In Summary

Mabingwa watetezi wa michuano hiyo ambao kama watashinda mechi hiyo ya fainali, watachukua kombe hilo na kulimiliki moja kwa moja kwa sababu itakuwa ni mara ya tatu mfululizo.

Unguja: Mzambia Obrey Chirwa wa Azam FC amefikisha mabao manne sasa kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi na kuwa kinara kwenye safu ya ufungaji bora ya mashindano hayo na timu yake ikitinga hatua ya fainali baada ya kuifunga KMKM mabao 3-0.
Azam imetinga fainali ambayo itachezwa keshokutwa Jumapili  Uwanja wa Gombani, Kisiwani Pemba na sasa inamsubiri mshindi kati ya Simba na Malindi mechi itakayochezwa usiku wa leo Ijumaa Uwanja wa Amaan.
Mabao ya Azam yalifungwa na Aggrey Morris dakika ya tisa huku la pili likifungwa na kiungo, Salum Aboubakary 'Sure Boy' dakika ya 62, akipokea krosi ya Nicolas Wadada raia wa Uganda.
Mabingwa hao watetezi wa michuano hiyo ambao kama watashinda mechi hiyo ya fainali, watachukua kombe hilo na kulimiliki moja kwa moja kwa sababu itakuwa ni mara ya tatu mfululizo.
Morris alifunga bao hilo akiunganisha mpira wa kona uliopigwa na Mghana Enock Atta na kuunganisha kwa kichwa.
Azam walishindwa kutumia nafasi mbili za wazi baada ya Sure Boy kupiga shuti kali lililotoka nje ya mwamba goli dakika ya
41.
Sure Boy alikosa bao lingine dakika ya 43, baada ya kupokea mpira wa kona uliopigwa na Joseph Mahundi ambapo shuti lake lilitoka nje kwa mara nyingine.
Azam maarufu kwa jina la Wanalambalamba ilipata bao la tatu
lililofungwa na Chirwa akipiga shuti la mpira wa krosi na
kutinga nyavuni moja kwa moja ikiwa ni dakika ya 81.
Mwamuzi wa mchezo huo, Mfaume Ali alitoa kadi ya njano kwa mchezaji wa KMKM, Richard Jaka baada ya kumchezea madhambi Atta.
Makocha wote walifanya mabadiliko ambapo kwa Mholanzi Hans Pluijm aliwaingiza, Mahundi, Mzimbabwe Bruce Kangwa, Lusajo Mwaikenda na Robert Dismas wakichukua nafasi za Mzimbabwe Donald Ngoma, Hassan Mwasapili, Morris na Stephan Kingue.
Kocha wa KMKM, Ame Msimu naye aliwatoa, Iliassa Mwinyi, Musa Mbaruk na Brown Costa nafasi zao zilichukuliwa na Juma Mohamed, Salum Bajaka na Faki Sharif.

ADVERTISEMENT