In Summary

Kocha, Emery alikuwa kwenye wakati mgumu sana kwenye mechi zilizochezwa hapo kati kutokana na kukosa huduma za wachezaji wake muhimu, lakini sasa mambo yamekaa sawa na West Ham United ndio watakaoanza kukutana na Arsenal iliyokamilika kwenye idara za

LONDON, ENGLAND. LAZIMA kieleweka na kitaeleweka tu. Kocha, Unai Emery amepata mzuka huko Arsenal baada ya mastaa wake kibao waliokuwa wagonjwa kupona na sasa wapinzani imekula kwao. Hapo kati, Arsenal ilikuwa na udhaifu mkubwa kutokana na mastaa wake kadhaa muhimu kuwa majeruhi, lakini kwa taarifa tu kuna vifaa sita matata vimerejea mazoezi na kukifanya kikosi cha wababe hao wa Emirates sasa kuwa kamilikamili katika mchakamchaka wao wa kuhakikisha kwamba suala la kumaliza msimu ndani ya Top Four haliwi tena mjadala mzito.

Kocha, Emery alikuwa kwenye wakati mgumu sana kwenye mechi zilizochezwa hapo kati kutokana na kukosa huduma za wachezaji wake muhimu, lakini sasa mambo yamekaa sawa na West Ham United ndio watakaoanza kukutana na Arsenal iliyokamilika kwenye idara zake.

Wachezaji sita muhimu kwenye kikosi cha kwanza cha Arsenal walikuwa wakikosekana kwenye kikosi hicho kutokana na kuwa wagonjwa, lakini sasa mambo yatakuwa tofauti kuanzia na kwenye mechi zijazo. Mesut Ozil na Hector Bellerin ni miongoni mwa mastaa hao sita waliokuwa hawapo kwenye kikosi cha Arsenal kwa kuwa majeruhi, lakini sasa watarudi uwanjani na sura zao zitaonekana kwenye mechi ya wikiendi hii dhidi ya West Ham. Ozil amekosekana uwanjani tangu alipotolewa uwanjani wakati wa mampumziko kwenye mechi dhidi ya Brighton kwenye Boxing Day kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya goti.

Lakini, Mjerumani huyo sasa yupo fiti na amerudi mazoezini huku akiwa na kazi moja ya kumshawishi kocha Emery ili akipige wakati wababe hao watakapomenyana na West Ham kesho Jumamosi. Bellerin mara ya mwisho kuonekana uwanjani ilikuwa Desemba 6 kwenye mechi ya kipigo dhini ya Southampton. Kurejea kwa mchezaji huyo kunatazamiwa kwenda kupunguza presha kwenye safu ya mabeki ya timu hiyo ambayo siku za karibuni imekuwa ikiruhusu mabao kuliko maelezo.

Mastaa wengine wanne wanaoungana na wawili hao ambao wanarejea kwa kishindo kwenye chama la Arsenal ni Laurent Koscielny, Shkodran Mustafi, Nacho Monreal na Dinos Mavropanos, ambao wanakuja kumfanya Emery sasa kutibu yale matatizo yaliyokuwa yakisumbua kwenye kikosi chake, kuwa na beki mchekea. Koscielny aliumia wakati akipasha misuli moto kabla ya mechi ya Blackpool, wakati Mustafi alikosa mechi hiyo kwa kuwa na tatizo la misuli. Monreal naye alikosa mechi kibao mwezi uliopita kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya misuli.

Beki Mgiriki, Mavropanos alikosa msimu wote kutokana na kufanyiwa upasuaji, lakini sasa amerudi mazoezini na sasa Arsenal imekuwa matata kwelikweli. Beki huyo mwenye umri wa miaka 21 amecheza mechi tatu tu kwenye kikosi cha Arsenal tangu alipojiunga na timu hiyo akitokea Olympiakos mwaka mmoja uliopita. Lakini, yote kwa yote ni kurejea kwa mastaa makini kabisa kwenye kikosi hicho cha Emery na kuifanya Arsenal kuwa kamili tayari kwa mapambano.

ADVERTISEMENT