In Summary

Timu hizi zimekuwa ndiyo kila kitu kwenye soka la Tanzania. Simba na Yanga ndiyo timu zenye mastaa wengi zaidi nchini. Ni timu zinazofanya usajili wa fedha nyingi zaidi nchini ukichana na Azam inayomilikiwa na mfanyabiashara Said Salim Bakhresa, hii ilianzishwa miaka saba iliyopita.

SIMBA na Yanga ndiyo wababe wa soka la Tanzania. Ndiyo timu zenye historia kubwa kwenye soka la Tanzania tangu kuanzishwa kwake zaidi ya miongo saba iliyopita.

Timu hizi zimekuwa ndiyo kila kitu kwenye soka la Tanzania. Simba na Yanga ndiyo timu zenye mastaa wengi zaidi nchini. Ni timu zinazofanya usajili wa fedha nyingi zaidi nchini ukichana na Azam inayomilikiwa na mfanyabiashara Said Salim Bakhresa, hii ilianzishwa miaka saba iliyopita.

Simba na Yanga ndizo timu zilizotwaa mataji mengi zaidi nchini. Zimetwaa mataji ya ligi, Kagame na mengineyo kwa kadiri zilivyojisikia. Kwa kifupi ndizo timu zilizo na historia ya maana nchini.

Hivi umewahi kujiuliza endapo timu hizi zisingekuwepo hali ya soka la Tanzania ingekuwaje? Umewahi kujiuliza bila Simba na Yanga maisha ya soka la Tanzania yangekuwaje. Watanzania wangekuwa wanashabikia timu gani?

Fahamu mambo ambayo yangetokea ama yasingetokea endapo klabu hizi kongwe nchini zisingekuwepo;

Pan African isingeanzishwa

Mwaka 1975 ulitokea mgogoro mkubwa kwenye klabu ya Yanga. Mgogoro huu ulileta mpasuko mkubwa ambapo baadhi ya viongozi wa klabu hiyo waliamua kuondoka na kwenda kuanzisha timu ya Pan African. Wachezaji walituhumiwa kuihujumu timu na ndipo wachache wao walipoonyeshewa mlango wa kuondoka lakini wakaondoka wengi zaidi kuonyesha kutounga mkono kutimuliwa wenzao, ndipo ilipoundwa Pan African. Mwaka 1976 Pan ilifanikiwa kutinga Ligi Kuu (Ligi Daraja la Kwanza kwa wakati huo) na kutikisa kwenye soka la Tanzania hadi ilipofanikiwa kutwaa taji la ligi mwaka 1982 ikiipokonya Yanga iliyokuwa bingwa mtetezi. Kwa hali ya kawaida kama Yanga isingekuwepo hakuna namna Pan African ingeanzishwa kwani timu hiyo chimbuko lake ni mgogoro ndani ya Yanga.

Tukuyu Stars isingeshuka daraja

Timu ya Tukuyu Stars kutoka jijini Mbeya ilipanda na kucheza ligi daraja la kwanza (ligi kuu) kwa mara ya kwanza mwaka 1986 ambapo ilitwaa taji la ligi hiyo kwa mwaka wake huo wa kwanza tu kwenye ligi. Tukuyu ilifanikiwa kuweka historia ya kuwa timu ya kwanza kucheza ligi kuu kwa mara ya kwanza na kutwaa taji. Hata hivyo baada ya mafanikio hayo Simba na Yanga ziligawana mastaa wa timu hiyo. Zilisajili mastaa wote walioipa ubingwa Tukuyu, jambo lililopelekea timu hiyo kushuka daraja miaka mitatu baadaye. Endapo timu hizi kongwe nchini zisingekuwepo Tukuyu isingeshuka daraja na yawezekana ingekuwa inashiriki ligi hiyo hadi hivi sasa.

Prisons ingeweza kutwaa taji

Hakuna timu ya jeshi ambayo imewahi kutwaa ubingwa wa ligi kuu. Timu hizo zimekuwa timu washiriki wa ligi hiyo bila mafanikio yoyote ya maana kwa miongo kadhaa sasa. Prisons ndiyo timu ya soka inayomilikiwa na jeshi ambayo ina mafanikio makubwa zaidi nchini ikiwa ipo chini ya Jeshi la Magereza. Timu hiyo iliwahi kumaliza kwenye nafasi ya pili mara mbili. Ilifanikiwa kufanya hivyo mwaka 2004 na 2008. Endapo Simba na Yanga zisingekuwepo pengine Prisons ingekuwa ina mataji mawili ya ligi kibindoni. Ingefanikiwa kutwaa taji hilo kwa miaka hiyo miwili iliyofanikiwa kumaliza katika nafasi ya pili kwani Simba na Yanga ndizo zilizotwaa mataji hayo na kuinyima nafasi Prisons.

Tusingemfahamu Amissi Tambwe

Simba na Yanga zisingekuwepo pengine tusingewafahamu mastaa kibao. Pengine tusingewafahamu Amissi Tambwe, Kpah Sherman na Emmanuel Okwi. Pengine tusingewafahamu Andrey Coutinho, Geilson Santos ‘Jaja’ na hata Nonda Shaaban ‘Papii’. Kusingekuwa na usajili wa mashindano. Tusingewaona wachezaji magalasha kama kina Komalmbil Keita, Daniel Akufor, Lino Masambo, Patrick Ochieng na wengineo. Kusingekuwa na timu zinazofanya usajili wa kishabiki kama timu hizo kongwe.

