In Summary

Kenya, Tanzania, Algeria na Senegal, ziko katika kundi C, kwenye fainali ya Mataifa ya Afrika, itakayoanza kutimua vumbi kuanzia Juni 21 hadi Julai 19, huko Cairo, Misri.

ZIKIWA zimesalia siku chache makala ya 32 ya Kombe la Mataifa ya Afrika, AFCON 2019, zitimue vumbi nchini Misri, Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), imetoa viwango vya ubora kwa mwaka 2019.
Kwa mujibu wa viwango hivyo vilivyotolewa leo Ijumaa, Kenya inayojiandaa na fainali za AFCON, imepanda kwa hatua tatu, kutoka nafasi ya 108 hadi nafasi ya 105 duniani baada ya kuongeza pointi tano kwenye kapu lake na kufikisha pointi 1207. Awali ilikuwa na pointi 1202.
Viwango hivyo vinaonesha kuwa, wapinzani wa Kenya kwenye kundi C ya AFCON Algeria na Senegal nao wamepanda huku Tanzania wao wakiendelea kung'ang'ania nafasi ya 131 na pointi zao 1105.
Algeria wamepanda kwa hatua mbili, kutoka nafasi ya 70 hadi 68, baada ya kufikisha pointi 1348 kutoka 1346 walizokuwa nazo awali huku Senegal wao wakipiga hatua moja juu, kutoka nafasi ya 23 hadi 22, licha ya kuendelea kuwa na pointi zilezile (1515).  
Viwango hivyo vimetoka wakati ambapo timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars, inajiandaa kucheza mechi ya kirafiki na DR Congo, inayoshika nafasi ya 49 duniani, ikiwa ni siku moja baada ya Tanzania kuchapwa 1-0 katika mchezo wa kirafiki na Misri.
Juni 23, Harambee Stars, ambayo imefuzu fainali hizo kwa mara ya kwanza, baada ya miaka 15, itaumana na Algeria, kisha ikipige na Tanzania (Juni 27), kabla ya kukutana uso kwa uso na Senegal (Julai mosi)


Belgium wababe, Ureno kicheko
Timu ya taifa ya Belgium imeendelea kukalia usukani katika ubora wa soka, wakikaa juu ya Mabingwa wa Kombe la Dunia (2018) Ufaransa ambayo imesalia nafasi ya pili, kufuatia ushindi walioupata dhidi ya Kazakhstan na Scotland.
Mabingwa wa msimu wa kwanza wa Kombe la UEFA Nations League,  taifa la Ureno wamepanda hatua mbili juu, kutoka nafasi ya saba hadi tano, wakifanikiwa kuingia tano bora huku Uholanzi waliopigwa kwenye fainali na Ureno, wakipiga hatua mbili kutoka nafasi ya 16 hadi 14.
Mabingwa wa zamani wa Dunia, Hispania, Ujerumani na Italia nao wamepanda hadi nafasi ya Saba, 11 na 14 mtawalia. Aidha, mataifa mengine yaliyopanda ni Austria (26, hatua 8), Northern Ireland (28, hatua 5), Czech Republic (41, hatua 7), Hungary (42, hatua 9), Armenia (97, hatua 9) na Malaysia (159, hatua 9).

ADVERTISEMENT