In Summary
  • Mwanzo  wa msimu huu, Simba walifanya usajili wa maana kwa wachezaji wengi lakini kiungo Mzambia, Cletus Chama amekua mchezaji mwenye mafanikio makubwa ndani ya timu ya Simba tangu alipotua msimbazi.

MWANZO wa msimu huu, Simba walifanya usajili wa maana kwa wachezaji wa ndani na nje ya nchi huku wakilenga kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa.

Katika usajili huo kuna baadhi ya wachezaji wameshindwa kutamba, lakini wengine wako moto na wamegeuka kuwa vipenzi vya mashabiki wa klabu hiyo.

Nyota wapya waliosajiliwa msimu huu na wameshindwa kutamba ni Marcel Kaheza, Mohammed Rashid, Deogratius Munishi ‘Dida’, na huenda wameshindwa kutamba baada ya kukosa nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza.

Wengine waliobaki wote wanatamba katika ligi kutokana kazi zao uwanjani kulingana na nafasi ambazo wanacheza kama Adam Salamba, Meddie Kagere, Cletus Chama na Hassan Dilunga ambao, wamekuwa watamu kwelikweli.

Lakini, mashabiki wa Simba hawaelezi lolote kuhusu kiungo Mzambia, Chama ambaye mbali na kufunga mabao, pia anatengeneza nafasi za kufunga kila anapokuwa dimbani na kuibeba Simba.

Makala haya yanakuletea mabao matano matata na ambayo unaweza kuyashindanisha popote duniani ambayo Chama amefunga tangu alipotua Simba msimu huu.

CHAMA vs STAND UNITED

Oktoba 21 Simba walicheza mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Stand United ‘Wapiga Debe’ na mabingwa hao waliendeleza ubabe wao kwa kuibuka na ushindi katika mechi hiyo.

Dakika 30 pasi ya Shiza Kichuya katikati ya uwanja inamkuta Chama, ambaye anampiga chenga nahodha wa Stand United, Jacob Masawe ndani ya boksi akiwa pembeni mwa uwanja kisha anapiga shuti la kuzungusha linalomshinda kipa Mohammed Makaka na kutinga nyavuni.

Lilikuwa bao lake la kwanza la msimu tangu alipotua Simba ambao mechi hiyo walishinda mabao 3-0 mawili mengine yakifungwa na Emmanuel Okwi na Meddie Kagere.

CHAMA vs ALLIANCE

Oktoba 24 Simba walicheza dhidi ya Alliance ambao walitoka kufungwa kipigo cha maana mabao 3-0 dhidi ya Yanga siku tatu zilizopita yaani Oktoba 20.

Chama alifunga bao lake la pili katika mechi hiyo ndani ya dakika 87, ambapo aliwapiga chenga mabeki wawili kisha akaingia katikati ya walinzi watano wa Alliance na kupiga kombora la chinichini.

Katika mechi hiyo Simba walipata ushindi wa mabao 5-1 ambayo yalifungwa na Asante Kwasi, Adam Salamba, Chama na Okwi ambaye alifunga mawili.

CHAMA vs MBABANE SWALLOWS

Simba imepania kutikisa msimu huu kuanzia Ligi Kuu Bara hadi kimataifa na ndio sababu ya kumnasa Chama na hakika haijakosea kabisa.

Novemba 28 Simba walianza safari katika mashindano ya kimataifa kwa kukipiga na Mbabane katika Ligi ya Mabingwa Afrika pale Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katika mechi hiyo Simba walishinda mabao 4-1 yaliyofungwa na Chama, Kagere na nahodha John Bocco ambaye alifunga mabao mawili.

Katika mabao hayo, Chama alifunga la nne katika dakika ya 90 akitumia vizuri kazi kubwa iliyofanywa na Hassan Dilunga, aliyewapiga chenga walinzi wawili wa Mbabane na kumtengea Chama, ambaye aliwapunguza mabeki wawili wa Mbabane ndani ya boksi na kupiga shuti huku akidondoka.

MBABANE SWALLOWS

Katika mechi ya marudiano dhidi ya Mbabane ambayo ilichezwa nchini Eswatini, Desemba 4 Simba waliibuka na ushindi wa maana wa mabao 4-0 wakisonga mbele katika hatua inayofaata huku wakiwa na idadi kubwa ya mabao ambayo yalikuwa ni 8-1 katika mechi zote mbili.

Katika mechi hiyo dakika 27 Chama alifunga mabao mawili na la kwanza alipiga baada ya shuti kali la Okwi kupanguliwa na kipa Mbabane kisha kumkuta Chama, ambaye alimpiga chenga beki akapiga shuti la chinichini ambalo lilikwenda moja kwa moja kambani na kuiandikia Simba bao la kuongoza.

LA PILI

Katika mechi hiyo hiyo, kabla ya kipindi cha kwanza kumalizika Chama zilimchukua dakika tano tu kuindikia Simba bao la pili ambalo lilikuwa la kideoni kuliko lile la kwanza ambalo alifunga kwenye mechi hiyo ya ugenini.

Bap hilo lilikuwa hivi, Erasto Nyoni alipiga pasi ndefu ya chinichini kwa Chama, ambaye baada ya kuipokea alimpiga kanzu kiungo wa Mbabane kisha akampa pasi Okwi, ambaye alitoa pasi ya maana ile kampa kampa tena ambayo Chama alikutana nayo ndani ya boksi na kumchagua kwa kumfunga kipa wa Mbabane na aliweza kufanya hivyo bila shida na kuindikia Simba bao la pili.

ADVERTISEMENT