mangungo akamtumia mkalimani wake kutoka hapo hapo Msovero (Ramazan) ambaye na yeye wala hakuijua lugha hiyo.

Mkataba huo ulisomeka kama ifuatavyo.

“Mangungo amekubali kutoa himaya yake yote pamoja na watu wake na hadhi yake kwa Dk. Karl Peters, kama mwakilishi wa Umoja wa Ukoloni wa Kijerumani, kwa ajili ya matumizi ya moja kwa moja ya koloni la Kijerumani.

Dk. Karl Peters, kwa niaba ya jina la Umoja wa Ukoloni wa Ujermani anatangaza dhamira yake ya kuitwaa himaya yote ya Sultan Mangungo na haki zote kwa ajili ya Koloni la Ujerumani inayohusisha kila kona na amali za Mwenyi Sagara.”

Baada ya mkataba huu, Karl Peters akalichukua eneo lote lililokuwa chini ya Mangungo na kuliweka chini ya kampuni yake ya Deutsch-Ostafrika (German East Africa) ambayo ilikuwa ikimiliki eneo lote ambalo leo hii ni Tanzania Bara na Rwanda na Burundi.

Wakati machifu wengine, kama Mkwawa, walipigana na Ujerumani kukataa maeneo yao kuchukuliwa, Mangungo alilitoa eneo lake kirahisi kabisa.

Hayo yalitokea mwaka 1884. Hayo yalitokea karne ya 19. Hayo yalitokea kwa sababu Mangungo hakusoma, hivyo asingeweza kufua dafu mbele ya msomi, Daktari wa Falsafa, Karl Peters.

Lakini leo hii, zaidi ya miaka 130, katika karne ya 21, inashangaza kuona mikataba ya aina hiyo ikiendelea kusainiwa.

MKATABA WA KOMBE LA SHIRIKISHO LA AZAM SPORTS

Desemba 14 mwaka huu, Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao aliongea na vyombo vya habari kuhusu sintofahamu ya zawadi kwa washindi wa Kombe la Shirikisho la Azam Sports, 2018 (Mtibwa Sugar) na hata 2017 (Simba SC).

Kidao alisema sababu za timu hizo kutopata zawadi zao ni kutokuwepo kwa kipengele cha zawadi kwenye mkataba wa mashindano hayo.

Hapo ndipo mimi napata shida. Inawezekanaje mkataba wa mashindano usielezee mshindi atapataje zawadi zake? Siku ya fainali, washindi walipewa mfano wa hundi ya zawadi ya fedha taslimu iliyokuwa na jina la mdhamini, Azam Media Limited. Nini kilibadilika baadaye?

Mkataba wa kwanza wa mashindano haya ulisainiwa mwaka 2015 na ukamalizika Mei 2018.

Unaweza ukawasamehe hawa viongozi wa sasa, wakati huo walikuwa hawajaingia madarakani.

Lakini mwaka huu umesainiwa mkataba mwingine wa miaka mitano na waliosaini ni hawa viongozi waliopo, kwa nini bado haki ni ile Ile? Au waliosaini hawakujua lugha iliyotumika, kama ilivyomtokea Chief Mangungo wa Msovero? Kwenu Azam Media, kauli ya Kidao inalenga katika kujivua lawama na kudondoshea mzigo kwenu mikataba yenu ni ya kitapeli.

Halafu ile picha iliyopigwa pale Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha Nahodha wa Mtibwa Sugar, Shaaban Nditi akipokea mfano wa hundi ya Sh50 milioni ilikuwa ina maanisha nini kama michuano hiyo haina zawadi ya fedha? Kila mwenye akili alitafakari hili na kupima majibu mepesi ya Kidao mbele ya wanahabari ambao waliridhika na kwenda kuandika habari bila ya kutafakari.

Ni jukumu lenu kujisafisha, aidha kwa kutoka hadharani na kusema ukweli (kama upo) au kutoa fedha za zawadi ili kuokoa jina lenu lisiharibike.

Azam, kama jina bendera la makampu za Bakhresa, linaheshimika sana Tanzania, msilichafue kirahisi namna hii.

Yawezekana kweli mkataba hausemi zawadi atatoa nani, lakini nyinyi ndio wadhamini na linalochafuka ni jina lenu.

Ulimwengu wa soka umetawaliwa na watu wenye kumbukumbu za muda mfupi ambao ushindi wa jana kwao siyo muhimu zaidi ya ushindi wa leo.

Hayupo atakayepoteza muda kuangalia ni kiasi gani Azam Media au Azam kwa jumla imewekeza kwenye mpira wa nchi hii. Watakachoangalia hilo chafu moja na kuwahukumu kijumla.

ADVERTISEMENT