In Summary

  •  Walipokutana mara ya kwanza, Zarika na Phiri walitoa burudani ya uhakika kwa mashabiki wa ndondi nchini kwa kuonyesha kiwango kikubwa cha pambano ambacho kilitawaliwa na damu, jasho mwanzo mwisho. 

BONDIA Fatuma ‘Iron Fist’ Zarika kaapa kumpa kipigo cha uhakika mpinzani wake Mzambia Catherine Phiri, atakapotetea mkanda wake wa WBC Super bantamweight kwa mara  ya tatu mfululizo wiki ijayo.

Zarika na Phiri watakutana kwa mara ya pili kwenye pambano hilo litakaloandaliwa katika ukumbi wa KICC, Nairobi ambalo Mzambia huyo atakuwa akisaka kulipiza kisasi.

Hata hivyo Zarika kamwahidi Phiri kipigo kibaya zaidi kuliko kile alichompokeza  safari ya kwanza walipokutana Disemba 2017 ugani Carnivore,  akiwa anatetea mkanda huo kwa mara ya kwanza toka alipompokonya Mjamaica Alicia Ashley Octoba 2016.

“Namahidi Phiri kitu kimoja kwamba baada ya pambano, mwili wake wote utakuwa na maumivu makali. Hataweza kula nyama kwa wiki nzima, hilo namhakikishia” Zarika  kamwonya.

Hayo ndiyo yaliyokuwa maneno yake Zarika kabla ya kuabiri ndege Jumanne kuelekea Uingereza ambapo atajenga kambi yake ya mazoezi kwa wiki moja.

Walipokutana mara ya kwanza, Zarika na Phiri walitoa burudani ya uhakika kwa mashabiki wa ndondi nchini kwa kuonyesha kiwango kikubwa cha pambano ambacho kilitawaliwa na damu, jasho mwanzo mwisho.

Baada ya pambano hilo la raundi 10, Zarika aliishia kutawazwa bingwa na kuhifadhi mkanda wake kwa wingi wa alama kutoka kwa majaji watatu akizoa pointi 97-92, 98-91 na 99-92.

Ni matokeo ambayo kambi ya Phiri ilipinga ikisisitiza bondia wao ndiye aliyeshinda na kuomba re-match ambayo Zarika yupo tayari.

“Hainishtui kwa sababu yeye sio boksa bora kati ya wale niliokutana nao hasa nilipokuwa majuu. Catherine anaamini hakupoteza pambano na kwamba safari hii ataondoka na huu mkanda. Kile anachopaswa kuelewa ni kwamba huu mkanda haung’oki kwangu, hilo namhakikishia” Zarika akatema cheche zaidi.

Baada ya kumchapa Phiri Disemba 2017, Zarika aliutetea tena mkanda huo dhidi ta Yamileth Mercado mzalendo wa Mexico Septemba 2018 na kumbwaga kwa tofauti za pointi kutoka kwa majaji akizoa alama 94-96, 97-93 na 99-91

Zarika kapambana mara 42 katika taaluma yake akiwa anajivunia rekodi ya 30-12-2  huku Phiri akiwa na rekodi ya 16-3-1 KOs 10

ADVERTISEMENT