Azam ingetwaa mataji matatu ya ligi mpaka sasa

Azam imefanikiwa kumaliza katika nafasi ya pili kwa misimu miwili mfululizo kabla ya kutwaa taji hilo msimu uliopita kwa mara ya kwanza kwenye historia ya timu hiyo. Ilimaliza kama mshindi wa pili msimu wa 2011/12 Simba ilipotwaa ubingwa. Ilimaliza tena kama mshindi wa pili msimu wa 2012/13 Yanga ilipotwaa ubingwa. Azam ilishindwa kutamba kwa misimu hiyo miwili kutokana na ubabe wa Simba na Yanga. Timu hizi zisingekuwepo pengine Azam ingekuwa na mataji matatu kibindoni mpaka sasa. Ingetwaa taji hilo mwaka 2012 na 2013 kabla ya kulitwaa tena mwaka huu.

Rage asingekuwa mbunge

Kuna baadhi ya watu wamekuwa wakizitumia Simba na Yanga kama daraja. Wanazitumia klabu hizi kama ngazi ya kupandia kwenda kwenye mafanikio yao. Miongoni mwa watu hawa ni mwenyekiti wa zamani wa Simba, Ismael Aden Rage. Mwenyekiti huyu aliitumia Simba vizuri kujipatia umaarufu nchini uliomwezesha kushinda ubunge wa jimbo la Tabora mjini kwenye uchaguzi wa mwaka 2010 kwa tiketi ya CCM. Simba iling’arisha jina lake na kumwezesha kushinda kiti hicho ikiwa ni miezi minne tu tangu aliposhinda nafasi ya Uenyekiti kwenye klabu hiyo. Endapo Simba na Yanga zisingekuwepo pengine leo Rage asingekuwa mbunge. Pengine asingepata umaarufu kwa urahisi na kufanikiwa kushinda kiti hicho.

Manji angekuwa mwanasiasa

Mwenyekiti wa sasa wa Yanga, Yusuf Manji alijaribu siasa na mambo hayakumuendea vizuri kisha akaamua kuingia kwenye soka. Alitaka kuwania ubunge mwaka 2005 lakini hakufanikiwa kwenye ndoto yake hiyo. Mwaka mmoja baadaye akaamua kuwa mfadhili wa klabu ya Yanga kabla ya baadaye kuwa Mwenyekiti wa klabu hiyo. Pengine Yanga isingekuwepo Manji asingekata tamaa kwenye siasa. Pengine angewania ubunge mwaka 2010 na kubahatika kushinda. Pengine angewania udiwani mwaka 2010 na kufanikiwa kushinda na kuwa meya wa moja ya Manispaa za Jiji la Dar es Salaam.

Wadhamini wangejazana Kagera, Mtibwa

Yanga na Simba ndizo timu zenye udhamini mkubwa zaidi achilia mbali ule wa Azam iliyopata msimu huu kutoka NMB. Timu hizi mbili zinapewa Sh500Milioni kila moja kwa mwaka na mdhamini wao, bia ya Kilimanjaro. Endapo Simba na Yanga zisingekuwepo pengine udhamini huo ungeenda kwa timu kongwe za Mtibwa Sugar na Kagera Sugar. Hizi ndizo timu ambazo si za jeshi na zimefanikiwa kucheza ligi kuu kwa miaka mingi sasa. Timu hizi zingekuwa ndiyo timu kubwa na kupata udhamini wa maana.

Ubingwa wa bara usingekuwa wa timu mbili

Yanga inaongoza kwa kutwaa taji la Ligi Kuu Bara, imelitwaa mara 24. Simba nayo si haba, imelitwaa mara 18 katika kipindi cha miaka 46 sasa. Klabu hizo mbili zimeigeuza ligi kama ya kwao. Zinapokezana ubingwa kwa kadiri zinavyojisikia. Mtibwa Sugar ndiyo inayozifuatia timu hizi kwa kutwaa mataji mengi ya ligi, imetwaa mara mbili pekee. Endapo timu hizi zisingekuwepo ubingwa huo usingekuwa wa timu mbili tu. Kila timu ingekuwa na fursa sawa ya kunyakua ubingwa.

Azam ingetwaa taji la Kagame

Nyota za timu nyingi nchini zimefunikwa na Simba na Yanga. Azam ilicheza fainali ya Kombe la Kagame mwaka 2012 na kufungwa mabao 2-0 na Yanga iliyotwaa ubingwa huo. Azam ilijitahidi kuhakikisha inatwaa taji hilo kwa mara ya kwanza lakini ndoto yao hiyo ilizimwa na Yanga iliyoonekana kuwa moto wa kuotea mbali kwa kipindi hicho. Endapo Simba na Yanga zisingekuwepo pengine Azam ingekuwa ina Kombe la Kagame kibindoni kwa sasa kwani Yanga ndiyo iliyozima ndoto hizo.

Majimaji isingeshuka daraja

Moja ya timu iliyoonekana kuleta upinzani mkubwa kwenye soka la Tanzania ni Majimaji ya Songea. Timu hii ilikuwa ikiungwa mkono na wakazi wa mji huo na kufanikiwa kufanya vizuri kwenye ligi kabla ya kuporomoka baadaye na kushuka daraja. Simba na Yanga kama zilivyofanya kwa Tukuyu, ziligawana mastaa wa timu hiyo na kuiacha ikiwa na kikosi dhaifu hivyo kushuka daraja. Endapo Simba na Yanga zisingekuwepo pengine Majimaji ingekuwa inacheza ligi kuu hadi hii leo.

ADVERTISEMENT
ADVERTISEMENT