In Summary
  • Usajili ni jambo muhimu sana. Kwa klabu inafahamu umuhimu wa usajili, ni wazi inafanya usajili wa wachezaji wasiozidi 23. Hata hivyo, kwa timu zetu hizi, huwa zinasajili tuu wachezaji hata 30. Ndipo najiuliza, wachezaji 30 ni wa nini hasa kwa klabu ambazo mishahara yao ipo juu na wakati huo huo wanataka ufanisi.

Ndugu zangu, natumai ni wazima. Ikiwa ni wiki ya mwisho ya mwezi Novemba tukikaribia kuukaribisha mwezi wa mwisho wa mwaka huu 2018, tumshukuru Mungu kwa kuweza kutufikisha hapa.

Leo nazungumzia usajili hasa kwa klabu zetu kubwa za ukanda huu wa Amfrika Mashariki za Simba, Yanga, Gor Mahia na AFC Leopards.

Ndio klabu zinazovuma katika ligi za ukanda huu, Ligi Kuu ya Kenya (KPL) na ile ya Tanzania (TPL).

Ligi Kuu ya Kenya imemalizika majuzi tu na inatarajiwa kuanza tena Desemba 8, huku Kenya ikiwa mbioni kufanya mabadiliko ya ratiba ili iendane na ile ya kalenda ya Shirikisho la Soka Duniani (Fifa).

Wakati Kenya ikisubiria ligi hiyo, huku Tanzania ikiwa ligi bado inaendelea, suala zima la usajili ndilo gumzo kwa sasa.

Kwa Tanzania, dirisha dogo la usajili tayari limefunguliwa na timu zinafanya kazi ya kutafuta wachezaji muhimu.

Usajili ni jambo muhimu sana. Kwa klabu inafahamu umuhimu wa usajili, ni wazi inafanya usajili wa wachezaji wasiozidi 23. Hata hivyo, kwa timu zetu hizi, huwa zinasajili tuu wachezaji hata 30. Ndipo najiuliza, wachezaji 30 ni wa nini hasa kwa klabu ambazo mishahara yao ipo juu na wakati huo huo wanataka ufanisi.

Ni afadhali ukafanya usajili wa wachezaji wawili kila nafasi wenye uwezo ambao utaweza kuwalipa, badala ya kuwa na wachezaji zaidi ya 30 unaowalipa tu lakini hawana lolote la kusaidia timu. Kwa nini usajili mchezaji ambaye unamlipa tu mshahara na hachezi kabisa?

Ndipo nasema. Ni wajibu kwa viongozi wa klabu hizi, kuzingatia zaidi usajili, kwani hakuna haja ya kusajili wachezaji wasio na msaada, kisha unawalipa pesa ndefu. Ni wazi timu zetu hizi hazina miundombinu ya kuziendesha, hii ni kwa sababu ya wengi hawa, hawafahamu lolote na hawataki kuuliza ili waelimishwe.

Pili, ni kwa baadhi ya viongozi kujiangalia wao kuliko maendeleo ya soka letu. Kiongozi analazimisha mchezaji fulani ndio apewe kandarasi, kisha pesa za usajili agawane naye.

Hii tabia iko pia kwa baadhi ya makocha hasa Kenya, anaingia mkataba na mchezaji atamsajili, lakini kwenye malipo atachukua asilimia 20. Mambo kama haya ndio yanayolimaliza soka letu hasa kwa klabu hizi kubwa,

Soka halitaki kubahatisha wala urafiki. Kutokana na ushindani, inabidi ufanyike usajili wa ukweli.

Kenya kwa usajili unaendelea na nionavyo mimi ni ule wa kujuana. Jambo hili si la kufurahia hata kidogo

Kwa nini timu zisifanye usajili kwa kuzingatia viwango vya wachezaji na sio kwa kuangaliana sura, huyu mtoto wa kaka yake fulani, mtoto wa dada yangu au wa bosi wangu.

Usajili wa hivi, haufai hasa kama tunataka kukuza soka letu. Hapo ndipo unakuta viwango vya klabu vipo chini kwa sababu tu alisajiliwa mtoto wa dada yake kiongozi.

Ndio, hakuna shida kuwasajili watoto wa shangazi yako, mpe kila kitu, lakini je, anaujua mpira? Ana kiwango cha kuichezea timu husika?

Nawakumbusha tu, makocha na viongozi wa klabu hizi, acheni kujiaibisha. Mkumbuke mashabiki wanachotaka ni ushindi, tena sio wa kubahatishabahatisha. Hii inamaanisha, ni lazima kazi ifanyike.

Angalia kwa mfano Manchester City, usajili unaofanywa na Kocha Pep Guardiolla ni hatari.

Ukiangalia viwango vya nyota wa timu hiyo na wale wa Manchester United, utaona tofauti. Man United wanapotea katika ramani ya soka.

Ni afadhali utumie pesa nyingi kusajili wachezaji wa viwango vya hali ya juu kuliko kujiweka kitanzi.

Isifikie kipindi hadio mashabiki wainue mabongo kushinikiza kocha aondoke au uongozi uondoke, kisa tu ni usajili mbovu uliofanyika.

Hata hivyo, ni wazi suala la usajili ni la kocha, ifikie mahala aachiwe kocha mwenyewe ndio ahangaikie usajili kama wafanyavyo kule Ulaya. Inakera sana kuona klabu zetu kila msimu zinasajili wachezaji zaidi ya kumi. Kusajili hakukatazwi, lakini usajili wa rundo la wachezji, inatatiza kidogo.

Hii inaonyesha jinsi klabu zetu hazina mikakati ya usajili. Zinasajili tu ilimradi. Wakati mwingine zinasajili kwa ushindani kisa tu flani kamtaka mchezji huyu, mwingine anaibuka na kumtaka.

Baadaye utasikia mchezaji katemwa kutokana na kiwango lakini ndiye huyo aliyekuwa akigombewa kwenye dirisha la usajili.

Ni aibu. Kwa nini hakuwepo na maskauti wa kuangalia wachezaji na kutoa ripoti badala yake viongozi na makocha wanaibuka tu na wachezaji wao wakiwaaminisha mashabiki ni mchezaji wa kiwango, matokeo yake anaishia benchi?

Tubadilikeni.

ADVERTISEMENT