In Summary
  • Mfano mzuri ni mwaka 1974, mchezo kati ya watani wa jadi, Simba na Yanga. Mchezo huo ulihamishwa kutoka jijini Dar es Salaam, Uwanja wa Taifa (wa zamani) hadi Mwanza (Uwanja wa Nyamagana), kipindi ligi ikichezwa kwa mtindo vituo mbalimbali na mwishowe kulikuwa na mchezo wa fainali.

MIAKA ya nyuma, imewahi kutokea mara kadhaa michezo ya Ligi Kuu ikihamishwa kutoka uwanja mmoja hadi mwingine. Hii ilikuwa ni kutokana na sababu mbalimbali. Ilikuwa ni kawaida sana na ikapata mashiko kweli.

Mfano mzuri ni mwaka 1974, mchezo kati ya watani wa jadi, Simba na Yanga. Mchezo huo ulihamishwa kutoka jijini Dar es Salaam, Uwanja wa Taifa (wa zamani) hadi Mwanza (Uwanja wa Nyamagana), kipindi ligi ikichezwa kwa mtindo vituo mbalimbali na mwishowe kulikuwa na mchezo wa fainali.

Ikapita miaka kadhaa huku michezo mingi ikichezwa kwenye viwanja vya timu husika kabla ya katikati ya miaka ya 1990 kurudi tena kwa michezo kuhamishwa vituo.

Mchezo mwingine ni ule wa mwishoni mwa miaka ya 90. Simba na Yanga zilicheza michezo miwili ya fainali kumtafuta bingwa wa Ligi Kuu Bara na mchezo wa kwanza ulifanyika Uwanja wa Sokoine, Mbeya, timu hizo zikitoka sare ya 1-1, kisha kurudiana mjini Dodoma kwenye Uwanja wa Jamuhusi na Yanga kushinda bao 1-0

Hata hivyo, kulikuwa na sababu za msingi za kufanyika kwa michezo hiyo kwa mtindo huo na taarifa za michezo hiyo zilitolewa mapema.

Hata wakati wa ukarabati wa Uwanja wa Uhuru miaka ya hivi karibuni, baadhi ya timu za Ligi Kuu zilizotumia uwanja huo, ilibidi zihamie viwanja vingine ili kupisha ukarabati huo.

Simba na Yanga zenyewe zilikimbilia Morogoro, huku JKT Ruvu na Ashanti zikikimbilia mikoa ya Kilimanjaro na Arusha.

Pia zipo timu nyingine zilifanya hivyo kupisha ukarabati wa viwanja vyao, mfano Kagera Sugar ilihamia Shinyanga kutumia Uwanja wa Kambarage kupisha matengenezo ya Uwanja wa Kaitaba, hizi zote zilikuwa sababu zilizofahamika na zenye mashiko.

Ukaja utaratibu mwingine, timu zilizomiliki viwanja vyao vidogo vinavyochukua watazamaji wasiozidi 2000, kama Mtibwa Sugar, Mwadui FC, Ruvu Shooting na Azam FC zikawa zinatumia viwanja viwili vya nyumbani.

Mtibwa wakitumia Uwanja wa Manungu na Jamhuri Morogoro, Mwadui ule wa Kambarage, Shinyanga Mjini, huku Ruvu Shooting, Azam FC na JKT Tanzania wakitumia Uwanja wa Taifa kama kiwanja chao cha pili cha nyumbani.

Walifanya hivi hasa kwa michezo dhidi ya timu mbili za Simba na Yanga sababu kubwa ikiwa ni kuwapa nafasi mashabiki wengi kuingia uwanjani huku mapato yakiwa yanalengwa zaidi pamoja na usalama.

Baada ya hapo ukaja mtindo wa timu kucheza na kanuni za ligi. Kwa mfano, msimu wa 2016/17 Ndanda iliombwa kuhamishia mchezo wao dhidi ya Yanga kwenye Uwanja wa Taifa badala ya Nangwanda Sijaona ulioko Mtwara kwa makubaliano maalaumu ikiwamo wachezaji wao kulipwa posho na hela nyingine Dar es Salaam.

Sasa umekuja utaratibu mpya kabisa na timu zinaweza kuchagua viwanja viwili vya nyumbani kutegemea na zinavyojisikia tena katikati ya msimu. Mfano ni Azam baada ya kubadilisha uwanja wa nyumbani kutoka Chamazi hadi Taifa kwa mechi za Simba na Yanga tu. JKT Ruvu nao wamehama kutoka Taifa hadi Uwanja wa Mkwakwani, Tanga kwa michezo dhidi ya Simba na Yanga, huku African Lyon ikichagua viwanja vya nyumbani vya Sheikh Amri Abeid Kaluta cha Arusha na Lake Tanganyika dhidi ya Yanga na Simba.

Sababu kubwa ni kupata mapato kama ilivyo kwa sasa timu mwenyeji ndiyo yenye haki ya kuchukua mapato yote ya mchezo husika. Kwa utaratibu huu ambao inasemekana upo kikanuni timu inaweza kubadili uwanja ili mradi tu kuwe na taarifa ya muda wa kutosha ingawa hata hivyo mabadiliko haya mwanzo yalipingwa vikali na timu za Simba na Yanga lakini bado msimamo wa Bodi ya Ligi ulibaki palepale.

Hata hivyo, eneo hili kwa jicho la upembuzi linaona hii sio sahihi kwani utaratibu wowote unatakiwa kufanywa kwa kwa kufuata misingi.

Ni kawaida kabla ya msimu kuanza timu huwa zinapewa nafasi ya kuchagua viwanja watakavyotumia kwenye michezo yao ya nyumbani, kisha bodi ya ligi hutuma watalaamu wake kuvichunguza viwanja hivyo kama vinakidhi matakwa ya michezo ya ligi itakayochezwa ndipo waruhusu kuvitumia viwanja hivyo.

Utambuzi wa viwanja hivyo mapema husaidia kwa kiasi kikubwa kuzifanya klabu husika kutengeneza bajeti mapema za usafiri, sehemu za kulala, kufanya mazoezi na mipango yote ya maandalizi yanayosaidia kuifanya michezo hiyo kuwa ya ushindani mkubwa.

Sidhani kama itakuwa sahihi sasa kwa timu moja kuwa na viwanja zaidi ya viwili vya nyumbani. Kuwa na kiwanja kimoja tu ndio utaratibu mzuri na unaoleta maana kamili ya ligi.

ADVERTISEMENT